Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Anuwai za kibayolojia kote ulimwenguni ziko hatarini kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Tuhusishe kila mtu kuokoa anuwai za kibailojia: Guterres

© Unsplash/Zdeněk Macháček
Anuwai za kibayolojia kote ulimwenguni ziko hatarini kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Tuhusishe kila mtu kuokoa anuwai za kibailojia: Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ili dunia kufikia mustakabali endelevu kwa wote,inahitaji kuchukua hatua za haraka za kulinda bioanuwai.Guterres amesema hayo katika taarifa yake ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya utofauti wa anuwai za kibaiolojia na kusisitiza kuwa “ni lazima tukomeshe vita vyetu visivyo na maana vya uharibifu dhidi ya asili.”

Ameeleza katika taarifa yake kuwa Kiwango cha vita ya uharibifu wa asili ni kubwa kwa makumi na mamia tofauti na miaka 10 iliyopita na hali ya uharibifu inaendelea kwa kasi.
Guterres ametoa wito kwa watu wote duniani kuchukua hatua za hataka kujenga mustakabali wa pamoja kwa manufaa ya maisha ya wote ili kuokoa utajiri wa asili wa lazima na dhaifu wa sayari yetu, kila mtu anahitaji kujumuika kushughulikia changamoto hizo ikiwa ni pamoja na vijana na watu wanaoishi katika mazingira magumu ambao wanategemea zaidi asili kwa ajili ya maisha yao. 
Amekumbusha kuwa “Bioanuwai ni muhimu tunapotaka kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu, kukomesha tishio lililopo la mabadiliko ya tabianchi, kusitisha uharibifu wa ardhi, kujenga usalama wa chakula na kusaidia maendeleo katika afya ya binadamu na viumbe hai hutoa ufumbuzi tayari kwa ukuaji wa kijani na jumuishi.”

Serikali zina jukumu kubwa

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa mwaka huu serikali zitakutana ili kukubaliana juu ya mfumo wa bioanuwai wa kimataifa wa baada ya mwaka 2020, wenye shabaha zilizo wazi na zinazoweza kupimika na njia thabiti za utekelezaji ambazo zinaweza kurejesha bayoanuwai ifikapo mwaka 2030.
“Mfumo huo lazima ushughulikie vichochezi vya upotevu wa bayoanuwai na kuwezesha mabadiliko kabambe na yakimageuzi yanayohitajika ili kuishi kwa amani na asili kwa kulinda kwa ufanisi zaidi ardhi ya dunia, maji safi na bahari, kuhimiza matumizi na uzalishaji endelevu, kutumia ufumbuzi wa asili kushughulikia hali ya hewa, kubadilisha na kukomesha ruzuku zenye madhara zinazoharibu mazingira. 
Guterres ameongeza kuwa inapaswa kuhamasisha hatua na rasilimali za kifedha ili kuendesha uwekezaji halisi wa asili, kuhakikisha kwamba sote tunanufaika kutokana na faida za bioanuwai.
“Tunapotimiza malengo haya na kutekeleza Dira ya 2050 ya "kuishi kwa upatano na asili", lazima tuchukue hatua kwa kuheshimu usawa na haki za binadamu, hasa kuhusiana na wakazi wengi wa kiasili ambao maeneo yao yana anuwai nyingi za kibaiolojia.”