Ukiukwaji wa haki za binadamu unaendelea Myanmar aonya Bachelet

14 Juni 2022

Hali ya haki za kibinadamu nchini Myanmar imeendelea kuzorota kwa kasi, amesema Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, Michelle Bachelet akizungumza mjini Geneva Uswisi hii leo kwenye mkutano wa 50 wa Baraza la Haki za binadamu.  

Wananchi bado wanateseka kutokana na matokeo mabaya ya mapinduzi ya kijeshi ya Februari mwaka 2021, sambamba na kunaswa katika mzunguko wa umaskini na kuyahama makazi yao na ukiukwaji wa haki za binadamu.    

“Takriban mauaji 1,900 ya jeshi yameripotiwa. Hali ya kibinadamu ni mbaya. Watu milioni moja wamesajiliwa na Umoja wa Mataifa kama wakimbizi wa ndani huku wengine milioni 14 wakisalia kuhitaji msaada wa dharura wa kibinadamu,” amesema Bi. Bachelet.   

Ameongeza kwamba kinachoshuhudiwa leo ni matumizi ya kimfumo na yaliyoenea ya mbinu dhidi ya raia, ambapo kuna sababu za kuridhisha za kuamini kutendeka kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita.    

Mapinduzi ya kijeshi yamedumaza uchumi wa Myanmar, huku mamilioni wakipoteza kazi au vyanzo vya mapato katika mwaka uliopita. Thamani ya sarafu ya taifa imeshuka, na bei ya bidhaa muhimu imepanda.    

Bachelet ameongeza, "kuzimwa kwa mtandao kunafanywa na wanajeshi katika sehemu kubwa za nchi, unyanyasaji na kufunguliwa mashtaka kwa waandishi wa habari na watu binafsi wanaoripoti juu ya haki za binadamu kuna mtiririko mdogo wa habari na nafasi ya raia."  

Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa inaendelea kufuatilia na kurekodi ukubwa wa ukiukaji mashinani.  

Ahadi za serikali ya kijeshi hazijatekelezwa 

"Licha ya ahadi zilizotolewa na jeshi kwa ASEAN, ghasia zisizo na maana nchini Myanmar zimeongezeka, na utoaji mdogo wa ulinzi wa raia au heshima ya haki za binadamu za kimataifa na sheria za kibinadamu na jeshi. Operesheni za hivi majuzi za kijeshi katika majimbo ya kusini-mashariki ya Kayin na Kayah, jimbo la kaskazini-magharibi la Chin, na maeneo ya kati ya Sagaing na Magway zimeongeza mateso ya raia," ameongeza Bi Bachelet.  

Kamishna huyo Mkuu amesema anaheshimu uthubutu wa watu wa Myanmar ambao licha ya kukabiliwa na ukandamizaji na uaktili wanaendelea kukaka jeshi na hatua zao za kuwadhibiti. Maandamano ya amani ya kila siku kote nchini na juhudi za kukataa huduma zinazotolewa na taasisi za serikali zinazosimamiwa na jeshi bado yanaendelea baada ya karibu siku 500.   

Hali jimbo la Rakhine  

Katika jimbo la Rakhine, hali ni mbaya, huku Jeshi la Arakan na Tatmadaw yakionekana kukaribia kuanzisha upya mzozo wa kivita. Tangu Novemba mwaka jana, kumekuwa na ghasia za mara kwa mara kati ya pande hizo mbili na majibizano ya matusi hadharani yamezidi kuwa ya chuki.  

Watu wa jamii ya Waislamu wa Rohingya wamenaswa katikati. Hakujawa na juhudi madhubuti na za utaratibu za kufanya kazi na Warohingya kutatua ukiukwaji wa muda mrefu wa haki za binadamu, ubaguzi na mazoea ya kutengwa ambayo yamekuwa yakisumbua jamii zao kwa miongo kadhaa.  

Kwa kuongezea, hali katika Jimbo la Rakhine bado haitoshi kwa Warohingya ambao walikimbilia Bangladesh, au kwa wale ambao wamekuwa wakiishi katika kambi za wakimbizi wa ndani nchini Myanmar kwa miaka 10 sasa, kurejea makwao.  

"Leo naomba hatua madhubuti zichukuliwe na pande zote kukomesha ghasia. Ulengaji wa raia na uchomaji wa vijiji lazima ukome sasa. Ulinzi wa raia ni jambo la lazima kabisa, na ufikiaji lazima utolewe kwa ajili ya  usaidizi muhimu wa kibinadamu kufikia jamii zote," Bi. Bachelet alisema.  

Ameongeza “ninayaomba mataifa yote wanachama, hasa yale yenye ushawishi mkubwa, kuzidisha shinikizo lao kwa uongozi wa kijeshi. Hatua zinazopatikana ni pamoja na kuweka vizuizi vinavyolenga umiliki wa fedha unaodhibitiwa na jeshi na maslahi ya biashara, na kuzuia ufikiaji wao wa sarafu za kigeni ili kuzuia uwezo wao wa kununua vifaa vya kijeshi."  

"Pia natoa wito wa kuendelea kuungwa mkono kwa juhudi zinazoendelea za kutafuta uwajibikaji kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaoendelea na uliopita, pamoja na madai ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, kupitia njia zote zilizopo," amesema Kamishna Mkuu.  

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter