Skip to main content

Ongezeko la mashambulizi dhidi ya wahudumu wa kibinadamu linatishia misaada kwa watu walio hatarini CAR - OCHA 

Ukatishaji wa huduma za kibinadamu unaathiri upatikanji wa maji Basse-Kotto Prefecture, CAR.
© UNOCHA/Virginie Bero
Ukatishaji wa huduma za kibinadamu unaathiri upatikanji wa maji Basse-Kotto Prefecture, CAR.

Ongezeko la mashambulizi dhidi ya wahudumu wa kibinadamu linatishia misaada kwa watu walio hatarini CAR - OCHA 

Msaada wa Kibinadamu

Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Bi. Denise Brown, kupitia taarifa iliyotolewa leo na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, OCHA, amelaani vikali ongezeko la mashambulizi dhidi ya mashirika ya kibinadamu, ambayo katika baadhi ya matukio yamelazimisha mashirika kusimamisha shughuli zao kwa ajili ya usalama wa wafanyakazi wao. 

Taarifa hiyo iliyotolewa katika mji mkuu wa CAR, Bangue, imeeleza kuwa mashambulizi manne dhidi ya wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu yalitokea katika muda wa wiki moja tu. 

Mashirika mawili ya misaada ya kibinadamu yalisitisha shughuli zao baada ya mashambulizi ya silaha dhidi ya wafanyakazi wao. Katika Zaidi, watu wenye silaha walivamia timu ya kibinadamu inayosambaza chakula na vifaa vingine na kuiba vitu vya msaada, na kuacha familia 230 zilizofurushwa zikisubiri msaada katika hali mbaya. 

"Wananchi ndio wameathirika zaidi na ongezeko hili la kutisha la ghasia. Na kila mara shirika la kibinadamu linaposhambuliwa, upatikanaji wa maji, chakula, huduma za afya na elimu unatishiwa katika hali ambayo zaidi ya nusu ya watu wanahitaji msaada wa kibinadamu. Natoa wito kwa pande zote kuheshimu wajibu wao chini ya Sheria ya Kimataifa ya Kibinadamu na kuruhusu mashirika ya kibinadamu kupita bure." amesema Bi. Brown. 

OCHA inaeleza kuwa usaidizi kwa zaidi ya watu 46,000 walio katika mazingira magumu, wengi wao wakiwa wakimbizi wa ndani, utakatizwa kaskazini-magharibi mwa nchi katika maeneo ya huduma za afya, unyanyasaji wa kijinsia, ulinzi na usimamizi wa kambi, kufuatia kusimamishwa kwa usaidizi wa mashirika hayo mawili kushambuliwa na watu wenye silaha. 

Denise Brown anaeleza kuwa, "watu milioni 2.2 nchini CAR hawana chakula cha kutosha na hawajui mlo wao ujao unatoka wapi. Itakuwa janga ikiwa shirika la kibinadamu linalofanya kazi katika usalama wa chakula litalazimika kusimamisha shughuli zake kutokana na mashambulizi ya watu wenye silaha."  

Kati ya Januari na Mei 2022, matukio 69 ya usalama yaliathiri wasaidizi wa kibinadamu, ikiwa ni pamoja na mtu mmoja aliyeuawa na 16 kujeruhiwa, inaeleza OCHA.