Zaidi ya watu milioni 30 walifungasha virago 2020 kutokana na majanga:UNDRR

31 Mei 2022

Zaidi ya watu milioni 30 walikimbia makazi yao kutokana na majanga mwaka 2020 pekee, na idadi hii huenda ikaongezeka kutokana na kuongezeka kwa hatari na idadi ya matukio makubwa yanayohusiana na hali ya hewa. Jopo katika Kikao cha 7 cha Jukwaa la Kimataifa la Kupunguza Hatari za majanga (GPDR2022), lililosimamiwa na Sarah Charles, Msimamizi Msaidizi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani, limeangazia mbinu za kuimarisha utawala ili kupunguza hatari za majanga ya kuhamishwa.

Baadhi ya wanajopo walijadili kuwa kujihusisha na jamii zilizoathiriwa ni muhimu, haswa katika kesi za mataifa ya visiwa vidogo na jamii ya watu wa asili.

Hindou Oumarou Ibrahim, Rais wa Chama cha Wanawake wa jamii ya asili na Watu wa Chad, alisema kuwa kuenea kwa jangwa kunaleta tishio lililopo kwa jamii asilia na vijijini. "Katika kipindi cha miaka 50 tu tutakuwa na jangwa katikati ya mji wangu, N'Djamena," alisema, ambayo inamaanisha kupoteza upatikanaji wa chakula, na malisho na maji kwa ajili ya ng'ombe.

"Tunapoteza nyumba yetu kwa uharibifu wa mfumo wa ikolojia, ni sehemu yetu, ni sehemu ya utambulisho wetu, utamaduni wetu."Amesema Bi Ibrahim.

Hindou Ibrahim, kutoka jamu ya Peule Mbororo nchini Chad.
UN News/Yasmina Guerda
Hindou Ibrahim, kutoka jamu ya Peule Mbororo nchini Chad.

Jamii za asili zina msaada mkubwa

Watu wa jamii za asili, amesema, wana uhusiano maalum na mfumo ikolojia wanamoishi, na wana ujuzi wa jadi ambao wamejifunza kutoka kwenye mazingira yao na kurithishwa kati ya vizazi.

"Tumejifunza hekima ya jinsi ya kutarajia na kuzuia baadhi ya hatari ambazo zinatujia na ambazo zinaweza kutulazimisha kuhama."

Watu wa asili wanaweza kutumia maarifa ya kitamaduni kupunguza kasi ya ongezeko la jangwa kwa "kujenga ukuta mkubwa wa kijani kibichi katika ukanda wa Sahel", amesema.

"Sisi ni wataalam wa upandaji miti, juu ya upandaji miti katika eneo la Savannah, kwa ajili ya kurejesha mifumo ya ikolojia kupitia njia ya maisha ya mababu zetu, na tunajua jinsi ya kutambua mazao ambayo yanastahimili ukame."

Wahamiaji huzingatia sana mabadiliko ya mazingira, kwani wamejifunza kutambua na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na upatikanaji wa rasilimali, kwa kuhama na misimu.

"Lakini sisi ni wahamiaji kwa makusudi," amesisitiza, "Sio wa kulazimishwa kuhamishwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi."

Washauri wachache, mabibi na mababu zaidi

Jamii za kiasili zina zana, lakini zinahitaji kutafuta njia za kuzishiriki na watu wanaofaa ambao wanaweza kuzitumia kwa upunguzaji mkubwa wa majanga (DRR).

Bi Ibrahim ameeleza jinsi upungufu wa maji katika eneo la Ziwa Chad ulivyolazimisha jamii za wavuvi na wakulima wa eneo hilo kuhama huku zikipoteza maisha yao.

Bibi Ibrahim alitumia teknolojia ya ramani ya satelaiti na maarifa ya jadi ya mahali hapo ili kukuza uelewa wa rasilimali za kimaumbile na kitamaduni.

Hii imesaidia jamii kujadiliana kugawana rasilimali, na hivyo kuepuka migogoro. Kwa kuchora rasilimali za kitamaduni, pia huhifadhi maarifa asilia ili kupitishwa kwa vizazi vijavyo.

Ujuzi wa asili wa kimapokeo kuhusu rasilimali na hatari, unaoshikiliwa na nyanya na mababu katika jamii, unakuzwa kutoka vizazi hadi vizazi na umejaribiwa na kubadilishwa ili kuhakikisha maisha ya watu wao uyanaendelea. Aina hii ya maarifa inapaswa kuthaminiwa zaidi ya mikakati ya washauri wa nje, amesema.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter