Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mambo 5 ya kufahamu kuhusu kulinda raia dhidi ya silaha za mlipuko vitani

Mvulana akitembelea karibu na majumba yaliyosambaratishwa jirani na nyumbani yao huko Novoselivka, viunga vya mji wa Chernihiv nchini Ukraine
© UNICEF/Ashley Gilbertson
Mvulana akitembelea karibu na majumba yaliyosambaratishwa jirani na nyumbani yao huko Novoselivka, viunga vya mji wa Chernihiv nchini Ukraine

Mambo 5 ya kufahamu kuhusu kulinda raia dhidi ya silaha za mlipuko vitani

Amani na Usalama

Kwa wastani, asilimia 90 ya wanaouawa na kujeruhiwa kwa silaha za milipuko zinazotumiwa katika maeneo yenye wakazi wengi ni raia.  Ahadi ya kisiasa ya kukabiliana na madhara ya kibinadamu yanayoongezeka kutokana na matumizi ya silaha hizo katika miji mikubwa, miji midogo na vijijini inaweza kuwa hatua kubwa kuelekea kuwalinda wale walioko kwenye maeneo ya migogoro na vita. 

Madhara makubwa yanayosababishwa na silaha za milipuko zinazoanguka kwenye vituo vyenye idadi  kubwa ya watu yameshuhudiwa tena na tena, kuanzia Syria hadi Ethiopia, Myanmar na Iraqi.  

Utitiri wa picha zinazotoka Ukraine umewashtua wengi. Pamoja na vifo, matumizi ya silaha hizo ni sababu ya athari za muda mrefu, kusambaratisha maisha, na miundombinu muhimu kama vile vituo vya afya. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amekuwa akisisitiza mara kwa mara mataifa yapitishe ahadi ya kuepuka matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yenye watu wengi. 

Hii hapa ni tathimini ya athari ambazo silaha hizi zina nazo kwa idadi kubwa ya raia, na baadhi ya njia ambazo mataifa, Umoja wa Mataifa, na washirika wengine duniani kote wanajitahidi kuzitumia ili kupunguza athari za kibinadamu za silaha hizo. 

Uharibifu uliosababishwa na makombora huko Bucha nchini Ukraine.
© UNDP/Yevhenii Zavhorodnii
Uharibifu uliosababishwa na makombora huko Bucha nchini Ukraine.

1. Silaha za mlipuko ni nini? 

Silaha za mlipuko ni silaha za mifumo inayotumia risasi au vifaa ambavyo athari yake kubwa ya uharibifu hutokana na ulipukaji wa vilipuzi vingi na kusababisha mlipuko mkubwa katika eneo na mlipuko huo kutawanyika.  

Kuna aina nyingi tofauti za silaha za mlipuko zinazotumiwa na vikosi vya kijeshi vya kitaifa na vikundi vyenye silaha visivyo vya kiserikali. 

Mifano ni pamoja na silaha za moto zisizo za moja kwa moja, kama vile mizinga, maroketi, na makombora, silaha zinavyofyatuliwa kwa mfululizo, kama vile mifumo ya roketi zinazorushwa kwa wingi, mabomu makubwa ya angani na baharini, makombora ya balestiki ya uso kwa uso, na vifaa vya milipuko vilivyoboreshwa. 

Migogoro ya silaha inazidi kupiganwa katika vituo vya idadi kubwa ya makazi ya watu.  

Ongezeko hilo la vita katika miji limesababisha athari mbaya na jinamizi kwa raia, mara nyingi kutokana na utumiaji wa mifumo ya silaha ambayo imeundwa kwa ajili ya matumizi kwenye uwanja wa kawaida wa vita. 

Nyingi za silaha hizi zina athari zinazoonekana na zisizobagua zinapotumiwa katika maeneo yenye watu wengi na kusababisha ongezeko la vifo vya raia na madhara makubwa ya kibinadamu. 

