Kuajirika kwa watu wenye ulemavu kwazidi kuwa finyu- ILO

Kuajirika kwa watu wenye ulemavu kwazidi kuwa finyu- ILO
Fursa za watu wenye ulemavu duniani kupata ajira zinazidi kuwa finyu wakati huu ambapo takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO zinakadiria uwepo wa watu bilioni 1 wenye ulemavu duniani saw ana asilimia 15 ya wakazi wote wa dunia.
ILO kupitia taarifa yake iliyotolewa leo Geneva, Uswisi inasema asilimia kubwa ya watu hao wenye ulemavu wako na umri wa kufanya kazi lakini wengi wao wanakabiliwa na changamoto zinazowakwamisha kupata ajira ikilinganishwa na watu wasio na ulemavu.
Mkataba wa kimataifa wa watu wenye ulemavu ulipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Desemba mwaka 2006 likieleza bayana “haki ya watu wenye ulemavu kufanya kazi kwa misingi sawa na watu wengine.”
Lakini hali si kama usemavyo mkataba huo. ILO inabainisha
Ushiriki wao kwenye ajira ni mdogo
ILO inasema idadi ya watu wenye ulemave kwenye nguvu kazi ni ndogo. Takwimu zinasema duniani kote ni watu 7 wenye ulemavu kati ya 10 hawako kwenye ajira wengi wao wakiwa ni wanawake, ikilinganishwa na watu 4 kati ya 10 wasio na ulemavu.
“Hii ina maana wanawake wako hatarini zaidi kutokana na jinsia yao na ulemavu wao,” imesema ILO katika takwimu kutoka nchi 60.

Elimu bado ni ndoto kwa watu wenye ulemavu
Ni mara mbili zaidi kwa mtu mwenye ulemavu kukosa elimu kuliko yule asiye na ulemavu. Hata wakipata elimu, nusu yao ndio husonga kwenda elimu ya juu.
Tangu umri mdogo wanakumbana na vikwazo vya kupata elimu, “nah ii ina madhara makubwa katika soko la ajira kwani fursa ya ajira inaendana na kiwango cha elimu,” imesema ILO.
Elimu pamoja na stadi za hali ya juu zinakwamisha zaidi watu wenye ulemavu, “hivyo ni muhimu kuhakikisha kundi hili linapata fursa sawa ya elimu na programu za kuondoa pengo la stadi za kuwawezesha kuajirika au kujiajiri.”
Kiwango cha kutoajirika kwa watu wenye ulemavu ni kikubwa
Kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira miongoni mwa watu wenye ulemavu ni kikubwa katika nchi 30 zilizowasilisha takwimu zao, sawa na asilimia 50 ya nchi 60 zilizohusika.
Mtu mwenye ulemavu akikosa ajira kwa muda mrefu huathiri fursa za usoni na wakati mwingine hutumbukia kwenye ajira hata zisizo rasmi ali mradi aweze kukimu maisha yake.
Theluthi moja ya watu wenye ulemavu ndio wameajiriwa
ILO inasema ni theluthi moja tu ya watu wenye ulemavu duniani ndio wameajiriwa.
Pengo la ajira kati ya watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu huongezeka kadri umri wao unavyoongezeka.
Utafiti uliofanyika Mongolia umebaini kuwa kigezo kikubwa cha kurahisisha mtu mwenye ulemavu kupata ajira ni pale tu mwajiri akiwa ameweka mazingira bora; msaada wa kuwawezesha kutambua ajira ziliko; na kuwa na sifa na stadi za kiwango cha juu na uzoefu.
“Hii ina maana watu wengi zaidi wenye ulemavu wanaweza kuajiriwa iwapo wanapatiwa msaada sahihi kwa wakati sahihi ikiwemo fursa za kutosha za mafunzo,” imesema ILO.
Je nchi yako imefanya nini kupatia watu wenye ulemavu kupata fursa za ajira? Bofya hapa.