Kamishna wa haki za binadamu apongeza CAR kupitisha ukomeshaji hukumu ya kifo

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Michelle Bachelet akitoa maoni kuhusu kupitishwa kwa sheria ya kukomesha hukumu ya kifo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR amepongeza hatua hiyo na akasema anamuhimiza Rais Faustin-Archange Touadéra aitangaze.
“Adhabu ya kifo haiendani na kanuni za msingi za haki za binadamu na utu.” Amesisitiza Bi Bachelet mjini Geneva Uswisi hii leo.
Mara tu sheria hiyo itakapoanza kutumika, CAR itakuwa Taifa la 24 la Afrika kukomesha hukumu ya kifo, na hivyo kuimarisha mwelekeo wa kimataifa kuelekea kukomesha kwa ulimwengu hivyo kuchangia katika kuimarishwa na maendeleo ya haki za binadamu. Mataifa 170 hadi sasa yamefuta au kuanzisha usitishaji wa hukumu ya kifo kisheria au kiutendaji.
CAR yenyewe ilikuwa haitekelezi hukumu hiyo ya kifo tangu mwaka 1981.
“Ofisi yangu itaendelea kuunga mkono CAR katika juhudi zake za kukomesha kabisa.” Amesema Kamishna huyo wa Haki za Binadamu akiongeza kuwa ikiwa ni pamoja na kuunga mkono uidhinishaji na utekelezaji wa Itifaki ya Pili ya Hiari ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa kuhusu kukomesha hukumu ya kifo.