Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje umerejea katika hali ya kabla ya COVID-19: UNCTAD 

Shehena kwenye bandari ya Mombasa, Kenya
© UNDP/Tamara Tschentscher
Shehena kwenye bandari ya Mombasa, Kenya

Uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje umerejea katika hali ya kabla ya COVID-19: UNCTAD 

Ukuaji wa Kiuchumi

Mpangilio wa uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje FDI umejikwamua na kurejea katika hali ya kabla ya janga la COVID-19  mwaka jana na kufikia kiwango cha dola trilioni 1.6 lakini matarajio kwa mwaka huu ni mabaya kwa mujibu wa ripoti mpya ya uwekezaji duniani iliyotolewa leo na kamati ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo ya uchumi na biashara UNCTAD. 

Ripoti hiyo iliyopewa jina "Mageuzi ya kimataifa ya kodi na uwekezaji endelevu" inasema ili kukabiliana na mazingira ya kutokuwa na uhakika na kuepusha hatari, nchi zinazoendelea lazima zipate usaidizi mkubwa kutoka kwa jumuiya ya kimataifa. 

"Haja ya uwekezaji katika uwezo wa uzalishaji, katika malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) na katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni kubwa mno. Mwenendo wa sasa wa uwekezaji katika maeneo haya si chanya kwa kauli moja," amesema Rebeca Grynspan, katibu mkuu wa UNCTAD

Dola za kimarekani
Picha ya UN
Dola za kimarekani

Uwekezaji wa muda mrefu 

Kwa katibu mkuu wa UNCTAD, haja ya kuwekeza katika uwezo wa uzalishaji mali, katika malengo ya maendeleo endelevu na katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni kubwa sana. 

Rebeca Grynspan anaongeza kuwa mwelekeo wa sasa wa uwekezaji katika maeneo haya haufuati mkondo wa kila mara.  

Anasisitiza kwamba wakati nchi zinakabiliwa na matatizo ya kutisha ya haraka yanayotokana na mgogoro wa gharama ya maisha, ni muhimu kwamba ufadhili wa changamoto za muda mrefu udumishwe. 

Kulingana na takwimu za ripoti hiyo, mtiririko wa uwekezaji wa kimataifa ulipanda kutoka kiwango cha chini mwaka 2020 na kuongezeka kwa 64% hadi dola trilioni $ 1.58 mwaka jana, ikichochewa na kuongezeka kwa shughuli za M&A na ukuaji wa ufadhili wa miradi ya kimataifa. 

Nchi zilizoendelea 

Ripoti hiyo ya UNCTAD inabainisha kuwa, ingawa ufufuaji huo umefaidi kanda zote karibu robo tatu ya ukuaji huo ulikuwa katika uchumi ulioendelea, kwani mtiririko wa uwekezaji wa kigeni uliongezeka kwa asilimia 134% na kampuni za kimataifa zilisajili faida. 

Mpangilio wa uchumi kwa nchi zinazoendelea ulipanda kwa asilimia 30% hadi kufikia dola bilioni $837, kiwango cha juu kabisa katika rekodi. 

Kulingana na utafiti huo, mwelekeo chanya ulionekana kwa kiasi kikubwa katika bara la Asia, na ahueni ya baadhi ya sehemu katika  ukanda wa Amerika ya Kusini Caribbea na Afrika. 

Sehemu ya nchi zinazoendelea katika mtiririko wa kimataifa ilisalia katika zaidi ya asilimia 50%. 

Zaidi ya hayo, sehemu ya mapato yaliyowekezwa tena ya uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni, yaani mapato yaliyohifadhiwa katika kampuni tanzu za kigeni na mashirika ya kimataifa, yalichangia sehemu kubwa ya ukuaji wa kimataifa, unaoakisi ongezeko la rekodi la mapato ya makampuni, hasa katika nchi zilizoendelea. 

Nchi 10 bora zilizo na mapato ya kigeni mwaka wa 2021 zilikuwa Marekani, Uchina, Hong Kong, Singapore, Canada, Brazili, India, Afrika Kusini, Urusi na Mexico. 

Mama na wanae wakulima Sao Paulo Brazil.
UN Women/Lianne Milton
Mama na wanae wakulima Sao Paulo Brazil.

 

Matarajio ya 2022 

UNCTAD inaeleza kuwa hali ya biashara na uwekezaji imebadilika sana mwaka huu. Vita nchini Ukraine inazidi kuongeza  mzozo mara tatu wa bei ya juu ya vyakula na mafuta na ufadhili mkubwa zaidi. 

Sababu zingine zinazopunguza mpango wa uwekezaji ni pamoja na athari kutoka kwenye janga la COVID-19, uwezekano wa kuongezeka kwa kiwango cha riba katika uchumi mkubwa, maoni hasi katika masoko ya kifedha na mdororo unaowezekana kutokea. 

Licha ya faida kubwa, uwekezaji wa makampuni ya kimataifa katika miradi mipya nje ya nchi mwaka jana ulikuwa chini kwa asilimia, tano ya viwango vya kabla ya janga la COVID-19. 

Ripoti hiyo inabainisha kuwa utabiri ni kwamba ukuaji wa mwaka 2021 hauwezi kudumishwa na kwamba mtiririko wa kimataifa mwaka 2022 unaweza kufuata mwelekeo wa chini, katika kusalia kwa utulivu. 

Malengo ya maendeleo endelevu 

Ripoti hiyo inabainisha kuwa, baada ya kupata athari kubwa katika mwaka wa kwanza wa janga hili, uwekezaji wa kimataifa katika malengo ya maendeleo SDGs uliruka  hadi asilimia 70% mwaka jana. 

Lakini ukuaji mwingi wa kujikwamua umekuja katika nishati mbadala na ufanisi wa nishati, ambapo maadili ya mradi yameongezeka mara tatu ikilinganishwa na kiwango cha kabla ya janga. 

Bado, ripoti hiyo inafichua kwamba ingawa ufufuaji wa 2021 ni mzuri katika suala la maadili, shughuli za uwekezaji katika sekta nyingi zinazohusiana na SDG katika nchi zinazoendelea, kama inavyopimwa kwa idadi ya miradi, zimekuwa nyuma ya viwango vya kabla ya mgogoro wa COVID-19. 

UNCTAD inakumbusha kuwa ufadhili wa miradi ya kimataifa unazidi kuwa muhimu katika kufikia SDGs na kuwekeza katika kudhibiti mabadiliko ya tabianchi. 

Mikataba ya kimataifa ya ufadhili wa miradi iliyotangazwa ilifikia rekodi ya miradi 1,262 mwaka jana na zaidi ya mara mbili ya thamani yake hadi kufikia dola bilioni $656. 

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa bidhaa maalum za uwekezaji uendelevu katika masoko ya fedha ya kimataifa zimeongezeka kwa asilimia 63% ikilinganishwa na 2020 na inapendekeza kwamba serikali kote ulimwenguni zitafute kuunda mifumo thabiti ya fedha endelevu.