Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlinda amani wa Zimbabwe ashinda tuzo ya UN ya  mtetezi bora mwanajeshi wa masuala ya jinsia 2021

Kufuatia ripoti za ukatili wa kijinsia nchini Sudan Kusini Meja Winnet Zharare (wa pili kutoka kulia) alienda kwa wanawake mashinani kujadili mbinu za kupambana na ukatili huo.
UNMISS
Kufuatia ripoti za ukatili wa kijinsia nchini Sudan Kusini Meja Winnet Zharare (wa pili kutoka kulia) alienda kwa wanawake mashinani kujadili mbinu za kupambana na ukatili huo.

Mlinda amani wa Zimbabwe ashinda tuzo ya UN ya  mtetezi bora mwanajeshi wa masuala ya jinsia 2021

Amani na Usalama

Mlinda amani raia Zimbabwe ambaye hivi karibuni alimaliza kazi yake katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini UNMISS, ameshinda tuzo ya Umoja wa Mataifa ya mwanajeshi mtetezi bora wa masuala ya jinsia kwa mwaka 2021.

Mshindi huyo ambaye ni wangalizi wa kijeshi Meja Winnet Zharare, mwenye umri wa miaka  39, alihudumu Bentiu, Sudan Kusini tangu mwaka 2021-2022, na atapokea tuzo hiyo kutoka kwa Katibu Mkuu  wa Umoja wa Mataifa António Guterres wakati wa hafla ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa itakayofanyika kesho Alhamisi , 26 Mei 2022 kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Tuzo hiyo ya mwanajeshi mtetezi bora wa kijinsia wa mwaka iliyoanzishwa rasmi mwaka 2016  na Umoja wa Mataifa ” inatambua kujitolea na juhudi za mlinda amani binafsi wa kijeshi katika kukuza kanuni za azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1325 linalohusu wanawake, amani na usalama, kama lilivyopendekezwa na wakuu na makamanda wa vikosi vya operesheni za amani za Umoja wa Mataifa.”

Katibu Mkuu Guterres amempongeza na kumwagia sifa Meja Zharare kwa kushinda tuzo hiyo akisema “Ni mfano wa kuigwa na mchechemuzi. Kupitia huduma yake, ameonyesha jukumu kubwa na muhimu ambalo wanawake wanalifanya katika kujenga uaminifu, kutetea mabadiliko na kuleta amani. Mfano wake unaonyesha jinsi sote tutakavyofaidikaendapo kutakuwa na wanawake zaidi katika meza ya kufanya maamuzi na usawa wa kijinsia katika operesheni za amani".

Meja Winnet Zharare, mwenye umri wa miaka  39,ameshinda tuzo ya Umoja wa Mataifa ya mwanajeshi mtetezi bora wa masuala ya jinsia kwa mwaka 2021.
UNMISS
Meja Winnet Zharare, mwenye umri wa miaka 39,ameshinda tuzo ya Umoja wa Mataifa ya mwanajeshi mtetezi bora wa masuala ya jinsia kwa mwaka 2021.

Meja Zharare kwa upande wake amelezea fahari kubwa aliyonayo na shukran zake kwa kuchaguliwa kupokea tuzo hiyo ambayo, amesema, "inampa motisha kudumisha mapambano yake yakufikia usawa wa kijinsia."

Ameongeza kuwa "Wazazi wangu walitupa fursa sawa pamoja na kaka zangu, hivyo ninaamini kuwa fursa sawa zinapaswa kutolewa kwa wanaume na wanawake katika nyanja zote za maisha".

Tweet URL

Mchango wa Meja Zharare

Meja Zharare alipelekwa UNMISS Novemba 2020. Katika huduma yake yote ya miezi 17, alitetea usawa wa kijinsia na ushiriki wa wanawake, ndani ya kikosi chake, miongoni mwa wanajeshi wa eneo hilo, na katika jamii iliyowakaribisha.

Kama afisa mkuu wa Habari za kijeshi katika ofisi ya UNMISS ya Bentiu, alisaidia kuhakikisha kuwa doria zinajumuisha wanawake na wanaume ili kuboresha juhudi za ulinzi na pia kujenga uaminifu miongoni mwa jamii  za wenyeji na mpango wa UNMISS.

Juhudi zake pia zilichangia kuongezeka kwa takwimu za kijinsia ili masuala yaliyoelezwa na wanawake na wasichana wa eneo hilo yapatiwe ufumbuzi.

Akitetea usawa wa kijinsia na ushiriki wa wanawake katika mazingira ambayo kijadi walitengwa katika kufanya maamuzi, alihimiza mamlaka za kiraia na kijeshi na wawakilishi wa jamii kuhusisha wanaume na wanawake katika mikutano na Umoja wa Mataifa.

Bidii yake na ustadi wa kidiplomasia haraka ulifanya aaminiwe na makamanda wa kijeshi wa eneo hilo ambao waliwasiliana naye kwa utaratibu kuhusu masuala yanayohusu ulinzi na haki za wanawake.

Wakati wa doria zake na mipango mingi ya ushirikishwaji wa jamii, Meja Zharare pia alifanikiwa kuwahimiza wanaume na wanawake kufanya kazi pamoja katika kilimo na katika ujenzi wa mitaro kuzunguka mji wa Bentiu ili kupunguza uhaba wa chakula na kuzuia watu kuhama zaidi.

Meja Zharare ndiye mlinda amani wa kwanza wa Zimbabwe kupokea tuzo hii ya kifahari.

Historia ya Meja Zharare

Ni mzaliwa wa eneo la Mhondoro, Zimbabwe, akitoka katika familia ya wasichana watano na wavulana wawili,

Meja Winnet Zharare alifunzwa na wazazi wake kwamba hakuna tofauti kati ya majukumu ya kijinsia nyumbani watoto wote ni sawa.

Meja Winnet Zharare alianza taaluma yake ya kijeshi mwaka wa 2006 kama Luteni wa Pili na alipelekwa kutumikia kama kamanda wa kikosi cha askari wa miguu na akishikilia jukumu la matroni, mwaka huohuo katika eneo la Mutare.

Mwaka 2009, alijiunga na kikosi cha masuala ya kiufundi na akamaliza kozi ya maafisa vijana katika chuo cha wafanyakazi cha Zimbabwe na kisha akasoma kozi ya makamanda wa kampuni katika Shule ya masuala ya vita mwaka 2014.

Baada ya hapo meja Zharare alifanya kazi kama afisa wa itifaki kuanzia mwaka 2015 hadi 2019, na kisha akateuliwa kwenda UNMISS Sudan Kusini kama mwangalizi wa kijeshi na huko nako aliteuliwa kwenda mjini Bentiu, kutimiza majukumu mengine ikiwa ni pamoja na kuwa afisa mkuu wa Habari, afisa wa mafunzo na sehemu ya kijinsia. Alihitimisha ziara yake ya kazi Sudan Kusini mwezi Aprili 2022, na sasa amerejea nchini mwake Zimbabwe.