Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna nchi iliyo na kinga dhidi ya njaa, lazima tuchukue hatua sasa:UN 

Chakula kinasambazwa kwa watu 450,000 kaskazini mwa Ethiopia walioathiriwa na mzozo.
© WFP/Sinisa Marolt
Chakula kinasambazwa kwa watu 450,000 kaskazini mwa Ethiopia walioathiriwa na mzozo.

Hakuna nchi iliyo na kinga dhidi ya njaa, lazima tuchukue hatua sasa:UN 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameliambia Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba vita vinapozuka, watu wanakabiliwa na njaa, na kwamba asilimia 60 ya watu wasio na lishe bora duniani wanaishi katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro huku akikumbusha kuwa "Hakuna nchi iliyo na kinga dhidi ya njaa,"  

Akizungumza leo katika mkutano wa Baraza hilo mjini New York Marekani kuhusu migogoro na uhakika wa chakula Antonio Guterres amesema mwaka jana, asilimia kubwa ya watu milioni 140 wanaokabiliwa na njaa kali duniani kote waliishi katika nchi kumi tu ambazo ni Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Ethiopia, Haiti, Nigeria, Pakistan, Sudan Kusini, Sudan, Syria na Yemen na kwamba nchi nane kati ya nchi hizi ziko kwenye ajenda ya Baraza la Usalama 

Ameongeza kuwa “Ni bayana kwamba Baraza hili linapojadili migogoro, mnajadili njaa. mnapofanya maamuzi kuhusu ulinzi wa amani na operesheni za kisiasa, mnafanya maamuzi kuhusu njaa. Na mnaposhindwa kufikia muafaka, watu wenye njaa hulipa gharama kubwa,”  

Guterres amesema mgogoro wa Ukraine pia umechochea tatizo la njaa akilikumbusha Baraza kuwa “Hadi mwezi Machi mwaka huu Ukraine ilikuwa inailisha dunia kwa chakula chake kingi lakini sasa inategemea msaada wa chakula ambapo mwezi Aprili shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limegawa chakula kwa zaidi watu milioni 3 nchini Ukraine.” 

Kundi la wanawake nchini Guinea wamepanda miti ya Moringa ambayo inasaidi kuepusha mmomonyoko wa udongo.
UN Women/Joe Saade
Kundi la wanawake nchini Guinea wamepanda miti ya Moringa ambayo inasaidi kuepusha mmomonyoko wa udongo.

Msaada wa dola milioni 30 kutoka CERF 

Ili kusaidia kukabiliana na mgogoro huu wa njaa unaoendelea kuongezeka Katibu Mkuu amesema , “ninafuraha kutangaza leo kwamba tunatoa dola milioni 30 kutoka mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF, ili kukidhi mahitaji ya dharura ya uhakika wa chakula na lishe nchini Niger, Mali, Chad na Burkina Faso. Lakini ni tone katika bahari na fedha hizo zitafanya jumla ya fedha zilizotolewa na CERF kwa Sahjel tangu mwanzoni mwa mwaka huu kufikia dola milioni 95.” 

Pia amesema anatiwa hofu na changamoto ya kutokuwa na uhakika wa chakula Pembe ya Afrika kutokana na ukame ambao haujawahi kushuhudiwa kwa takriban miongo minne. 

Watu milioni 18 wameathirika huku WFP ikionya kwamba mathalani Somalia mamilioni ya watu wako kwenye hatihati ya baa la nja katika miezi michache ijayo. 

Duniani kote watu milioni 49 katika nchi 43 wako kwenye kiwango cha hatari na cha dharura cha njaa huku waathirika wakubwa wakiwa ni wanawake, wasichana na watoto na vita vya Ukraine vimezidisha madhila 

Vita lazima vikomeshwe 

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka hatua zichukuliwe kukomesha vita ambavyo ni chachu kubwa ya njaa duniani  kwa kusisitiza mambo manne  

  • Mosi: Ametoa wito kwa wanachama wote wa Baraza kufanya kila wawezalo katika uwezo wao kunyamazisha mtutu wa bunduki na kuendeleza amani, nchini Ukraine na kila mahali. 
  • Pili: ametaka sheria ya kimataifa ya kibinadamu, iliyoainishwa katika azimio namba 2417 la Baraza la Usalama, inayobainisha kuwa bidhaa na vifaa ambavyo ni muhimu kwa maisha ya raia ikiwa ni pamoja na chakula, mazao na mifugo ni lazima vilindwe. Pia inasema kuwa wahudumu wa kibinadamu lazima wawe na fursa zisizo na kipingamizi za kuwafikia raia wanaohitaji msaada. “Baraza hili lina jukumu muhimu katika kudai utekelezaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu, na kufuatilia uwajibikaji unapokiukwa. Nawaomba mchukue hatua za juu ili kutimiza wajibu wenu.” 
  • Tatu:amesema hatari zinazoingiliana za uhaba wa chakula, nishati na ufadhili zinahitaji uratibu na uongozi mkubwa zaidi. 

Kwani amesema “kuna chakula cha kutosha kwa kila mtu ulimwenguni. Suala ni usambazaji, na linahusishwa sana na vita ya Ukraine.” 

Na nne: Amewagukia wafadhili akisema ni lazima wafadhili maombi ya msaada wa kibinadamu kwa ukamilifu. 

“Takriban nusu ya mwaka wa 2022, Mipango yetu ya maombi ya msaada wa kibinadamu duniani yamefadhiliwa kwa asilimia 8 pekee.”Amesema Guterres 

Na kuongeza kuwa hiki ni kiasi kidogo, ninaomba nchi zionyeshe ukarimu sawa kwa nchi zote kama zinavyoonyesha kwa Ukraine. Kulisha wenye njaa ni uwekezaji katika amani na usalama wa kimataifa. Katika ulimwengu wetu uliojaaliwa vitu tele, sitakubali kamwe kifo kitokanacho na njaa mtoto, mwanamke au mwanamume hata mmoja wala nanyi wajumbe wa Bsaraza hampaswi kulikubali hilo.”