Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bachelet afanya mikutano ya muhimu na Rais Xi wa China 

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet mkutanoni kwa njia ya mtandao na rais wa China Xi Jinping ziarani Guangzhou, China.
© OHCHR
Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet mkutanoni kwa njia ya mtandao na rais wa China Xi Jinping ziarani Guangzhou, China.

Bachelet afanya mikutano ya muhimu na Rais Xi wa China 

Haki za binadamu

Katika siku ya tatu ya ziara yake rasmi nchini China, kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amelezea kuwa ni fursa muhimu ya kuangazia masuala ya haki za binadamu na shuku na shaka katika mazungumzo yake na Rais Xi Jinping na maafisa wengine wakuu wa serikali , ikiwa ni ziara ya kwanza ya aina hiyo kufanywa na mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2005. 

Katika ujumbe wake wa Twitter siku ya leo Jumatano, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, Bi.Bachelet ameonyesha kuwa ameweza "kujadili moja kwa moja masuala muhimu kupitia njia ya video na waziri mkuu wa nchi hiyo, bila kutoa maelezo zaidi kuhusu hoja zake za walizozungumza.” 

Ujumbe wa kibinafsi 

"Nimejitolea kufanya ziara hii, ikiwa ni ziara ya kwanza ya kamishna mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini China katika kipindi cha miaka 17, kwa sababu kwangu, ni kipaumbele cha kwanza kuwasiliana na serikali ya China moja kwa moja katika masuala ya haki za binadamu, ndani ya nchi, kikanda na kimataifa,” amesema Bi. Bachelet katika maoni yaliyotolewa na ofisi yake, OHCHR

Almeongeza kuwa "Ili maendeleo, amani na usalama kuwa endelevu ndani na nje ya mipaka haki za binadamu lazima ziwe ni msingi." 

Katika hotuba yake kwa Rais Xi, mkuu huyo wa haki za binadamu pia amesisitiza kwamba China ina "jukumu muhimu la kuchukua ndani ya taasisi za kimataifa katika kukabiliana na changamoto nyingi zinazoikabili dunia kwa sasa", maoni aliyoyatoa katika hotuba yake kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Guangzhou. 

Changamoto hizi ni pamoja na "vitisho kwa amani na usalama wa kimataifa, kukosekana kwa utulivu katika mfumo wa uchumi wa dunia, ukosefu wa usawa, mabadiliko ya tabianchi na zaidi", Bi Bachelet ameelezea, akiongeza kuwa "Tunatazamia kuongeza mijadala yetu kuhusu masuala haya na mengine"

Kama ilivyo kwa nchi nyingine, kamishna mkuu pia ametoa msaada wa kiufundi wa China katikia kuambatana na juhudi za kuimarisha na kulinda haki za binadamu, haki na utawala wa sheria kwa wote bila ubaguzi 

Maendeleo Xinjiang  

Kipaumbele kinajiri wakati Bi Bachelet akijiandaa kuzuru leo mkoa huo unaojiendesha wa Xinjiang ulioko jimbo la Uyghur ambapo wataalam huru wa haki za binadamu walioteuliwa na Umoja wa Mataifa wameibua wasiwasi mkubwa kuhusu madai ya kuwekwa kizuizini na kulazimishwa kufanya kazi kwa Waislamu wa Uyghur. 

China imekanusha vikali madai hayo juu ya kutowatendea haki watu hao wachache wa Uyghur, ambapo mamia kwa maelfu wameripotiwa kushikiliwa katika vituo vinavyoitwa elimu ya upya au kuhamishwa kwa nguvu hadi kwenye viwanda vya Xinjiang au majimbo mengine ya China. 

Ufumbuzi wa wanafunzi 

Pia leo Jumatano katikati ya ziara yake ya siku sita nchini China mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa somo kwa wanafunzi katika chuo kikuu cha Guangzhou. 

“Wakati wa kutokuwa na uhakika na kutotabirika, elimu ya haki za binadamu ni muhimu sana kwa kila mtu,” amesisitiza Bi Bachelet.  

Ameongeza kuwa “amani inatoa fursa ya kuunda ukweli wetu wenyewe wa kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa ili kutoa suluhisho la kweli kwa changamoto ambazo watu wanakabiliana nazo". 

Licha ya vitisho vingi vya kimataifa, kuanzia kwa janga la COVID-19 hadi mabadiliko ya tabianchi, migogoro na ukosefu wa usawa unaokua, Kamishna Mkuu amewaambia wasikilizaji wake kwamba "nguvu kubwa ya ujana ilikuwa moja ya nguzo za matumaini". 

"Kiungo cha msingi kwa vijana kuweza kutekeleza jukumu hilo ni fursa ya wazi ya kiraia ambapo wanaweza kutoa maoni yao na kuleta mabadiliko," Bi. Bachelet amesema, akiongeza kuwa ametiwa moyo na vuguvugu la wanaharakati vijana ambao walipinga ubaguzi, dhuluma na ukosefu wa usawa. 

Aliongeza kuwa "Vijana wanashawishi mijadala umuhimu ya kitaifa na kimataifa na kuchagiza mabadiliko ya kijamii ikiwa ni pamoja na kudai kiti kwenye meza na kuwajibisha serikali na wafanyabiashara kwa kutochukua hatua." 

Akirejea wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kuchukua hatua kwa ajili ya Haki za Binadamu na mpango wa ajenda yetu ya pamoja kwa ajili ya hatua za kimataifa, ambao unasisitiza jinsi vijana wanavyopaswa kupata fursa ya kushiriki katika mijadala inayowahusu, Bi. Bachelet amesisitiza haja ya "Fursa iliyo wazi kwa raia ambapo wanaweza kutoa maoni yao na kuleta mabadiliko”. 

Akirejea kwenye mada ya haki isiyoweza kuondolewa ya kushiriki katika mazungumzo ya wazi, pia amesema “Wakati sekta mbalimbali za jamii zinapoletwa katika majadiliano, zikijumuishwa katika mjadala, inaruhusu uelewa wa kina wa masuala. Kuwa na sauti tofauti mezani, mataifa yanaweza kutambua vyema mapungufu katika sheria na sera, ili kuhakikisha kuwa yanatenda haki zaidi." 

Alipowasili Guangzhou leo ambako alilakiwa na naibu waziri wa mambo ya nje Ma Zhaoxu, Bi Bachelet amewaambia waandishi wa habari kwamba alitarajia kujadili "baadhi ya masuala muhimu sana na nyeti katika ziara yake, ili kusaidia kujenga ujasiri". 

Bachelet anatarajiwa kufanya mkutano na waandishi wa habari mwishoni mwa misheni yake ya siku sita.