Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 na vita ya Ukraine  vyakwamisha lengo la upatikanaji wa nishati kwa wote:UN

Mama na mwanae wakiwa kando mwa jiko lisilohifadhi mazingira ambalo ni shida kwa afya yao.
Benki ya Dunia/Prabir Mallik
Mama na mwanae wakiwa kando mwa jiko lisilohifadhi mazingira ambalo ni shida kwa afya yao.

COVID-19 na vita ya Ukraine  vyakwamisha lengo la upatikanaji wa nishati kwa wote:UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ripoti mpya kuhusu maendeleo ya nishati iliyotolewa leo na Umoja wa Mataifa imesema janga la COVID-19 limezorotesha mchakato wa kuelekea upatikanaji wa nishati kwa wote, huku vita inayoendelea nchini Ukraine huenda ikaudumaza zaidi mchakato huo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya mwaka 2022 “Kufuatilia SDG 7: Ripoti ya maendeleo ya nishati” duniani kote watu milioni 733 bado hawana nishati ya umeme na wengine bilioni 2.4 bado wanapikia nishati ambazo ni hatari kwa afya zao na mazingira.

Ripoti hiyo iliyotolewa kwa pamoja na idara ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii DESA, Benki ya Dunia na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, imeendelea kusema kwa mwenendo wa sasa wa kusuasua watu milioni 670 watabaki bila nishati ya umeme ifikapo mwaka 2030 ikiwa ni watu milioni 10 zaidi ya ilivyotabiriwa.

Akiongezea kuhusu athari ya hilo Dkt. Maria Neira mkurugenzi wa idara ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na afya wa WHO amesema “Mamilioni ya watu wanakufa kwa magonjwa ya moyo, kiharusi, saratani na kichomi kwasababu bado wanategemea nishati chafu za kupikia na teknolojia ambazo ni vyanzo vikuu vya uchafuzi wa hewa. Wanawake na watoto wako hatarini zaidi kwani hutumia muda mwingi ndani na nje ya nyumba zao na kwa hivyo hubeba mzigo mzito zaidi wa afya na ustawi wao. Kwa hivyo kuhamia nishati safi na endelevu haitachangia tu kuwafanya watu kuwa na afya bora, pia italinda sayari yetu na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ripoti imeonyesha kuwa athari za COVID-19 ikiwemo masharti ya kusalia majumbani, kuvurugika kwa mnyororo wa kimataifa wa usambazaji na rasilimali kuelekwezwa katika kufanya bei ya mafuta na chakula kuwa ambayo watu wanaweza kumudu kumeathiri kwa kiasi kikubwa mchakato wa lengo la maendeleo enedelevu namba 7 la kuhakikisha nishati ya gharama nafuu, yakuaminika, endelevu na ya kisasa ifikapo 2030.

Pia imeonya ripoti kwamba karibu watu milioni 90 Afrika na Asia ambao waliweza kupata fursa ya nishati ya umeme sasa hawawezi tena kulipa mahitaji yao ya msingi ya nishati hiyo

Kwa mujibu wa ripoti kana kwamba athari za COVID-19 hazitoshi vita ya Ukraine katika miezi michache iliyopita ambayo imesababisha hali ya sintofahamu duniani katika soko la mafuta na gesi imechangia ongezeko kubwa la gharama za nishati.

Afŕika imetajwa na ripoti hiyo kusalia kuwa bara yenye idadi ndogo zaidi ya umeme duniani ikiwa na watu milioni 568 wanaoishi bila umeme.

Na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara idadi ya watu duniani wanaoishi bila umeme iliongezeka hadi asilimia 77 mwaka 2020 kutoka asilimia 71 mwaka 2018 wakati ambapo kanda zingine zilishuhudia kupungua kwa pengo la wasio na nishati.

Wakati watu milioni 70 duniani kote walipata fursa ya nishati safi ya kupikia na teknolojia, hata hivyo maendeleo haya hayakutosha kuendana na ongezeko la idadi ya watu, hususan katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.