Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sekta zote zihusishwe ili kuondoa tatizo la ajira za watoto Guatemala

Uchunaji wa kahawa San Marcos nchini Guatemala.
Unsplash/Gerson Cifuentes
Uchunaji wa kahawa San Marcos nchini Guatemala.

Sekta zote zihusishwe ili kuondoa tatizo la ajira za watoto Guatemala

Ukuaji wa Kiuchumi

Ikiwa leo wakuu wa nchi na wanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani wanakutana katika mkutano wa 110 wa Kimataifa wa wanachama wa shirika hilo kujadili hatua za haraka zinazoweza kuchukuliwa ili kukabiliana na athari za ajira na kijamii za migogoro mingi iliyoibuka duniani nchini Guatemala wadau wamehimiza sekta zote kujumuishwa ili kutatua tatizo la ajira kwa watoto.

Guatemala, nchi ya nane duniani kwa uzalishaji wa zao la kahawa ikisifika kuwa na kahawa nzuri lakini miongoni mwa wazalishaji wa kahawa hiyo ni watoto.

Watoto hawa wapo kwenye ajira rasmi kwa kuwa taifa hilo linatambua umri wa ajira ni kuanzia miaka 14.

Utafiti uliofanywa na ILO nchini Guatemala umeonesha zaidi ya asilimia 65 ya watoto wanashiriki katika ajira kwenye sekta ya kilimo hususan katika zao la kahawa. Miguel Ostumarai Mundo ni miongoni wa wakulima wadogo wa kahawa na anaeleza nini kifanyike ili kupunguza ajira za watoto, “Tatizo ni kuwa wazazi wengine wanaweza kuwatoa watoto wao mashuleni na kuwapeleka mashambani, hii si sawa. Jambo bora zaidi kufanyika ni kuwahudumia na kuhakikisha wanapata elimu bora na muda wao wa ziada wanaweza kuwafundisha kuhusu kilimo na kuwapeleka shambani chini ya usimamizi wa wazazi wao”

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO linashirikiana na wadau nchini Guatemala kutoa elimu kwa wakulima ya kilimo chenye tija pamoja na kuwaelimisha umuhimu wa kuhakikisha watoto wanapata elimu

Otonier Mora ni Mratibu wa mradi wa vijana wa FAO ambaye anasisitiza umihimu kujumuisha sekta zote ili kuondoa ajira za watoto na kuhamasisha ajira zenye staha, “Sekta zote, binafsi, za kiserikali na zisizo za kiserikali pamoja na Umoja wa Mataifa lazima ziunganishe nguvu katika kuhakikisha kuwa hatua zinazochukuliwa zinasaidia kupunguza ajira kwa Watoto. Hili litawezekana tuu iwapo vijana hawa watapata fursa ya kupata elimu bora, ajira, usaidizi wa kifedha na fursa za ujasiriamali”