Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yasikitishwa sana na ghasia zilizozuka upya katika eneo la Kivu Kaskazini, DR Congo

UNHCR inatoa msaada wa dharura kwa watu wanaokimbia mapigano ya silaha katika eneo la Rutshuru katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
© AIDES/Josaphat Tshilembi
UNHCR inatoa msaada wa dharura kwa watu wanaokimbia mapigano ya silaha katika eneo la Rutshuru katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

UNHCR yasikitishwa sana na ghasia zilizozuka upya katika eneo la Kivu Kaskazini, DR Congo

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema lina wasiwasi mkubwa kuhusu mahitaji ya dharura na makubwa ya zaidi ya watu 72,000 waliokimbia makazi yao kutokana na mapigano katika siku za hivi karibuni katika Jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. 

“Tangu tarehe 19 Mei, mapigano makali yametikisa maeneo ya Rutshuru na Nyiragongo huku wanamgambo wanaodai kuwa sehemu ya kundi lenye silaha la M-23 wakipambana na vikosi vya serikali katika mapambano yanayoendelea kaskazini mwa Goma, mji mkuu wa jimbo hilo.” Ameeleza hii leo Msemaji wa UNHCR Shabia Mantoo katika mkutano na waandishi wa habari kwenye ‘Palais des Nations’ yaani ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswisi. 

Takriban raia 170,000 wameyakimbia makazi yao, mara nyingi mara kwa mara tangu kuongezeka kwa mapigano mashariki mwa DRC kuanzia Novemba 2021. Wimbi la hivi karibuni la ghasia limesababisha makumi ya maelfu ya watu kutoka makwao kutafuta usalama katika maeneo tofauti ya jimbo hilo, ikiwa ni pamoja na Goma. Katika wiki iliyopita pekee, takriban 7,000 pia wameripotiwa kuvuka hadi nchi jirani ya Uganda nchi ambayo tayari inawahifadhi zaidi ya wakimbizi milioni 1.5. 

Bi Matoo ameendelea kueleza hali ilivyo akisema, “Wale wanaohama, njiani wanakabiliwa na vurugu za mara kwa mara. Mashamba na maduka yameachwa katika hatari kubwa ya kuporwa, hivyo kutishia maisha. Wanawake na wasichana wanakabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na ubakaji, pamoja na vitisho vya kimwili na unyang'anyi wa pande zinazozozana.”  

Aidha amesema watoto wengi wametenganishwa na familia zao. Mapigano hayo yanakuja wakati jamii zilizofurushwa hapo awali kutokana na ukosefu wa usalama katika eneo hilo zilikuwa zimeanza kurejea nyumbani na kuanzisha tena maisha yao. Mzunguko huu wa vurugu na uhamisho umekuwa chanzo cha mara kwa mara cha kukata tamaa na hatari. 

Maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na mapigano ya sasa wanakabiliwa na matatizo ya kupata makazi na vifaa vya nyumbani, pamoja na kupata chakula na maji safi. Wengine wanategemea ukarimu wa familia za raia wengine, na wengine wametafuta usalama katika shule, makanisa na maeneo yaliyojengwa awali na mamlaka kuwahifadhi wale waliolazimika kukimbia mlipuko wa volcano ya Nyiragongo uliotokea mwaka jana 2021 mwezi Mei. 

Maeneo mengi ya makazi ya muda kama haya yanakosa miundombinu ya kusaidia wahamiaji wapya, na kuwaweka kwenye hatari ya ugonjwa wa kipindupindu, malaria na magonjwa mengine. Utumiaji wa miundombinu ya elimu pia inawaacha watoto nje ya shule, ambapo wangeweza kujifunza katika mazingira yanayolindwa. 

Wakati hatua zilichukuliwa mwezi wa Aprili kutoa msaada unaohitajika sana kama blanketi, magodoro ya kulalia na sabuni kwa zaidi ya watu 2,900 walio katika mazingira hatarishi ambao tayari wamehamishwa katika maeneo ya Rutshuru na Kiwanja, maelfu zaidi sasa wanakimbia na mali zao chache au bila chochote. Mahitaji yanazidi sana usaidizi unaopatikana, na ufikiaji wa kibinadamu katika eneo hilo unatatizwa sana na ghasia. Takriban watu milioni 1.9 wamekimbia makazi yao huko Kivu Kaskazini. 

DRC ikiwa ni nyumbani kwa wakimbizi wa ndani, IDPs milioni 5.6, ni nyumbani kwa hali kubwa zaidi ya ukimbi wa ndani barani Afrika. 

UNHCR nchini Uganda, kwa ushirikiano na wadau wengine, inatoa msaada wa dharura kwa watu 25,000 waliovuka mpaka tangu tarehe 28 Machi na wanapata hifadhi katika vituo vilivyoanzishwa na UNHCR. 

UNHCR inahitaji kwa dharura dola za Marekani milioni 5 ili kuimarisha ulinzi wake na mwitikio wa kibinadamu huko Kivu Kaskazini. “Mahitaji yetu ya kifedha kote DRC yanasalia kuwa makubwa, na asilimia 16 tu ya dola milioni 225 zinazohitajika zimefadhiliwa.” 

Nchini Uganda, UNHCR na wadau hivi karibuni walitoa wito wa dola za Marekani milioni 47.8 ili kukabiliana na mahitaji muhimu ya maelfu ya wakimbizi ambao wamewasili nchini humo mwaka huu, ikiwa ni pamoja na karibu dola milioni 35 kwa ajili ya wapya waliowasili kutoka DRC.