Vita, mabadiliko ya tabianchi na uchumi vyachochea mgogoro wa chakula:FAO/WFP

7 Juni 2022

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la chakula na kilimo, FAO na mpango wa chakula duniani, WFP yametoa ripoti inayotaja maeneo 20 duniani ambako janga la njaa linaweza kuchochewa na mizozo, mabadiliko ya tabianchi, COVID-19, madeni ya umma na vita ya Ukraine.

Maeneo hayo ni pamoja na Kenya, Ethiopia, Nigeria, Sudan Kusini, Yemen na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. 

Mengine ni Afghanistan, Somalia, Haiti, Sudan, Syria, Sri Lanka, Benin, Cabo Verde, Guinea, Ukraine, Zimbabwe, Angola, Lebanon, Madagascar, na Msumbiji. 

Mamilioni kutumbukia katika umasikini

Kwa mujibu wa ripoti hiyo “Maeneo mapya yenye njaa tahadhari ya mapema ya FAO na WFP kuhusu hali mbayá ya kutokuwa na uhakika wa chakula” iliyotolewa leo mamilioni ya watu katika nchi nyingi duniani wanasukumwa kutumbukia katika umasikini na njaa wakati huu bei ya chakula na mafuta ikiendelea kupanda na kuyasogeza mataifa mengi katika hali ya kutokuwa na utulivu.

Hivyo ripoti imetowa wito wa hatua za haraka za kiboinadamu katika maeneo 20 yenye hatari ya njaa Kali inayotarajiwa kuwa mbayá zaidi kati ya mwezi Juni na Septemba 2022 ili kuokoa Maisha na uwezo wa watu kuishi  lakini pia kuzuia baa la njaa.

Pia ripoti imeonya kwamba vita ya Ukraine inachochea hal;i ambayo tayari ilikuwa mbayá kuwa mbayá zaidi kukishuhudiwa ongezeko la bei ya chakula na nishati kote duniani, na athari zinatarakjiwa kuwa mbayá zaidi katika maeneo ambako hali ya kiuchumi inayumba, ukichanganya na kushuka kwa uzalishaji wa chakula kutokana na mabadiliko ya tabianchi kama vile matukio ya kujirudia ya ukame na mafuriko.

Athari za pamoja za ukame, COVID-19 na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama kumedhoofisha zaidi hali ya uhakika wa chakula na lishe ya watu wa kusini mwa Madagascar.
WFP/Tsiory Andriantsoarana
Athari za pamoja za ukame, COVID-19 na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama kumedhoofisha zaidi hali ya uhakika wa chakula na lishe ya watu wa kusini mwa Madagascar.

Tunakimbizana na wakati kuwasaidia wahitaji

Mkurugenzi mkuu wa Fao Qu Dongyu amesema “Tunatiwa hofu kubwa kuhusu athari mchanganyoiko za majanga yanayoingiliana , na kutishia uwezo wa watu kuzalisha na kupata chakula, na hivyo kuwatumbukiza wengi katika kiwango cha juu ya kutokuwa na uhakika wa chakula. Tuko katika mbio dhidi ya muda ili kuwasaidia wakulima katika nchi zilizoathirika zaidi ikiwemo kuongeza haraka uwezekano wa uzalishaji wa chakula na kuinua mnepo katika kukabiliana na changamoto.”

Naye mkurugenzi mtendaji wa WFP David Beasely kwa upande wake  ameonya kwamba “Sasa hivi dunia inakabiliwa na dhoruba kubwa ambayo sio tu itaathiri na kuumiza watu nmasikini, lakini pia itaathiri mamilioni ya familia ambazo hadi sasa ziliweza kujimudu japo kiasi. Hali sasa ni mbayá zaidi kuliko ilivyokuwa wakati wa Arab Spring mwaka 2011 na 2007 hadi 2008 wakati wa mgogoro wa bei za chakula ambapo nchi 48 zikikabiliwa na changamoto za kisiasa, machafuko na maandamano makubwa. Tayari tunashuhudia nini kinachotokea Indonesia, Pakistan, Per una Sri Lanka, hicho ni kiocho tu. Tuna suluhu lakini tunahitaji kuchukua hatua na kuchukua hatua hizo haraka.”

Mamia ya maelfu ya watu wanaoishi nchini Burkina Faso hawana uhakika wa chakula
UNOCHA/Otto Bakano
Mamia ya maelfu ya watu wanaoishi nchini Burkina Faso hawana uhakika wa chakula

Ilichobaini ripoti

Ripoti hiyo imebaini kwamba mbali ya vita matukio ya mra kwa mara ya mabadiliko ya tabianchi ynaendelea kuchochea janga la njaa na kuonyesha kwamba tumeingia katika hali mpya ya kawaida ambapo ukame, mafuriko na vimbunga yanaripotiwa kuvuruga kabisa kilimo na ufugaji na hivyo kuwasukuma mamilioni ya watu katika hali ya kutawanywa  huku wengine wakiwa katika hatihati  katika nchi zote duniani.

Pia ripoti imesema hali mbayá ya uchumi katika nchi nyingi iliyochangiwa na janga la COVID-19 , kupanda kwa bei ya chakula na nishati kunasababisha watu wengi kupoteza kipato  miongoni mwa jamii za mataifa masikini  na hivyo kuathiri uwezo wa serikali kufadhimi mifuko ya hifadhi ya jamii, hatua za kusaidia kifedha jamii na uingizaji wa bidhaa muhimu.

Ripoti imetoa mapendekezo kuhusu vipaumbele vya haraka vya hatua za kibinadamu ili kuokoa Maisha na kuzuia baa la njaa, kulinda uwezo wa watu kuishi na kuhakikisha majanga yanayotabirika hayawi zahma kubwa.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter