Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Mwanamke akivuna majani ya chai katika eneo la Mto Tana nchini Kenya

Wazalishaji wa chai waunganishe nguvu kwenye mapambano ya mabadiliko ya tabianchi

© CIAT/Georgina Smith
Mwanamke akivuna majani ya chai katika eneo la Mto Tana nchini Kenya

Wazalishaji wa chai waunganishe nguvu kwenye mapambano ya mabadiliko ya tabianchi

Tabianchi na mazingira

Leo ni siku ya chai duniani, chai ni kinywaji kinachotengenezwa kutoka kwa mmea wa Camellia sinesis na ni kinywaji kinachotumiwa zaidi ulimwenguni baada ya maji.

Inaaminika kuwa chimbuko la chai ni kaskazini mashariki mwa India, kaskazini mwa Myanmar na kusini magharibi mwa China, lakini mpaka sasa haijulikani wapi kulikuwa mahali halisi ambapo mmea ullikua.

Kinywaji cha chai kimekuwa kikitumika ulimwenguni kwa muda mrefu na kuna ushahidi kwamba chai ilitumiwa nchini China miaka 5,000 iliyopita.

Uzalishaji na usindikaji wa chai ni chanzo kikuu cha mapato kwa mamilioni ya familia katika nchi zinazoendelea na ndio njia kuu ya kujikimu kwa mamilioni ya familia maskini, ambazo zinaishi katika nchi zinazoendelea. 

Uzalishaji na usindikaji wa chai huchangia katika kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu SDG kadhaa ikiwemo lile ya kupunguza umaskini uliokithiri (Lengo 1), mapambano dhidi ya njaa (Lengo 2), uwezeshaji wa wanawake (Lengo la 5) na matumizi endelevu ya mifumo ikolojia ya nchi kavu (Lengo 15).

Uzalishaji wa chai na Mabadiliko ya tabianchi

Hali ya hewa kubadilika mara kwa mara ni suala linalopaswa kuangaliwa kwenye uzalishaji wachai kwakuwa linaweza kuwa na athari kwenye ukuaji wa chai.

Chai inaweza tu kuzalishwa katika hali ya mazingira ya kilimo-ikolojia na, kwa hiyo si nchi zote zao hili linaweza kustawi na mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuathiri hata nchi ambazo zinajulikana kwa uzalishaji wa chai.

Mabadiliko ya hali ya joto na mvua, pamoja na mafuriko na ukame mkali, tayari yanaathiri mavuno, ubora wa bidhaa ya chai na bei, kupunguza mapato na kutishia maisha ya vijijini. 

Mabadiliko haya ya tabianchi yanatarajiwa kuongezeka, na hivyo zinatakiwa hatua za haraka kuchukuliwa ili kuweza kukabiliana nayo ikiwemo kupunguza uzalishaji wa kaboni kutoka kwenye uzalishaji na usindikaji wa chai.

Kwa hivyo, nchi zinazozalisha chai zinapaswa kuunganisha, changamoto za mabadiliko ya tabianchi katika kukabiliana na kuwa na mikakati madhubuti ya kitaifa ya maendeleo ya chai.