Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mambo 5 ya kufahamu kuhusu mkutano wa Bahari wa UN, fursa ya kuokoa mfumo mkubwa kabisa wa ikolojia 

Viwavi wa baharini, miongoni mwa milo ya siku zijazo ingawa kwa sasa ni mlo pendwa kwa nchi za Asia
FAO
Viwavi wa baharini, miongoni mwa milo ya siku zijazo ingawa kwa sasa ni mlo pendwa kwa nchi za Asia

Mambo 5 ya kufahamu kuhusu mkutano wa Bahari wa UN, fursa ya kuokoa mfumo mkubwa kabisa wa ikolojia 

Tabianchi na mazingira

Bahari ndiyo mfumo mkubwa zaidi wa ikolojia wa sayari dunia, unaodhibiti hali ya hewa, na kutoa uwezo wa maisha kwa mabilioni ya watu.  

 

Boti zikiwa zimeweka nanga karibu na nadari ya Mombasa, Kenya.
© Unsplash/Prolific Ke
Boti zikiwa zimeweka nanga karibu na nadari ya Mombasa, Kenya.

Lakini afya yake iko hatarini. Kongamano la pili la Umoja wa Mataifa la bahari, linalotarajiwa kufanyika mwezi huu wa Juni, litakuwa fursa muhimu ya kurekebisha uharibifu ambao wanadamu wanaendelea kusababishia viumbe na maisha ya baharini. 

Huku wajumbe kutoka nchi wanachama, mashirika yasiyo ya kiserikali, na vyuo vikuu wakihudhuria, pamoja na wafanyabiashara wanaotafuta njia za kuendeleza uchumi wa bluu, kuna matumaini kwamba tukio hilo, litakalofanyika katika jiji la Ureno la Lisbon kati ya tarehe 27 Juni na tarehe 1 Julai, litaashiria enzi mpya kwa Bahari. 

1.Ni wakati wa kujikita na suluhu 

Mkutano wa kwanza, uliofanyika mwaka 2017, ulionekana kama tahadhari ya kuleta mabadiliko ulimwengu kuhusu changamoto za bahari.  

Kwa mujibu wa Peter Thomson, mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu bahari, mkutano wa Lisbon "utahusu kutoa suluhu kwa matatizo hayo". 

Mkutano huo umeandaliwa ili kutoa nafasi kwa jumuiya ya kimataifa kushinikiza kupitishwa kwa ufumbuzi wa ubunifu, unaotegemea sayansi kwa usimamizi endelevu wa bahari, ikiwa ni pamoja na kupambana na tindikali kwenye maji, uchafuzi wa mazingira, uvuvi haramu na kupoteza makazi na viumbe hai. 

Mkutano wa mwaka huu pia utaamua kiwango cha matarajio ya muongo wa Umoja wa Mataifa wa sayansi ya bahari kwa maendeleo endelevu wa kuanzia (2021-2030).  

Muongo huo utakuwa mada kuu katika mkutano huo, na utakuwa mada ya matukio kadhaa muhimu, kutanabaisha kuhusu bahari yenye afya na endelevu zaidi. 

Umoja wa Mataifa umeweka malengo 10 yanayohusiana na bahari yatakayofikiwa katika muongo huu, kama sehemu ya Ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu, ambao ni mwongozo wa shirika la Umoja wa Mataifa kwa mustakabali wa haki kwa watu na sayari.  

Muongozo huo unajumuisha hatua za kuzuia na kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuongezeka kwa tindikali, kulinda mifumo ya ikolojia, kudhibiti uvuvi, na kuongeza maarifa ya kisayansi.  

Katika mkutano huo, midahalo shirikishi itazingatia jinsi ya kushughulikia mengi ya masuala haya.

Samaki wakiogelea katika Bahari ya Sham
© Ocean Image Bank/Brook Peters
Samaki wakiogelea katika Bahari ya Sham

Jukumu la vijana litakuwa mstari wa mbele huko Lisbon, wakiwa ni wajasiriamali wachanga wanaofanya kazi katika masuala ya ubunifu, suluhu za kisayansi kwa changamoto muhimu, ni sehemu muhimu ya mazungumzo. 

Kuanzia tarehe 24 hadi 26 Juni, watashiriki katika jukwaa la vijana na ubunifu, jukwaa linalolenga kusaidia wafanyabiashara wachanga na wavumbuzi kuongeza juhudi zao, miradi na maoni yao, kwa kutoa mafunzo ya kitaalamu, na kuwaunganisha na washauri, wawekezaji, sekta binafsi na maafisa wa serikali. 

Kongamano hilo pia litajumuisha “Mtandao wa ubunifu” ambapo timu za washiriki watano zitafanya kazi pamoja kuunda na kupendekeza suluhu mpya kwa ajili ya bahari. 

2.Mtihani ni mkubwa 

Bahari hutupatia sote hewa ya oksijeni, chakula, na riziki. Inakuza bayoanuwai isiyofikirika, na inasaidia moja kwa moja ustawi wa binadamu, kupitia rasilimali za chakula na nishati. 

Kando na kuwa chanzo cha uhai, bahari hutuliza hali ya hewa na kuhifadhi hewa ukaa, ikifanya kazi kama beseni kubwa la gesi chafuzi. 

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, karibu watu milioni 680 wanaishi katika maeneo ya ukanda wa pwani, na kuongezeka hadi karibu bilioni moja ifikapo mwaka 2050. 

Zaidi ya hayo, uchanganuzi wa hivi karibuni unakadiria kuwa watu milioni 40 wataajiriwa na tasnia zinazotegemea bahari kufikia mwisho wa muongo huu. 

3.Kenya na Ureno kuangaziwa 

Ingawa Kongamano hilo linafanyika nchini Ureno, linaandaliwa kwa pamoja na serikali ya Kenya, ambapo asilimia 65 ya wakazi wa pwani wanaishi katika maeneo ya mashambani, wakijishughulisha zaidi na uvuvi, kilimo, na uchimbaji madini kwa ajili ya maisha yao. 

Mvuvi nchini Kenya ambaye anategemea samaki kama mlo na pia kujipatia kipato
© UNDP/Amunga Eshuchi
Mvuvi nchini Kenya ambaye anategemea samaki kama mlo na pia kujipatia kipato

 

Kwa Bernadette Loloju, mkazi wa Kaunti ya Samburu, Kenya, bahari ni muhimu kwa watu wa nchi yake kwa sababu inawaruhusu kupata bidhaa nyingi wanazohitaji. “Bahari ina viumbe hai vingi wakiwemo samaki. Pia inatupa chakula. Tunapoenda katika jiji la Mombasa, tunafurahia ufuo wa bahari na kuogelea, na hivyo kuongeza furaha yetu”. 

Nzambi Matee, mshindi wa tuzo ya shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP ya kijana bingwa wa dunia, ana maono sawa. Nzambi anaishi Nairobi, Kenya, na ndiye mwanzilishi wa Gjenge Makers, kampuni ambayo inazalisha vifaa endelevu vya ujenzi vya bei nafuu vilivyotengenezwa kwa taka za plastiki zilizorejelewa. 

Bi. Matee anachukua taka za plastiki kutoka baharini, zinazovuliwa na wavuvi, na kuzigeuza kuwa matofali ya lami "kazi yangu ya kuchakata taka za plastiki kutoka baharini imeniwezesha kuajiri zaidi ya vijana na wanawake 113, ambao kwa pamoja wamezalisha matofali 300,000. Ninapata riziki yangu kutoka kwa bahari, na kwa hivyo bahari ni uhai kwangu,” amesema. 

Shauku ya bahari inashirikiwa na Ureno pia, nchi kubwa zaidi la pwani ambayo ni mwanachama wa Muungano wa Ulaya yenye takriban kilomita milioni nne za ukanda wa pwani unaoendelea, na kwa hivyo, nchi ambayo ina jukumu kubwa katika bonde la Atlantiki. 

Ufukwe wa Nazaré Ureno.
© Unsplash/Tamas Tuzes-Katai
Ufukwe wa Nazaré Ureno.

 

"Matarajio yetu kwa mkutano huo wa Umoja wa Mataifa wa bahari ni kwamba utakuwa mkutano kuhusu hatua na sio kujitolea tu," anasema Catarina Grilo, mkurugenzi wa uhifadhi na sera katika Associação Natureza Ureno (ANP), shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi sanjari na mfuko wa wanyamapori duniani (WWF). 

ANP inaendesha miradi kadhaa katika maeneo ya ulinzi wa baharini, uvuvi endelevu, na uhifadhi wa bahari. 

"Mkutano uliopita huko New York ulikuwa wakati mzuri sana wa kuongeza ufahamu juu ya jukumu la bahari kwa ustawi wa wanadamu. Wakati huo tulikuwa na ahadi nyingi za hiari kutoka kwa nchi wanachama na mashirika yasiyo ya serikali, lakini sasa ni wakati wa kutoka kwenye maneno kwenda kwenye vitendo”. 

