Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wachanga 11 wateketea baada ya wodi ya wazazi kuungua Senegal:UNICEF 

Wakazi Mbar Toubaba nchini Senegal.
UNIC Dakar
Wakazi Mbar Toubaba nchini Senegal.

Watoto wachanga 11 wateketea baada ya wodi ya wazazi kuungua Senegal:UNICEF 

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limeeleza kusikitishwa na vifo vya takriban watoto 11 wachanga waliozaliwa hivi karibuni, kufuatia moto katika kitengo cha watoto wachanga cha hospitali ya Tivaouane nchini Senegal.  

Katika taarifa iliyotolewa na mwakilishi wa UNICEF Silvia Danailov, hii leo katika mji mkuu wa Senegal, Dakar, imesema, UNICEF inatoa pole nyingi kwa familia na jamii zilizoguswa na msiba huu hasa wale waliopoteza watoto wao.  

Imeongeza kuwa “Hakuna mzazi anayepaswa kupata huzuni wa kuona mtoto wake akipoteza maisha katika ajali kama hii.” 

UNICEF inasimama pamoja na mamlaka na wadau katika kutoa msaada, usaidizi unaohitajika kwa familia hizi na kuzuia majanga zaidi.   

Kwa mujibu wa duru za habari waziri wa afya wa Senegal Diouf Sarr ambaye kwa sasa yuko Geneva kuhudhuria Baraza la afya duniani lililoandaliwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO akizungumza na kituo cha radio cha RFM amesema “Tuliposikia kuhusu ajali hiyo tuliupigia simu uongozi wa hospitali ili kujua nini kilichotokea, na tukaambiwa kwamba kulikuwa na shoti ya umeme kwenye idara ya wodi hiyo na wauguzi waliokuwa zamu walijaribu kuingilia kati kuokoa maisha ya watu.” 

Wizara ya afya ya Senegal imesema waziri huyo wa afya ameamua kukatisha ziara yake Geneva na atarejea nyumbani Senegal mara moja.