Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwendazake Kapteni Abdelrazakh Hamit Bahar wa Chad ashinda tuzo ya pili ya UN ya kulinda amani kwa 'ujasiri wa kipekee' 

Kapteni Abdelrazakh(katikati) alitumwa kambi ya wakimbizi ya Aguelhok Kaskazini mwa Mali wakati ilishambuliwa na kundi la kigaidi.
Kwa hisani ya Luteni Kanali Chahata Ali Mahamat
Kapteni Abdelrazakh(katikati) alitumwa kambi ya wakimbizi ya Aguelhok Kaskazini mwa Mali wakati ilishambuliwa na kundi la kigaidi.

Mwendazake Kapteni Abdelrazakh Hamit Bahar wa Chad ashinda tuzo ya pili ya UN ya kulinda amani kwa 'ujasiri wa kipekee' 

Amani na Usalama

Marehemu Kapteni Abdelrazakh Hamit Bahar wa Chad, alitajwa Jumanne ya wiki hii kama mpokeaji wa tuzo ya juu zaidi ya Umoja wa Mataifa ya Kulinda Amani, kwa ujasiri wa kipekee, akihudumu nchini Mali, ambayo itatolewa Alhamisi hii katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa  New York, Marekani. 

Kapteni Abdelrazakh ambaye alijiunga na Kikosi cha  Umoja wa Mataifa cha Kulinda Utulivu nchini Mali (MINUSMA) mnamo Januari 2021 alitumwa katika Kambi ya Aguelhok Super  kaskazini mashariki wakati iliposhambuliwa na kundi la kigaidi lenye silaha lililojaribu kuteka kambi hiyo na viunga vyake. 

Aliongoza mashambulizi ya ujasiri ili kulinda kambi, kulinda maisha ya wenzake na kuzuia majeraha ya raia, lakini wakati akijaribu kulinda eneo hilo, Kapteni Abdelrazakh aliona washambuliaji wenye silaha walikuwa wakiingia kwenye nyumba karibu. 

Akiwa amedhamiria kuhakikisha kwamba hawadhuru wenzake na raia, aliongoza pekee yake, operesheni ya kulinda nyumba hiyo, ambapo alipigwa risasi na kuuawa. 

Tukio hilo lilitokea mwanzoni mwa Aprili mwaka jana 2021. 

Kapteni Abdelrazakh Hamit Bahar wa Chad.
Kwa hisani ya Hamid Bahr Ahmar
Kapteni Abdelrazakh Hamit Bahar wa Chad.

Mfano wa kujitolea 

"Nia ya Kapteni Abdelrazakh kuhatarisha maisha yake ili kuokoa wengine ni mfano wa ujasiri na kujitolea kwa zaidi ya walinzi wa amani milioni moja ambao wamehudumu kwenye mstari wa mbele wa vita tangu 1948," amesema Naibu Katibu Mkuu wa Operesheni za Amani, Jean-Pierre Lacroix.  

Ameongeza kuwa kujitolea kwa kapteni huyo pia kunaonesha hatari inayoongezeka inayowakabili walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanapofanya kazi yao muhimu katika baadhi ya mazingira yenye changamoto nyingi zaidi duniani. 

"Kapteni Abdelrazakh alijitolea kabisa katika kutafuta amani. Tunaomboleza msiba wake pamoja na familia yake, wafanyakazi wenzake na taifa la Chad. Huduma yake ya kujitolea inatumika kututia moyo sisi sote na tunajivunia kumheshimu.” Bw. Lacroix ameongeza. 

Kuhusu Tuzo 

"Nishani ya Kapteni Mbaye Diagne kwa Ujasiri wa Kipekee" itawasilishwa kwa familia ya Kapteni Abdelrazakh kwenye halfa itakayofanyika Alhamis hii jijini New York, Marekani. 

Medali hiyo ilipewa jina hilo kwa heshima ya Kapteni Mbaye Diagne ambaye aliokoa mamia ya maisha alipokuwa akihudumu kama mlinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa nchini Rwanda mwaka 1994, kabla ya kuuawa akiwa kazini. 

Mnamo mwaka wa 2014, tuzo hiyo ya juu ilianzishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama tuzo rasmi ya kuwatambua walinzi wa amani waliovalia sare na raia ambao wanaonyesha ujasiri wa kipekee. Mwaka huu ni mara ya pili tu kwa tuzo hiyo kutunukiwa. 

Pongezi zaidi 

Barua ya Pongezi kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia itakabidhiwa kwa walinda amani wengine watatu kwa kutambua ujasiri wao katika kutekeleza majukumu yao. 

Luteni Kanali Chahata Ali Mahamat wa Chad: 

Mnamo tarehe 2 Aprili 2021, wakati wa shambulio la magaidi wenye silaha kwenye Kambi Kuu ya Aguelhok nchini Mali, afisa mkuu anayehudumu na MINUSMA, alionesha ushujaa wa kweli kwa kuchukua jukumu la kuongoza katika shambulio la kukabiliana na washambuliaji. Alifaulu kusitisha shambulio hilo na akaongoza juhudi za kupata eneo la kutua ili kuwezesha kuwaondoa askari 16 waliojeruhiwa kwa dharura. 

Sajenti Cristofer Jose Citan Ramos wa Guatemala: 

Mnamo tarehe 30 Januari 2022, alikuwa kiongozi wakati wa doria iliposhambuliwa na kundi la waasi la CODECO katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Alihudumu katika tume ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani nchini humo, MONUSCO. Wakati wa shambulio hilo, alipigwa risasi na kujeruhiwa. Licha ya kuumia kwake, alionyesha ujasiri wa ajabu kwa kuendelea kujibu mashambulizi ili kuwazuia wapiganaji na kuwalinda wenzake. 

Kapteni Md Mahatab Uddin wa Bangladesh: 

Mnamo Novemba 2021, aliendelea na zaidi ya wito wa wajibu kwa kufanya mazungumzo kwa ujasiri na makundi yenye silaha nchini Sudan Kusini, kama Afisa Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, UNMISS, ili kuzuia mashambulizi dhidi ya raia na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa huko Tonj. Wakati wa mapigano ya mara kwa mara, pia alitoa ulinzi na hifadhi kwa raia 1,300, wakiwemo wanawake, watoto na wazee, katika kituo cha muda huku akishirikiana na jamii za eneo hilo kupunguza hali ya wasiwasi na kurejesha utulivu. 

Mlinda amani kutoka Chad aliyefarikia kupewa tuzo ya kuu zaidi ya UN ya ulinzi wa amani
Umoja wa Mataifa
Mlinda amani kutoka Chad aliyefarikia kupewa tuzo ya kuu zaidi ya UN ya ulinzi wa amani