Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yalazimika kusitisha msaada wa chakula Sudan Kusini

Mtoto mwenye umri wa miezi 6 nchini Sudan Kusini ambaye ana utapiamlo akilishwa chakula kwa kutumia bomba.
© UNICEF/Bullen Chol
Mtoto mwenye umri wa miezi 6 nchini Sudan Kusini ambaye ana utapiamlo akilishwa chakula kwa kutumia bomba.

WFP yalazimika kusitisha msaada wa chakula Sudan Kusini

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP limesema limelazimika kusitisha mgao wa chakula Sudan Kusini kutokana na ukata, hali ambayo itaacha theluthi moja ya wakazi wa taifa hilo changa zaidi duniani bila uhakika wa chakula na wengine milioni 1.7 hatarini kufa kwa njaa.

Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini Sudan Kusini Adeyinka Badejo amesema hayo leo akizungumza kwa njia ya video na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kutoka Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini.

“Usitishaji wa misaada unakuja wakati mbaya ziadi kwa watu wa Sudan Kusini kwani nchi hii inakabiliwa na njaa isiyo ya kawaida, tena kuwahi kutokea tangu taifa hili lipate uhuru. Zaidi ya asilimia 60 ya wananchi wanahaha kupata chakula wakati huu wa msimu wa mwambo, ikichochewa na mizozo, mafuriko, ukame na kuongezeka kwa bei ya chakula kunakochochewa na vita ya Ukraine,” amesema Bi. Badejo.

Madhara ya kusitisha mgao wa chakula kwa watoto

Amesema wana wasiwasi mkubwa jinsi uhaba wa fedha unaweza kuwa na madhara kwa watoto, wanawake na wanaume ambao hawakuwa na chakula wakati wa kipindi cha mwambo.

“Wanahitaji msaada wa haraka wa chakula ili wawe na mlo kwa kipindi hiki na kuweza kujenga mbinu za kujipatia kipato na mnepo kwa siku za usoni,” ameongeza Kaimu Mkuu huyo wa WFP Sudan Kusini. 

Amesisitiza kuwa mahitaji ya kibinadamu yanazidi kiwango cha fedha kilichopo ambacho walipokea mwaka huu. “Iwapo hali hii itaendelea, tutagharimika zaidi siku za usoni, ikiwemo vifo kuongezeka, utapiamlo, udumavu na magonjwa.”

Tumetumia mbinu zote kunusuru lakini wapi

WFP inasema imesaka mbinu zote kabla ya kuamua kusitisha mgao wa chakula, hatua ambazo ni pamoja na kupunguza kwa asilimia 50 mgao wa chakula mwaka 2021, hali iliyoacha baadhi ya familia zenye uhitaji wa chakula, bila chakula.

Hatua ya sasa itaathiri pia watoto wa shule 178,000 ambao hawatapa tena mlo shuleni kila siku, mlo ambao ulikuwa kivutio cha watoto kusalia shuleni kusoma, kujifunza na kukua.

Hatua zaidi za kupunguza mgao haziepukiki

WFP inasema hatua zaidi hazitaepukika, labda fedha zipatikane. Na kama hatua zaidi zitachukuliwa basi wananchi wa Sudan Kusini walio hatarini zaidi hawatakuwa na mbadala wa cha kufanya zaidi ya kutumbukia kwenye uamuzi hatari zaidi ili wapate mlo.

Hatua hizo ni pamoja na kuuza mali, kuchagua mlo mmoja tu kwa siku, kutumikisha watoto na hata kuoza watoto wao.

WFP imepokea kiasi kidogo cha fedha mwaka huu kwa ajili ya operesheni zake za kujengea wananchi mnepo na ndio maana inasema inahitaji dola milioni 426 ili kufikisha msaada wa chakula kwa watu milioni 6 walio na uhitaji zaidi wa chakula hadi mwishoni mwa mwaka huu wa 2022.