Mtoto akitembea kwenye magofu huko Craiter mjini Aden nchini Yemen. Eneo hili liliharabiwa kwa kiasi kikubwa na makombora yaliyoangushwa kutoka angani mwaka 2015 wakati vikosi vya washirika vilipokuwa vikifurumusha wahouthi.
OCHA/Giles Clarke
Mtoto akitembea kwenye magofu huko Craiter mjini Aden nchini Yemen. Eneo hili liliharabiwa kwa kiasi kikubwa na makombora yaliyoangushwa kutoka angani mwaka 2015 wakati vikosi vya washirika vilipokuwa vikifurumusha wahouthi.

 

2. Ni nini athari za kibinadamu na matokeo ya matumizi ya silaha hizi katika maeneo yenye watu wengi? 

Silaha hizio zinapotumiwa katika vijiji, miji mikubwa na miji midogo, au maeneo mengine yenye watu wengi, silaha za mlipuko huwa na athari kubwa na madhara ya mara moja na ya muda mrefu kwa raia, kusambaratisha maisha, riziki na miundombinu muhimu. 

Mbali na athari za haraka, raia wengi wanaathiriwa na athari zisizo za moja kwa moja na mara nyingi ni za muda mrefu kutokana na silaha hizo, pia hujulikana kama athari za kujirudia.  

Watoto huathirika zaidi na aina mbalimbali za kiwewe cha kisaikolojia au kihisia. 
Vituo vya kutolea huduma za afya vinaathirika, hivyo kukwamisha utoaji wa huduma za matibabu.  

Nyumba na miundombinu muhimu, kama vile maji ya kunywa na mitambo ya kusafisha maji machafu na mifumo ya usambazaji wa umeme, huharibiwa au kusambaratishwa kabisa, na hivyo kuongeza hatari ya kuenea kwa magonjwa na kulemea zaidi mfumo wa huduma za afya. 

Shule zinalipuliwa, zinakatiza au kusimamisha upatikanaji wa elimu, hivyo kusababisha hatari kubwa kwa watoto na mara nyingi kufichua ukosefu wa usawa wa kijinsia.  

Utumiaji wa silaha hizi katika maeneo yenye watu wengi pia unaweza kuchangia watu wengi kuhama makazi yao, na kuwalazimisha watu kuondoka makwao, mara nyingi kwa muda mrefu na katika mazingira hatarishi. 

Pia utumiaji wa silaha hizi kila mara huacha mabaki ya vita ambayo yanaweza kuua na kuumiza raia, haswa watoto, muda mrefu baada ya uhasama kumalizika. 

Mabaki yanaweza pia kuzuia au kuchelewesha kazi ya ujenzi mpya au uzalishaji wa kilimo, pamoja na kurudi kwa wakimbizi na watu waliolazimika kufungasha virago na kuondoka. 
 

Mtoto akiendesha kigari chake wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya Idd el Fitr  huko Ghouta Mashariki nchini Syria.
© UNICEF/Amer Al-Mohibany
Mtoto akiendesha kigari chake wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya Idd el Fitr huko Ghouta Mashariki nchini Syria.

3. UN na washirika wanafanya nini kupunguza idadi ya vifo vya raia? 

Tangu mwaka 2009, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, na watangulizi wake, mara kwa mara wametoa wito kwa pande zinazozozana kuepuka matumizi yao ya silaha hizo katika maeneo ya raia, hasa kupitia ajenda yake ya upokonyaji silaha, ambayo inajizatiti kuunga mkono nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kuandaa tamko la kisiasa linalozungumzia matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yenye watu wengi, pamoja na vikwazo, viwango vya kawaida, na sera za uendeshaji, kulingana na sheria za kimataifa za kibinadamu. 

Mwaka  2019, pamoja na Rais wa kamati ya kimataifa ya chama cha msalaba mwekundu, Bwana. Guterres alitoa wito kwa pande zinazozozana kutumia mikakati na mbinu za kuondoa vita nje ya maeneo yenye watu wengi na "kujaribu kupunguza mapigano kabisa mijini". 

