Emma Theofelus wa Namibia na BKKBN ya Indonesia ndio washindi wa Tuzo ya UNFPA mwaka 2022 

13 Juni 2022

Tuzo ya kila mwaka ya shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi, UNFPA ambayo hutolewa kwa mtu binafsi na shirika au taasisi inayojikita katika kuboresha afya ya uzazi kwa wanawake, pamoja na afya ya akina mama na wajawazito, mwaka huu imeenda kwa Emma Theofelus ambaye ni Naibu Waziri wa Habari wa sasa nchini Namibia na mshindi wa kwanza mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kupata tuzo hiyo.

Ushindi wa mbunge huyo mwenye umri wa miaka 25 umetangazwa hii leo na shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi, UNFPA kupitia hafla iliyofanyika kwa njia ya mtandao.  

Tuzo hiyo inayofahamika kama UN Population Award, pia imeenda kwa Bodi ya Kitaifa ya Idadi ya Watu na Uzazi wa Mpango ya nchini Indonesia, BKKBN, ambayo yenyewe imeshinda tuzo hiyo kama taasisi.  

Bi. Theofelus amepokea tuzo ya mtu binafsi kwa kazi yake ya kutetea uwezeshaji wa wanawake na afya ya uzazi kwa vijana nchini Namibia. Alizaliwa mwaka wa 1996 na ni mmoja wa mawaziri wenye umri mdogo zaidi barani Afrika. 

Akiwa naibu waziri, aliongoza kampeni ya nchi hiyo ya mawasiliano ya umma kuhusu kuzuia ugonjwa wa COVID-19 nchini Namibia, na kama Mbunge, hoja yake bungeni iliwezesha bidhaa za usafi wa wanawake kutambuliwa kama bidhaa isiyolipishwa kodi. Kabla ya uteuzi wake, Bi. Theofelus alikuwa mwanachama wa taasisi ya AfriYAN, shirika la kikanda linaloongozwa na vijana, ambako aliongoza juhudi za awali za kupigana na mimba za vijana wadogo na kulinda afya ya vijana ya ngono na uzazi. 

Kwa upande wa taasisi iliyoshinda tuzo hiyo, Bodi ya Kitaifa ya Idadi ya Watu na Uzazi wa Mpango nchini Jamhuri ya Indonesia, ni taasisi isiyo ya kiserikali inayounda sera za kitaifa, inayotekeleza mipango ya uzazi wa mpango na wataalam washauri katika uwanja wa mienendo ya idadi ya watu. 

Miongoni mwa mafanikio yake mengi, taasisi hiyo imetoa mafunzo kwa wataalam wa idadi ya watu, kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali na ya kidini kuhusu masuala ya idadi ya watu, na kuandaa programu za kusaidia familia zinazowajali wazee na iliendelea kuhudu hata katikati ya janga la Covid-19. "Pia ilichukua nafasi kubwa katika kuelimisha dhidi ya  mila potofu, na kusaidia kuongeza umri wa chini wa kuolewa kwa wasichana kutoka miaka 16 hadi 19 mnamo 2019." Taarifa iliyotolewa na UNFPA imeeleza.  

Tuzo hii ya Umoja wa Mataifa ya Idadi ya Watu imewatunuku watu binafsi na taasisi kwa mchango wao bora kwa idadi ya watu, maendeleo na afya ya uzazi tangu mwaka 1983. Kamati ya tuzo hiyo mwaka huu 2022 inaongozwa na Balozi Amal Mudallali, Mwakilishi wa Kudumu wa Lebanon katika Umoja wa Mataifa, na inaundwa na wawakilishi wa Mataifa mengine tisa Wanachama wa Umoja wa Mataifa. Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii, DESA, inamwakilisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kamati hiyo, na UNFPA inahudumu kama sekretarieti ya kamati. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter