Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasafirishwa kiharamu Niger ili kutumikishwa kwenye kuombaomba- IOM 

Usafirishwaji haramu wa binadamu.
IOM
Usafirishwaji haramu wa binadamu.

Wasafirishwa kiharamu Niger ili kutumikishwa kwenye kuombaomba- IOM 

Haki za binadamu

Asilimia 69 ya watu waathirika na manusura wa usafirishaji haramu binadamu nchini Niger ni wanawake na wasichana, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM. 

Kupitia taarifa yake iliyotolewa hii leo mji mkuu wa Niger, Niamey, IOM inasema takwimu hizo ni kwa mujibu wa utafiti mpya wa aina yake uiofanyika nchini humo na umeangazia mbinu na mwenendo mpya wa usafirishaji haramu binadamu. 

Utafiti huo umebainisha kuwa usafirishaji haramu binadamu ni suala la jinsia ukiathiri zaidi wanawake na wasichana; asilimia 31 walikuwa wanaume na wavulana. Lakini kwa ujumla asilimia 37 ni watoto. 

Umri ni kati ya miezi minne na miaka 66 lakini kwa umri wa wastani ni miaka 20. 

“Kati ya mwaka 2017 na 2021, waathirika 666 wa usafirishaji haramu walisaidiwa katika vituo vya mpito vya usaidizi wa wahamiaji huko Niger, pamoja na vingine vinavyoendeshwa na serikali huko Zinder na maeneo mengine nje ya vituo hivyo. Idadi kubwa walisajiliwa Zinder, Agadez, Arlit, Dirkou, na mkoa wa Niamey,” imesema taarifa hiyo. 

“Huu ni utafiti muhimu sana kwa sababu unaongeza taarifa katika historia yetu ya muda mrefu ya ushirikiano na serikali ya Niger katika kulinda na kusaidia manusura wa usafirishaji haramu hapa Niger,” amesema Barbara Rijks, Mkuu wa Ofisi ya IOM nchini humo. 

Amesema utafiti huo utachangia katika kuimarisha harakati za kudhibiti usafirishaji haramu wa binadamu na kutoa msaada unaohitajika wa kusaidia manusura wa ukatili huo. 

Halikadhalika utafiti unabainisha kuwa asilimia 56 ya waliosafirishwa kiharamu wanatoka Nigeria na asilimia 23 Niger na waliosalia wanatoka nchi mbalimbali za Afrika zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara. 

Na uchambuzi wa takwimu hizo unaonesha asilimia 38 wamesafirishwa kwa ajili ya kutumikishwa kwenye ngono, ikifuatiwa na utumikishwaji kazini, asilimia 21 ilihali asilimia 23 wanasafirishwa ili kutumbukizwa kwenye janga la kuombaomba. 

Tangu mwaka 2006, IOM imekuwa ikisaidia wahamiaji walio hatarini nchini Niger na kusaidia kupata haki zao.