4.Bahari na hali ya hewa duniani vina uhusiano wa ndani 

Bahari na hali ya hewa ya kimataifa huingiliana kwa njia nyingi. Wakati mzozo wa mabadiliko ya tabianchi unaendelea kuwa tishio kubwa, kuna baadhi ya takwimu muhimu za wanasayansi wanaangalia kwa karibu. 

Kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya mabadiliko ya tabianchi kutoka shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO, vina vya wastani vya bahari viliongezeka kwa wastani wa milimita 4.5 kwa mwaka kati ya 2013 na 2021, kutokana na kuyeyuka kwa barafu kwa kasi inayoongezeka. 

Bahari hufyonza karibu asilimia 23 ya hewa ukaa au CO2 inayotokana na shughuli za binadamu, na inapotokea athari za kemikali hufanyika, na kutia tindikali kwenye maji ya bahari.  

Hiyo inaweka mazingira ya bahari katika hatari na, jinsi maji yanavyozidi kuwa na tindikali, ndivyo hewa ukaa au CO2 inavyoweza kunyonya. 

Samuel Collins, meneja wa mradi katika wakfu wa Oceano Azul, mjini Lisbon, anaamini kwamba mkutano huo utatumika kama daraja la kuelekea mkutano wa COP27 wa mabadiliko ya tabianchi, unaotarajiwa kufanyika huko Sharm El-Sheikh, Misri mwezi wa Novemba mwaka huu. 

"Bahari kimsingi ni muhimu kwa hali ya hewa. Inahifadhi asilimia 94 ya nafasi ya kuishi kwenye sayari. Niliweza kuachana na takwimu ambazo zilitushtua sote.”, asema kijana Scot mwenye umri wa miaka 27. 

"Sababu inayofanya bidhaa tunazonunua dukani kuwa nafuu ni kwa sababu meli husafirisha asilimia 90 ya bidhaa majumbani mwetu, kwa hiyo kuna sababu nyingi zinazotufanya tuunganishwe na bahari, iwe nchi isiyo na bandari au la. Hakuna kiumbe hai duniani ambacho hakiathiriwi na Bahari."ameongeza 

Samaki wakiogelea katika eneo linaololindwa nje ya pwani ya Malta bahari ya Mediterenea.
© FAO/Kurt Arrigo
Samaki wakiogelea katika eneo linaololindwa nje ya pwani ya Malta bahari ya Mediterenea.

5.Unaweza kufanya nini ili kusaidia? 

Tumeuliza baadhi ya wataalam ikiwa ni pamoja na Catarina Grilo na mwanabiolojia Nuno Barros kutoka ANP, pamoja na Sam Collins kutoka wakfu Oceano Azul, nini wananchi wanaweza kufanya ili kukuza uchumi endelevu wa bluu, huku tukisubiri watoa maamuzi na viongozi wa dunia kuchukua hatua.  

Hapa kuna maoni kadhaa ambayo unaweza kujumuisha katika maisha yako ya kila siku: 

1. Ikiwa unakula samaki, badilisha  au panua wigo wa lishe yako katika suala la matumizi, usile kila wakati aina moja. Pia epuka kula wanyama wanaokula Wanyama wenzao na hakikisha unachokula kinatoka kwenye vyanzo vinavyowajibika. 

2. Zuia uchafuzi wa taka za plastiki, wakati asilimia 80 ya uchafuzi wa baharini ukiwa umetokana na nchi kavu, fanya sehemu yako  kwa kukomesha uchafuzi unaofika baharini. Unaweza kusaidia kwa kutumia bidhaa zinazoweza kutumika tena, epuka kutumia bidhaa zinazoweza kutupwa, na pia kuhakikisha kuwa unaweka taka zako kwenye mapipa yanayofaa. 

Usafi kwenye ufukwe wa Praia da Poça, pwani ya Estoril - Cascais nchini Portugal.
UN News/Teresa Salema
Usafi kwenye ufukwe wa Praia da Poça, pwani ya Estoril - Cascais nchini Portugal.

3. Okota takataka kutoka pwani, na usitupe takataka. Lakini pia fikiria hatua yoyote unayoweza kuchukua ili kupunguza alama kwenye mazingira yako ambayo itasaidia bahari kwa njia isiyo ya moja kwa moja. 

4. Kuendelea kutetea suluhu, iwe ni barabarani, kuandika barua kwa watoa maamuzi, kusaini maombi, au kuunga mkono kampeni zinazolenga kushawishi watoa maamuzi, katika ngazi ya kitaifa au katika ngazi ya kimataifa. 

Waandishi wa Habari za UN watakuwepo Lisbon ili kuangazia mkutano huo wa Bahari, kwa hivyo tarajia kupata habari, mahojiano na maoni ya wataalamu, vijana na sauti za Umoja wa Mataifa.