Kuweka kumbukumbu kikamilifu za athari za muda mfupi na za muda mrefu za kibinadamu za matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yenye watu wengi, ikiwa ni pamoja na kukusanya takwimu kuhusu vifo vya raia, ni muhimu katika kuchukua hatua zinazofaa. 

Umoja wa Mataifa, kamati ya kimataifa ya chama cha msalaba mwekundu na NGOs kote ulimwenguni wamechapisha tafiti nyingi kuhabarisha mijadala na kuboresha sera na mazoezi ya kijeshi. 

Baadhi ya vikosi vya kijeshi vimepitisha sera za kuepuka au kuzuia matumizi ya baadhi ya silaha za milipuko katika hali fulani ili kuwalinda vyema raia, kama vile kikosi cha kimataifa cha usaidizi wa usalama nchini Afghanistan na Mmpango wa Muungano wa Afrika nchini Somalia. 
 

Watoto wakipita karibu na majengo yaliyoharibiwa kwa makombora huko Benghazi nchini Libya
© UNOCHA/Giles Clarke
Watoto wakipita karibu na majengo yaliyoharibiwa kwa makombora huko Benghazi nchini Libya

4. Ni nini kingine kinachotokea katika ngazi ya kimataifa? 

Katika miongo kadhaa iliyopita, miungano ya serikali na mashirika ya kiraia imefaulu kufanya kampeni ya kukamilisha vyombo vipya vinavyoshughulikia madhara ya kibinadamu, kama vile mkataba wa kupiga marufuku ya matumizi ya mabomu ya kutegwa ardhini, Mkataba dhidi ya matumizi ya mabomu mtawanyiko na azimio la shule salama. 

Tangu mwaka wa 2010, wahusika wa misaada ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na mashirika ya kiraia, wameongoza juhudi za kuongeza ufahamu kuhusu athari zisizobagua na kali za kibinadamu za matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yenye wakazi. 

Mchakato wa mashauriano kwa ajili ya kuunda tamko la kisiasa la kimataifa linaloshughulikia madhara ya kibinadamu yanayotokana na matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yenye watu wengi yanayoongozwa na Ireland yamekuwa yakiendelea tangu 2019, kufuatia miaka ya juhudi za utetezi thabiti.  

Baada ya kusitishwa kwa sababu ya janga COVID-19, Mataifa yalikutana tena Aprili mwaka jana ili kujadili tamko la kisiasa, ambalo linatarajiwa kukamilika mwezi huu wa Juni. 

Katibu Mkuu ameeleza kuunga mkono kikamilifu mchakato huu, na anaendelea kutetea tamko la kisiasa linalojumuisha dhamira ya wazi ya kuepuka matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yenye watu wengi. 
 

Watoto wakisomea ndani ya darasa lao ambalo liliharibiwa kwa makombora huko mji wa Saada nchini Yemen. Kwa sasa wanajifunzia ndani ya mahema yaliyojengwa na UNICEF.
© UNOCHA/Giles Clarke
Watoto wakisomea ndani ya darasa lao ambalo liliharibiwa kwa makombora huko mji wa Saada nchini Yemen. Kwa sasa wanajifunzia ndani ya mahema yaliyojengwa na UNICEF.

5. Tamko la kisiasa linaweza kuleta tofauti gani? 

Kupitishwa kwa tamko la kisiasa kuhusu matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yenye watu wengi kunaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza madhara ya kibinadamu yanayohusiana na silaha hizo, kwa kutambua kwamba vita haiwezi kupiganwa katika maeneo yenye watu wengi kwa njia sawa na inavyopiganwa katika medani za wazi za vita. 

Mataifa yanapaswa kujitolea kuendeleza sera za uendeshaji kulingana na dhana dhidi ya matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yenye wakazi ili kuendeleza mabadiliko ya tabia, kukuza hatua madhubuti za kulinda raia na hatimaye kuimarisha utiifu wa sheria za kimataifa ya kibinadamu.