Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu ya watu wazima, 'ngumbaru' haiwafikii wenye uhitaji zaidi - UNESCO 

Madarasa yako wazi lakini elimu inaendelezwa kwa kutumia teknolojia wakati huu wa kukabiliana na COVID-19
CC0 Public Domain
Madarasa yako wazi lakini elimu inaendelezwa kwa kutumia teknolojia wakati huu wa kukabiliana na COVID-19

Elimu ya watu wazima, 'ngumbaru' haiwafikii wenye uhitaji zaidi - UNESCO 

Utamaduni na Elimu

Changamoto kuu ya kujifunza na elimu ya watu wazima kote ulimwenguni ni kufikia wenye uhitaji zaidi. Huo ndio ujumbe muhimu wa Ripoti ya Tano ya kimataifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO kuhusu Mafunzo na Elimu ya Watu Wazima (GRALE 5) ambayo imewekwa wazi leo tarehe 15 Juni 2022 katika Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Elimu ya Watu Wazima huko Marrakech, Morocco. 

Ripoti ya UNESCO inaonesha kuwa pamoja na kwamba kuna maendeleo, hasa katika ushiriki wa wanawake, wale wanaohitaji elimu ya watu wazima zaidi, makundi ya watu wasio na uwezo na walio katika mazingira magumu kama vile wanafunzi wa wa jamii za asili, wakazi wa vijijini, wahamiaji, wazee, watu wenye ulemavu au wafungwa – wananyimwa upatikanaji wa fursa za kujifunza. 

Takriban asilimia 60 ya nchi ziliripoti kutoboresha ushiriki wa watu wenye ulemavu, wahamiaji au wafungwa. Asilimia 24 ya nchi ziliripoti kuwa ushiriki wa watu wa vijijini ulipungua. Na ushiriki wa watu wazima pia ulipungua katika asilimia 24 ya nchi 159 zilizochunguzwa. GRALE 5 inataka “mabadiliko makubwa katika mbinu ya Nchi Wanachama ya kujifunza na elimu ya watu wazima inayoungwa mkono na uwekezaji wa kutosha ili kuhakikisha kwamba kila mtu ana fursa ya kufaidika kutokana na kujifunza na elimu ya watu wazima.” 

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay amesema, “ninaziomba serikali na jumuiya ya kimataifa kuungana na juhudi zetu na kuchukua hatua ili kuhakikisha kuwa haki ya elimu inafikiwa kwa kila mtu – bila kujali umri wake, yeye ni nani, au anaishi wapi. Mabadiliko ya haraka ya kiteknolojia na kijamii pamoja na changamoto kubwa za kimataifa zinahitaji kwamba wananchi wawe na fursa ya kujifunza mambo mapya katika maisha yao yote. Ujuzi upya na uboreshaji kupitia ujifunzaji na elimu ya watu wazima lazima uwe utaratibu. Ustadi wa mwisho wa karne ya ishirini na moja ni uwezo wa kujifunza." 

Zaidi ya nusu ya nchi ziliripoti ongezeko la ushiriki katika kujifunza na elimu ya watu wazima tangu 2018 lakini changamoto bado zipo. Ingawa ushiriki wa wanawake na vijana umekuwa bora kwa kiasi kikubwa, ushiriki wa jumla katika kujifunza na elimu ya watu wazima unaendelea kuwa duni. Ripoti imeeleza.  

Ubora unakua 

Nchi nyingi ziliripoti maendeleo kuhusiana na ubora wa mitaala, tathmini na taaluma ya waelimishaji watu wazima. Zaidi ya theluthi mbili waliripoti maendeleo katika mafunzo ya kabla ya kazi na mafunzo ya kazini kwa waelimishaji wa Elimu ya watu wazima, ALE, na pia katika hali ya ajira, ingawa maendeleo haya yalitofautiana sana kulingana na eneo na kundi la kipato. Hii inakuza ubora wa elimu ya watu wazima.