Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Côte d'Ivoire yakaribisha familia zinazorejea kutoka ukimbizini

Wakimbizi kutoka Côte d'Ivoire wakipungia mikono ndugu na jamaa zao wanaowasubiri  chombo chao kitie nanga Côte d'Ivoire kikitokea Liberia
© UNHCR/Colin Delfosse
Wakimbizi kutoka Côte d'Ivoire wakipungia mikono ndugu na jamaa zao wanaowasubiri chombo chao kitie nanga Côte d'Ivoire kikitokea Liberia

Côte d'Ivoire yakaribisha familia zinazorejea kutoka ukimbizini

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi, ameadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani nchini Côte d'Ivoire, pamoja na wakimbizi wa zamani ambao wamerejea nyumbani kabla ya kumalizika rasmi kwa hadhi ya ukimbizi kwa raia hao baadaye mwezi huu. 

Mchakato wa kukomesha rasmi hadhi ya ukimbizi kwa wakimbizi wa Côte d'Ivoire utaanza kutekelezwa tarehe 30 mwezi huu wa Juni. Kusitishwa kwa hadhi ya ukimbizi kunafuatia ufikiaji wa amani dhidi ya miongo miwili ya migogoro ya mara kwa mara ya wenyewe kwa wenyewe na ukosefu wa utulivu wa kisiasa katika taifa hilo la Afrika Magharibi. 

Utatuzi wa mzozo ambao uliwalazimu zaidi ya watu 300,000 kukimbilia nchi jirani na kwingineko ni jambo la kukaribisha huku kukiwa na hali inayoongezeka ya kimataifa ya kulazimishwa kuhama makazi yao. Mwezi uliopita, UNHCR ilisema vita ya Ukraine na migogoro mingine inayoendelea ilisukuma idadi ya watu wanaolazimika kukimbia migogoro na mateso duniani kote zaidi ya milioni 100 kwa mara ya kwanza. 

Katika sherehe mjini Abidjan iliyoandaliwa na Rais wa Jamhuri ya Côte d'Ivoire, Alassane Ouattara, na iliyoshirikisha wawakilishi wa kitaifa na mabalozi kutoka nchi zilizowahifadhi wakimbizi wa Côte d'Ivoire, Kamishna Mkuu amekutana na familia za wakimbizi wa zamani na kuwatakia heri watakaporejea nyumbani. 

"Kwa sisi tulioko UNHCR, hakuna kitu kizuri kama kushuhudia mwisho wa uhamisho. Baada ya miongo miwili, wakimbizi wa Ivory Coast wanaweza kurudi nyumbani salama na kwa heshima. Wanajivunia raia wa Ivory Coast – wanaoishi na kufanya kazi katika jumuiya zao au katika nchi jirani,” Grandi amesema akiongeza kwa kusema, “nilifurahi kutumia Jumamosi na wakimbizi wa Côte d'Ivoire kurudi nyumbani. Kurejea kwa mamia ya maelfu ya raia wa Côte d'Ivoire kunaonesha kwa  eneo hilo - na ulimwengu - kile kinachowezekana wakati kuna nia ya kisiasa ya kukomesha ghasia na ushirikiano wa kweli kati ya mataifa."  

Chini ya masharti ya vifungu vya kusitisha hadhi ya ukimbizi, nchi zinazohifadhi wakimbizi wa Côte d'Ivoire zinahimizwa kuwezesha urejeshwaji wao kwa hiari au kwa wale watu wachache wa Côte d'Ivoire ambao wamechagua kubaki, kuwezesha ushirikiano wa ndani, upatikanaji wa ukaazi wa kudumu na uraia. 

Raia wa Côte d'Ivoire waliikimbia nchi katika mawimbi mawili tofauti kufuatia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kati ya 2002 na 2007, na 2011 na 2012. Maelfu ya watu pia walikimbilia nchi jirani mwaka 2020 huku kukiwa na hofu ya ghasia zilizohusishwa na uchaguzi wa rais na wabunge. 

Zaidi ya wakimbizi 310,000 wa Côte d'Ivoire, au asilimia 96 ya wote waliosajiliwa kote Afrika Magharibi, wamechagua kurejea nyumbani. Zaidi ya watu 11,000 kati ya 14,000 waliorejea mwaka huu, wamewasili kutoka nchi jirani ya Liberia, ambako UNHCR inaandaa usafiri wa kila wiki kwa raia wa Côte d'Ivoire wanaotaka kurejea nyumbani. Raia wa Côte d'Ivoire wanaorejea nyumbani wanaweza kukabiliwa na changamoto fulani wanaporejea na watahitaji usaidizi endelevu, lakini Serikali imejitolea kuunga mkono kujumuishwa kwao na jumuiya za wenyeji zinawakaribisha tena. 

Mnamo tarehe 18 Juni, Grandi alisafiri hadi mpaka wa Liberia kuandamana na wakimbizi wa Côte d'Ivoire katika hatua ya mwisho ya safari yao ya kurudi nyumbani kwa feri kuvuka mto unaoashiria mpaka kati ya nchi hizo mbili. Wakati wa kuvuka, mamlaka ya Liberia iliwasilisha rasmi vyeti vya kuzaliwa kwa wenzao wa Côte d'Ivoire ili kuhakikisha wanaorejea wanaweza kuandikisha watoto wao shuleni, kupata vitambulisho vya kitaifa na kujiandikisha kupiga kura. 

Kamishna Mkuu aliahidi kuhusu UNHCR kuendelea kuiunga mkono Côte d'Ivoire na nchi zilizowahifadhi wakimbizi wa nchi hiyo kutekeleza vifungu vya kumaliza hadhi ya ukimbizu na kusaidia wale wote wanaotaka kurejea nyumbani.