Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya chakula ni tete Malawi. Vita ya Ukraine imechochea ukali wa bei - WFP

Nchini Malawi, kupanda kwa bei ya vyakula kunawasukuma maskini kwenye ukingo wa njaa.
© WFP/Francis Thawani
Nchini Malawi, kupanda kwa bei ya vyakula kunawasukuma maskini kwenye ukingo wa njaa.

Hali ya chakula ni tete Malawi. Vita ya Ukraine imechochea ukali wa bei - WFP

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, limesema lina wasiwasi mkubwa kuhusu kupanda kwa bei ya vyakula nmchini Malawi, hali ambayo inawasukuma maskini kwenye ukingo wa njaa. 

Msemaji wa WFP, Toson Phiri amewaeleza waandishi wa habari hii leo mjini Geneva, Uswisi kwamba tathmini mpya ya WFP imegundua kuwa changamoto hizi sasa zinachochewa zaidi na athari za Mgogoro wa Ukraine. 

“Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita gharama ya kikapu cha chakula imeongezeka kwa asilimia 18 nchini Malawi, na kufikia ongezeko kubwa zaidi katika eneo la Kusini mwa Afrika. WFP inatarajia hali mbaya zaidi ikiwa bei ya kikapu cha chakula itaendelea kuwa juu.” Ameeleza Bwana Phiri akiongeza kuwa asilimia 50 ya wakazi wa Malawi tayari wanaishi katika umaskini (chini ya dola 2 kwa siku) kabla ya kupanda kwa bei hizi. 

WFP inaona kwamba ikiwa bei ya chakula duniani itaendelea kupanda, shirika hilo litaathiriwa kwa njia mbili: itagharimu zaidi kununua chakula kwa wenye njaa, na idadi ya watu wanaohitaji msaada wa chakula itaongezeka. 

Kutokana na ongezeko hili la bei, WFP ililazimika kurekebisha viwango vyake vya fedha. Hii ina maana kwamba rasilimali fedha zilizopo hazitadumu kwa muda mrefu. 

“Kwa wastani tunasaidia watu milioni 1.5 kila mwaka kwa msaada wa aina mbalimbali.” Amefafanua Phiri akitoa mifano ya ongezeko la bei katika bidhaa kadhaa muhimu kama:   

Mkate:  Bei za mkate na vyakula vingine vinavyotokana na ngano tayari zinapanda tangu Machi 2022. Mahojiano na wamiliki wa maduka ya kutengeneza mikate yanafichua kuwa bei ya rejareja ya gunia la kilo 50 za unga wa ngano imepanda kwa asilimia 42 tangu kuanza kwa vita. Bei ya mkate imeongezeka kwa asilimia 50 katika kipindi hiki. 

Mafuta: Malawi inaagiza kutoka nje asilimia 100 ya bidhaa zake za petroli zinazohitajika (petroli na dizeli). Kati ya Oktoba 2021 na Aprili 2022, bei ya petroli na dizeli imeongezeka kwa asilimia 54 na asilimia 64, mtawalia. Ongezeko la bei ya mafuta limechochea kupanda kwa bei za vyakula. 

Mbolea: Mnamo Januari 2021, kabla ya mzozo huo wa Ukraine, bei ya mbolea nchini Malawi ilikuwa juu kabisa, kati ya asilimia 130-160 juu kuliko mwaka wa 2020. 

Maharage: Kufikia wiki ya kwanza ya Mei 2022, bei ya maharagwe ilikuwa imeongezeka kwa asilimia 28 ikilinganishwa na wakati kama huo mwaka jana. 

Mafuta ya kupikia: Bei zimesalia juu licha ya kuondolewa kwa ushuru, VAT hadi tarehe 1 Aprili 2022 huku bei ikifikia Kwacha ya Malawi 8,000 - 9,000 (takribani dola 9 hadi 10) kwa chupa ya lita mbili, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 300 ikilinganishwa na Novemba 2020. 

“Kwa pamoja, vichochezi hivi vina uwezekano wa kuathiri wakulima wadogo na kuzidisha hali ambayo tayari ni tete ya uhaba wa chakula.” Inaeleza WFP. 

Watu wana wasiwasi juu ya kupanda kwa bei, huku wengi wakiangalia akiba zao na kujiuliza watapataje riziki. Bei ya wastani ya nafaka ya mahindi kwa kawaida inatarajiwa kushuka sana wakati wa mavuno. Lakini mapema Aprili 2022 bei ya mahindi ilipanda sana. Mambo mengi yanachangia kupanda kwa bei ya mahindi ambayo taifa linakabili kwa sasa, ambayo ni: 

Kupunguzwa kwa mgawo: WFP imelazimika kutoa asilimia 75 ya mgao wa kawaida kwa watu 400,000 wanaohitaji msaada wa chakula kutokana na majanga ya tabianchi (msimu wa 2021/22 na kukabiliana na mafuriko). Vile vile, wakimbizi 46,000 wamekuwa wakipokea mgawo wa asilimia 50 hadi 75 tangu Mei 2019. 

Pengo la ufadhili: USD 2.9 milioni kusaidia kaya 22,500 zilizoathiriwa na mafuriko (watu 101,000) kwa miezi mitatu na uhamisho wa fedha wa masharti. 

WFP inahitaji dola milioni 3.4 ili kuendelea kutoa msaada muhimu wa chakula (katika mfumo wa pesa taslimu bila masharti) kwa wakimbizi 48,000 na wanaotafuta hifadhi, kwa mgawo wa asilimia 100 kuanzia Agosti hadi Desemba 2022 (miezi 5).