Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Masalia ya samaki yatumika kutengeneza chakula cha mbwa Ureno 

Ngozi ya salmoni na magamba yake yanavirutubisho muhimu vya Omega 3ambayo husaidia manyoya ya mbwa na paka kuwa na afya
Sancho Pancho
Ngozi ya salmoni na magamba yake yanavirutubisho muhimu vya Omega 3ambayo husaidia manyoya ya mbwa na paka kuwa na afya

Masalia ya samaki yatumika kutengeneza chakula cha mbwa Ureno 

Tabianchi na mazingira

Hakuna shaka kwamba utupaji na upotevu wa chakula, umekuwa ukidhoofisha uendelevu wa mifumo yetu ya chakula. Katika jitihada za kukabiliana na hili, baadhi ya makampuni ya biashara ndogo ndogo duniani kote yanaweka mkazo katika mbinu mpya endelevu za usimamizi wa taka.

UN News imetembelea mradi mmoja wa aina hiyo hivi karibuni katika mji mkuu wa Ureno, Lisbon, ambako mkutano wa Umoja wa Mataifa wa bahari, utafanyika, mwishoni mwa mwezi huu wa Juni.

 

Kampuni ya biashara ya chakula cha mbwa kiitwacho Sancho Pancho ilianzishwa na Mrusi Daria Demidenko, ambaye alihamia Ureno mwaka wa 2015.

 

Wazo lake bora na la busara la biashara linahusisha kugeuza mabaki za samaki wabichi, kuwa chakula cha mbwa.

 

Bi. Demidenko, alianzisha biashara yake kwa kushirikiana na mkahawa mmoja wa  Kijapani na baadhi ya masoko ya samaki katika mji mkuu wa Ureno.

 

Anatumia sehemu sa Samaki ambazo haziwekwi mezani kwa mlo na haziwezi kutumika wakati wa kuweka kwenye sahani mlo wa sushi na sashimi.

 

Sancho Panchoi biashara ndogo ambayo inabadili mabaki ya samaki kuwa vitafunwa vya mbwa. Bisahara hiyo iko Lisbon Ureno
UN News/Leda Letra
Sancho Panchoi biashara ndogo ambayo inabadili mabaki ya samaki kuwa vitafunwa vya mbwa. Bisahara hiyo iko Lisbon Ureno

Kudhibiti upotevu wa chakula

 

 

Kila siku, pauni na pauni za vichwa vya samaki, mifupa, na ngozi huishia kwenye mapipa ya takataka, lakini Bi. Demidenko amefanya mageuzi katika mbinu ya upotevu huo wa chakula, kwa kushirikiana na Sekai Sushi Bar, mgahawa wa Kijapani uliopo katikati mwa kitongoji cha Santos.

 

Kila siku, mgahawa hupokea karibu kilo 10 za samaki aina ya lax, Jodari au tuna na samaki nyeupe.

 

Mpishi wa Sushi Sunil Basnet anasafisha na kuandaa mlo wa samaki hao ikiwemo, mabaki yasiyohitajika kuliwa yenye uzito wa kilo tatu Samaki waliovuliwa karibu na pwani ya Ureno.

 

Mmiliki wa Sekai, Edilson Neves, ameileza UN News kwamba, kwa wastani, asilimia 30 ya samaki hawawezi kutumiwa kama chakula na mgahawa huo.

 

“Mgongo, sehemu ya mkia, kingo, mapezi ya pembeni, sehemu inayoungana na tumbo, baadhi ya sehemu za samaki ambazo ni kali, zenye nyuzi nyingi na ngozi pia, tunaishia kutozitumia. Hii ni asilimia 30 hadi 40 ambayo ingepotea, tunaishia kuitumia tena kupitia Sancho Pancho”.

 

Asilimia 30 hadi 40 ya samaki huishia kwenye mapipa ya taka, Sancho Pancho hutumia mabaki hayo.
Sancho Pancho
Asilimia 30 hadi 40 ya samaki huishia kwenye mapipa ya taka, Sancho Pancho hutumia mabaki hayo.

Vitafunwa vyenye lishe

 

 

Jina la biashara ya Bi. Demidenko, linarejelea mhusika Sancho Panza, kutoka kwenye riwaya mashuhuri ya Miguel de Cervantes, Dom Quixote, na pia ni kumuenzi binafsi mbwa wake mmoja, anayeitwa Pancho.

