Dkt. Tedros kuiongoza WHO kwa awamu ya pili

24 Mei 2022

Mkutano Mkuu wa 75 wa nchi wanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO uliofanyika leo jijini Geneva Uswisi umemthibitisha Dkt.Tedros Adhanom Ghebreyesus kuliongoza shirika hilo kwa awamu ya pili ya miaka 5.

Dkt .Tedros anayeliongoza shirika la WHO akiwa Mkurugenzi Mkuu tangu mwaka 2017 ataanza rasmi kipindi chake cha pili cha uongozi tarehe 16 Agosti 2022 na hiki ndio kitakuwa kipindi cha mwisho kwa mujibu wa sheria na miongozo ya shirika hilo.

Kiongozi huyu raia wa Ethiopia barani Afrika amethibitishwa rasmi baada ya kumalizika kwa mchakato wa uchaguzi ulioanza mwezi April 2021 wa kuwasilisha mapendekezo ya wagombea ya wadhifa huo wa Mkurugenzi Mkuu na kisha bodi ya utendaji ya WHO iliyokutana mwezi Januari 2022 kumteua Dkt.Tedros kuwania muhula wa pili akiwa ni mgombea pekee.

Dkt.Tedros alileta mabadiliko WHO

Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus katika uongozi wake akiwa Mkurugenzi Mkuu wa WHO anaelezwa kuanzisha mabadiliko mapana yaliyolenga kuongeza ufanisi wa shirika hilo katika ngazi za mataifa ya nchi wanachama ili kuboresha maisha ya afya, kulinda watu wengi wakati wa dharura na kuongeza usawa katika upatikanaji wa huduma ya afya.

Kiongozi huyo pia aliongoza WHO kushughulikia janga la ulimwengu la Corona au COVID-19, mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC, pamoja na athari za kiafya za majanga mengine mengi ya kibinadamu.

Historia yake kabla ya WHO

Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia kuanzia 2012-2016 na Waziri wa Afya, Ethiopia kuanzia 2005-2012. Pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria; kama mwenyekiti wa Bodi ya Ubia ya Roll Back Malaria (RBM), na kama mwenyekiti mwenza wa Bodi ya Ubia kwa ajili ya Afya ya Mama, watoto wachanga na afya ya watoto kwa ujumla.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter