Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walionyanyaswa kijinsia washukuru Mfuko wa UN kufadhili miradi yao Kavumu, DRC  

Umoja wa Mataifa unafanya kazi na jamii Kavumu, DRC kwa ajili ya kuelimisha watu kuhusu ukatili wa kijinsia.(Picha ya maktaba)
MONUSCO/Alain Likota
Umoja wa Mataifa unafanya kazi na jamii Kavumu, DRC kwa ajili ya kuelimisha watu kuhusu ukatili wa kijinsia.(Picha ya maktaba)

Walionyanyaswa kijinsia washukuru Mfuko wa UN kufadhili miradi yao Kavumu, DRC  

Haki za binadamu

Miaka sita iliyopita, yaani mwaka 2016, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliunda Mfuko wa kufadhili miradi inayolenga kusaidia waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia na hata watoto waliozaliwa kutokana na ukatili wa kingono uliofanywa na baadhi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wakiwemo walinzi wa amani au watu wengine wanaohusika na shughuli za Umoja wa Mataifa katika mataifa mbalimbali. 

Kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, usaidizi kwa waathiriwa, “ndio kiini cha mwitikio wetu kwa unyanyasaji wa kingono unaofanywa na wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa.” 

Kufikia Februari mwaka huu 2022, Nchi Wanachama 24 ziliuchangia fedha mfuko huu, na wafadhili wapya watano walijiunga mwaka 2021. 

Umoja wa Mataifa unaeleza kuwa Mfuko una zaidi ya dola za kimarekani 4.3 milioni katika michango ambayo inajumuisha malipo ambayo yamezuiwa kutoka kwa wahusika wa matendo hayo ya unyanyasaji ikiwa ni njia mojawapo ya kuwawajibisha. 

Kwa kushirikiana na Nchi Wanachama, Umoja wa Mataifa umeendelea kusaidia kutambua haki na utu wa waathirika wa matendo hayo yasiyofaa yanayofanywa na baadhi ya watu wasio waadilifu katika familia kubwa ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa. 

Kwa kufanya hivyo, Umoja wa Mataifa, kupitia mfuko huu  umekuwa ukiwasaidia waathirika wa unyanyasaji huu wa kijinsia na ukatili wa kingono. 

Miongoni mwa waliofadhiliwa ni shirika lisilo la kiserikali la Kavumu Community Based Complaint Network katika mji mkuu wa Kivu Kusini, Bukavu, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. 

Mwa Cidende, mmoja wa wanufaika akiwa na wenzake katika ofisi yao ya kushona na kuuza nguo, kwa niaba ya wenzake hakusita kuonesha furaha yake walipotembelewa na Rais wa shirika hilo, Zawadi Bagaya Basilienne ambaye kupitia kwake, wanawake hawa walipata elimu ya ushoni na sasa wanaendesha maisha yao kwa kazi hii. 

“Tulikuwa watu ambao hatukuwa tunajiweza.” Ndivyo anavyoanza kueleza Mwa Cinende akiwa amembeba mtoto wake mdogo mgongoni. Kisha anaendelea akieleza maisha yalivyobadilika baada ya kupokea vyerehani kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Kavumu Community Based Complaint Network ambalo limepata ufadhili kutoka mfuko huu wa Umoja wa Mataifa.  

Mama huyu anaeleza kuwa yeye na wenzake wamepitia mateso mengi. Mtoto huyu aliyembeba mgongoni ni wa 13 wa kumzaa mwenyewe, ingawa wamesalia watoto 10.  

“Huyu mtoto wa 10 nilimzaa nikiwa nimeshapata hii machine kutoka kwa Mama Zawadi (Zawadi Bagaya Basilienne). Ilinisaidia sana ten asana kulipa gharama za kujifungua. Hadi leo hii mashine inaendelea kunisaidia.” Anaeleza Mwa Cidende akionesha mashine ya kushonea nguo na pia nguo zenyewe ambazo wamezishona. Nyingi ni nguo za vitenge, magauni mazuri ya wanawake.  

Kwa niaba ya wenzake Bi Cidende anatoa shukrani akisema, “tunasema asante sana na nyinyi ambao mlienda kututafutia (ufadhili), msichoke, kesho mtutafutie, maendeleo yaendelee. Mungu awabariki.” Anaongea akitabasamu na anaongoza wimbo mfupi wa hamasa akisema “Mama enyanyaa”, na wenzake wote wanaitikia, “Enyanyaa”, ikifuatiwa na vicheko vya furaha.