 

Ameiambia UN News, kuhusu baadhi ya viambato na vyakula maalum, alivyoweza kupata kutokana na kutumia mabaki hayo ya salami.

 

"Vidakuzi hivi vinatengenezwa na aina hii ya samaki nyeupe, ambayo sisi hupika kwanza, na kisha kuponda, ili mifupa iwe laini zaidi", alisema, akionyesha moja ya vitafunwa vya mbwa.

 

"Tunaviponda, tunachanganya na unga na kutengeneza keki. Lakini pia kuna aina nyingine za taka, kama vile ngozi nyeupe ya samaki au lax, ambayo unaweza kuipunguza maji. Aina hii ya vitafunwa huingia kwenye mashine, hukaa kwa saa 20 katika joto la nyuzi joto 70˚C na kisha hutoka zikiwa kavu zaidi, na tunazikata vipande vipande na kuvifanya kama chips ndogo, vijipande vidogovidogo vya ngozi ya lax au Salmon.”

 

Nchi za Scandinavia ziko mstari wa mbele

 

 

Kando na kuchukua mabaki kwenye mkahawa wa Sekai, Daria ana ushirikiano na migahawa mingine na masoko ya samaki huko Lisbon.

 

Anakusanya takriban kilo 25 za mabaki ya samaki kwa wiki. Mpango wake umemwagiwa sifa kemkem kutoka kwa Márcio Castro de Souza mtaalamu mkuu wa uvuvi wa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO, lenye makao yake makuu mjini Roma Italia.

 

Mabaki ya samaki weupe Daria hutumia kutengeneza vitafunwa vilivyochanganywa na viazi vitamu
Sancho Pancho
Mabaki ya samaki weupe Daria hutumia kutengeneza vitafunwa vilivyochanganywa na viazi vitamu

“Mradi huu ni wa kuvutia sana na kwa kweli tumeona, sio tu katika ngazi ya viwanda, lakini pia mifano midogo ya jinsi ya kupunguza upotevu wa samaki. Tayari kuna viwanda kadhaa vya kuzalisha samaki aina ya salmoni katika nchi za Scandinavia ambavyo tayari vimefikia kiwango cha kutumia asilimia 100 ya samaki wote. Hawapotezi chochote. Wanatengeneza minofu, wanatumia macho kutengeneza mbolea au kuzalisha mafuta muhimu, kwa hiyo tayari kuna uzalishaji mzima unaolenga kutopoteza chochote”, amefafanua.

 

Mipango mingine duniani kote ni pamoja na kutumia ngozi ya samaki kutengeneza bidhaa zinazoweza kuvaliwa, kutumia mizani ya samaki katika utengenezaji wa lipstick; na wino wa ngisi kupaka rangi chakula kama tambi.

 

Ufahamu wa watumiaji

 

 

Vitafunwa vilivyotengenezwa kwa ngozi ya lax au salmoni vina mafuta mengi ya samaki yanayojulikana kama omega 3, ambayo husaidia kudumisha afya ya ngozi na manyoya ya wanyama kipenzi kama mbwa na paka.

 

Mbali na kutumia tena mabaki ya Samaki, chapa ya Daria hutengeneza vitafunwa kutokana na mabaki ya nyama ya sungura na nyama ya nguruwe.

 

Mwanzilishi wa Sancho Pancho anasema tayari ameweza kuongeza ufahamu wa wateja, juu ya athari zinazosababishwa na upotevu wa chakula.

 

"Baadhi ya wateja wametuambia kwamba wanajifunza kutoka kwetu, na sasa wanaenda kwenye masoko ya samaki na bucha hapa Ureno na pia kuchukua taka za chakula nyumbani sasa wenyewe. Hawatengenezi vitafunwa vya kuuza, lakini wanaweza kuwatengenezea mbwa, au paka, chakula wao wenyewe.”

 

Kupunguza nusu ya upotevu wa chakula duniani ifikapo 2030 ni moja ya malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa.

 

Lengo namba 14 pia linahusisha udhibiti endelevu wa viumbe vya baharini, Kuokoa bahari na kulinda mustakbali ndio kauli mbiu ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa bahari, unaofanyika katika mji mkuu wa Ureno Lisbon kuanzia Juni 27 hadi Julai 1.