Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaadhimisha siku ya kwanza ya kimataifa kuwaangazia wanawake wanaofanya kazi katika tasnia ya bahari 

Bahari akiwa katika mafunzo
IMO
Bahari akiwa katika mafunzo

UN yaadhimisha siku ya kwanza ya kimataifa kuwaangazia wanawake wanaofanya kazi katika tasnia ya bahari 

Wanawake

Siku ya kwanza ya Kimataifa ya Wanawake katika Usafiri wa Baharini imeadhimishwa leo tarehe 18 Mei 2022 ikiwa ni mara ya kwanza na ikiwa na lengo la kutoa jukwaa la kuangazia na kusherehekea mafanikio ya wanawake katika bahari na kubainisha maeneo ya kuboreshwa kwa ajili ya usawa wa kijinsia. 

Siku hii ya kwanza ya Kimataifa ya Wanawake katika ubaharia au shughuli za baharini inaangazia mada au kaulimbiu ya "Mafunzo-Kuonekana-Utambuzi: Kusaidia mazingira ya kazi yasiyo na vizuizi." 

Katibu Mkuu wa IMO Kitack Lim amenukuliwa akisema kuwa, “bado hakuna usawa wa kijinsia katika shughuli za baharini lakini nyakati zinabadilika. Inatambulika kuwa tofauti katika usafiri baharini hunufaisha sekta nzima. Wanawake wa baharini wanafanya kazi kila mahali ili kuunga mkono mabadiliko ya maisha yajayo yaliyopunguzwa kaboni, ya dijitali na endelevu zaidi.” 

Bwana Lim anaongeza akisema, "hebu tuchukue fursa hii kusherehekea wanawake wengi wanaochangia mustakabali wa baharini: kudumisha injini kwenye meli, kuendesha kampuni, kuandaa kandarasi, kupima meli, au kuongoza mkutano wa kamati wa IMO. Ingawa kuna mengi ya kusherehekea, pia kuna haja ya maendeleo zaidi kufanyika." 

Utafiti  wafichua kukosekana kwa usawa 

Tofauti za kijinsia katika shughuli za baharini zimegawanyika sana kisekta, kwa mujibu wa data za Ripoti ya Utafiti wa Wanawake katika Ubaharia au shughuli za baharini.  

Ripoti hiyo IMO-WISTA (Chama cha Kimataifa cha Usafirishaji na Biashara Baharini cha Wanawake IMO-WISTA iliyozinduliwa katika Siku ya kwanza ya Kimataifa ya Wanawake katika Usafiri wa Baharini, ina taarifa kuhusu uwiano na usambazaji wa wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya baharini kutoka Nchi Wanachama wa IMO na sekta ya baharini kiujumla. Data zinaonesha kuwa wanawake wanachangia asilimia 29 pekee ya wafanyakazi wote katika tasnia nzima na asilimia 20 ya nguvu kazi ya mamlaka ya kitaifa ya baharini katika Nchi Wanachama. 

Utafiti huu wa WISTA unachangia juhudi za kuunga mkono Lengo la 5 la Maendeleo Endelevu kuhusu usawa wa kijinsia. 

Wanawake katika kazi 

Aidha ripoti hiyo inaangazia tofauti kubwa kati ya sekta ndogo za kibinafsi. Kwa mujibu wa takwimu iliyokusanywa kutoka kwa Mataifa Wanachama, timu za utafutaji na uokoaji katika mamlaka ya kitaifa ya baharini zinachukua wafanyakazi wachache sana wanawake (asilimia 10 tu ikilinganishwa na wanadiplomasia wa kike (asilimia 33) na wafanyakazi wa mafunzo (asilimia 30). Takwimu za tasnia zinaonyesha kuwa mabaharia wanawake ni asilimia 2 tu ya wafanyakazi na wanapatikana zaidi katika sekta ya meli za starehe, wakati katika kampuni za umiliki wa meli ni asilimia 34 ya wafanyakazi. 

Rais wa Kimataifa wa WISTA, Despina Panayiotou Theodosiou amesema, "maarifa ambayo tumekusanya kuhusu tofauti za kijinsia katika tasnia ya bahari kupitia Utafiti huu wa kwanza wa Wanawake katika Utafiti wa Bahari wa 2021 ni hatua muhimu katika azma yetu ya kuunda utofauti kamili wa kijinsia. Kama mukhtasari wa kwanza, uchunguzi huu unatoa ushahidi unaoonesha ni kazi ngapi bado inahitajika kufanywa. Lakini pia inatuonesha ambapo kuna mwanga. Sekta ya bahari inaweza kujionea yenyewe ni sekta zipi zinazosonga mbele kwa ujumuishaji wanawake na wanaume, na zipi hazina.”