Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

 Mkutano wa dunia wa mawasiliano waanza nchini Rwanda 

 Uunganisho wa kidijitali, katika maeneo kama India, ni muhimu sana kuondokana na janga hili, na kwa urejeshaji endelevu na unaojumuisha.
United Nations/Chetan Soni
Uunganisho wa kidijitali, katika maeneo kama India, ni muhimu sana kuondokana na janga hili, na kwa urejeshaji endelevu na unaojumuisha.

 Mkutano wa dunia wa mawasiliano waanza nchini Rwanda 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa kimataifa wa maendeleo ya mawasiliano umeanza leo mjini Kigali nchini Rwanda ukiwa na lengo la kupitisha mwongozo wa kimataifa wa mabadiliko ya kidigitali ili hatimaye kusaidia kuweka ufikiaji wa maana wa teknolojia za kidijitali mikononi mwa mabilioni ya watu duniani kote na kuhakikisha wananchi wasiounganishwa na mtandao wanaunganisha ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu SDGs.

Mkutano huo wa siku kumi ulioanza leo (Juni 6 mpaka Juni 16, 2022) ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano Duniani, ITU unawaleta pamoja zaidi ya wadau elf moja na mia mbili ikiwemo wakuu wa nchi na serikali, mawaziri pamoja na wawakilishi wa vijana kutoka kila kona ya dunia.

Katika ujumbe wake kwa njia ya video wakati wa ufunguzi wa mkutano huo katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekumbusha dhima ya kuhakikisha hakuna mtu anaachwa nyuma katika kusaka maendeleo kwa wote.

“Zaidi ya theluthi moja ya wanadamu bado hawana uwezo wa kufikiwa na huduma ya intaneti. Jukumu lako katika mkutano huu wa mawasiliano ( #ITUWTDC) ni kuandaa mpango Kazi mpya ambao utawaleta karibu watu bilioni 3 ambao hawajaunganishwa katika jumuiya yetu ya kimataifa ya kidijitali kwa sababu tunavyosema tusimuache mtu nyuma,  tunamaanisha kutomwacha mtu yeyote nje ya mtandao wa intaneti.”

Guterres mbali na kuishukuru Rwanda kwa kuandaa mkutano huo pia amekumbusha umuhimu wa Mpango kazi wa Kigali utakao pitishwa katika mkutano kuweka ubinadamu mbele na kutatua changamoto ya mgawanyo wa kidigitali katika jamii maana unachochea kuongeza pengo la usawa.

“Pengo la kidigitali linachochea utofauti wa kijamii, kiuchumi na kijinsia katika maeneo yote kutoka mijini mpaka vijijini, kutoka kwenye elimu mpaka sekta ya afya, kutoka utotoni mpaka utu uzima na kwakuwa mkutano huu unawaleta watu pamoja ikiwemo wakuu wa nchi, makampuni binafsi, asasi za kiraia na wadau wengine ni sehemu nzuri ya kukubaliana masuala muhimu ikiwemo uwazi, uhuru na usalama katika mitandao ya kidijitali.” 

Mkutano huu ambao hufanyika mara moja kila baada ya miaka minne unatoa wito wa kutumia uwezo ambao haujatumiwa wa teknolojia ya kidijitali ili kuharakisha kufikiwa kwa Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa na Ajenda ya ITU ya kuunganisha wote ifikapo mwaka 2030.

Pia unatoa fursa ya kipikee kwa jumuiya ya kimataifa kuunda mikakati ya kijasiri na ya kibunifu inayolengwa kidijitali ili kusaidia kuvunja vizuizi sugu vya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Janga la COVID-19 limeonesha kwa kina umuhimu wa jamii nzima kuunganishwa na mtandano ili kuimarisha uthabiti wa kiuchumi na kuhakikisha ushirikishwaji wa kijamii kila mahali.