Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakulima wa Embu Kenya wavalia njuga vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa kupanda miti:IFAD 

Wakulima kwa msaada wa IFAD, Serikali na wadau wanatunza msitu wa Njukiri kwa ajili ya kulinda mazingira.
IFAD/Video Capture
Wakulima kwa msaada wa IFAD, Serikali na wadau wanatunza msitu wa Njukiri kwa ajili ya kulinda mazingira.

Wakulima wa Embu Kenya wavalia njuga vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa kupanda miti:IFAD 

Tabianchi na mazingira

Kenya ni moja ya nchi zilizoathirika sana na ukame uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi katika Pembe ya Afrika, lakini sasa baadhi ya wakulima wa nchi hiyo kwa msaada wa mfuko wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo IFAD wameamua kuchukua hatua kulinda mazingira, maisha yao na kujenga mnepo kwa kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. Katika kaunti ya Embu wakulima wamepanda msitu mpya ambao unawapa sio tu jukumu jipya la kuulinda lakini pia kuwa chanzo cha kuwapatia kipato.

Katika msitu mpya wa Njukiri kwenye kaunti ya Embu kilichotawala ni kijani kibichi  kila pembe, na ni vigumu kuamini kwamba miaka sita tu iliyopita msitu huu haukuwepo. 

Programu kubwa ya upandaji miti ambayo ni sehemu ya mradi wa IFAD, kwa ushirikiano na serikali ya Kenya na Hispania umebadili kabisa mandhari ya eneo hili la ekari 2982 za ardhi iliyokuwa imemomonyoka na kuwa msitu mnene wa kijani. 

Na sasa ni maskani ya maelfu ya aina za mimea na wanyama yaani Flora na Fauna.  

Pia linatoa kipato kwa wakulima ambao wanaruhusuiwa kupanda mazao kwa mbadala wa kuilinda misitu huo. Simon Kangele Wambua ni mwenyekiti wa jumuiya ya msitu wa Njukiri,“Kazi yetu ni ya kupanda miti na kuzuia mmomonyoko wa udongo na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hapa kile kinachofanya pawe pazuri kwa ukulima ni kwa sababu matawi haya ya miti na hasa miti ya kienyeji yakianguka yanatengeneza kama mbolea, tunapolima kitu cha kwanza tunachofanya ni kuvuna, tunakata miti na kwa muda wa miaka miwili tunapanda mahindi, maharagwe na viazi na baada ya hapo sasa tunapanda miti na kuihudumia vyema kwa hivyo udongo wa hapa una rutuba nzuri sana kwa kilimo.” 

Kwa muongo mmoja uliopita Kenya kama nchi zingine za Afrika Mashariki imekuwa ikishuhudia ukame mkali ambao ni matokeo ya mabadiliko ya tanianchi. Lakini sasa asante kwa msitu huu wananchi wa Embu wanapata mvua kutokana na miti mingi iliyopandwa hapa. Margaret Wanjeru wa Kiragu ni mkulima kwenye msitu huu anasema, “Tangu tumeanza kulima hapa kuna tofauti kubwa hasa ukizingatia kuna miti inayochagiza mvua, hivyo kuna tofauti kati ya vijiji vingine na hapa, hata wakati wa jua kali hapa bado tunapata chakula kwa sababu tuna miti inayoleta mvua.” 

Mradi huu unawachagiza wakulima kuishi kwa amani na wanayama pori ingawa Margaret anasema hilo wakati mwingine linakuwa ni changamoto lakini wanayoweza kuikabili. 

Hadi sasa mradi umeshawasaidia wakulima zaidi ya 1000 kufanya kazi na kuendesha maisha yao msituni hapa na msitu unaendelea kukua kwani bado kuna ekari zingine 3500 zinazosubiri kupandwa miti.