Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fikra potofu kuhusu mimba zisizotarajiwa -Sehemu ya kwanza

Dankay Kanu mwenye umri wa miaka 14 alipata ujauzito baada ya kushiriki kimapenzi na mwanamume mkubwa wake kwa umri ambaye alikataa majukumu kama baba.
@ UNFPA/Michael Duff
Dankay Kanu mwenye umri wa miaka 14 alipata ujauzito baada ya kushiriki kimapenzi na mwanamume mkubwa wake kwa umri ambaye alikataa majukumu kama baba.

Fikra potofu kuhusu mimba zisizotarajiwa -Sehemu ya kwanza

Utamaduni na Elimu

Nusu ya ujauzito ambao wanawake na wasichana wanabeba si wao wameamua. Hili ni janga ambalo limepuuzwa. Imesema UNFPA, ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi kupitia ripoti yake ya hali ya Idadi ya Watu Duniani kwa mwaka huu wa 2022. 

Kila mwaka kuna  ujauzito milioni 121 ambazo hazikupangwa au mwanamke au msichana hakuchagua kuubeba. Hii ina maana ujauzito 331, 000 kila siku na idadi inaweza kuongezeka kama hakuna hatua zinachukuliwa. 

Uwezo wa kuamua kuwa kuwa na mtoto au la, idadi yao na nani kuzaa naye, ni  uamuzi wa msingi katika afya ya uzazi kwa wasichana na wanawake. Haki hii inapopuuzwa au kupondwa na vikwazo vya kijamii, ukatili, ukosefu wa huduma za afya au kupuuzwa kwa masuala ya wanawake ambao ni nusu ya idadi ya binadamu athari zake huongezeka kwa kasi. 

Mimba zisizopangwa zinaathiri maisha ya mtu mmoja mmoja na jamii nzima; hukwamisha maendeleo ya afya, elimu na usawa wa jinsia, huongeza umaskini na fursa. 

UNFPA inataka dunia ambamo kwayo kila ujauzito unatakiwa. Sasa UNFPA inataka ufahamu fikra potofu 4 kuhusu mimba zisizotarajiwa ili kukomesha aibu, unyanyapaa na kutokuelewa kulikoshamiri. 

1:  Ni wanawake makahaba na vijana balehe wasio na adabu ndio hupata mimba zisizotarajiwa 

 Mwanamke yeyote mwenye uwezo wa kubeba ujauzito, bila kujali umri wake, ameolewa au la, alikotoka, anaweza kupata ujauzito bila kutaraji, kama ilivyo kwa watu wasiojitambulisha kama wanawake. Kulaumu kiwango cha juu cha ujauzito usiotarajiwa kwa jinsia moja ni fikra potofu. 

Mathalani njia za uzazi wa mpango zinaendelea kupatikana, lakini hakuna mbinu ambayo ina uhakika asilimia 100. Mbinu ya kutofanya ngono inaweza kushindikana kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo matumizi ya nguvu na  mizozo. Ukosefu wa usawa, umaskini, aibua, hofu na ukatili wa kijinsia vinaweza pia kupora wanawke na wasichana uwezo wa uamuzi juu ya miili yao na afya ya uzazi. 

Wanaume wana nafasi kuu: Duniani kote robo ya wanawake wanashindwa kukataa kufanya ngono. Ubakaji husababisha ujauzito usiotakiwa katika kiwango ambacho ni sawa au kikubwa kuliko kujamiiana kwa makubaliano. 

Wanawake wote: vijana au wazee, walioolewa au wasioolewa, wanaojamiiana au wasiojamiiana, waliobadili jinsia na wengineo wote wako hatarini iwapo wana uwezo wa kubeba ujauzito. 

Yajaira Alberto alipata ujauzito baada ya kushiriki ngono mara ya kwanza akiwa na miaka 16 kwa sababu hakujua kuhusu njia za kupanga uzazi na akiwa na umri wa miaka 34 baada ya mbinu ya kupanga uzazi kufeli.
© UNFPA/Wilton Castillo
Yajaira Alberto alipata ujauzito baada ya kushiriki ngono mara ya kwanza akiwa na miaka 16 kwa sababu hakujua kuhusu njia za kupanga uzazi na akiwa na umri wa miaka 34 baada ya mbinu ya kupanga uzazi kufeli.

2: Wanawake hawatumii njia za uzazi wa mpango kwa kuwa hawazifahamu au hawana 

Duniani kote, takribani wanawake milioni 257 wanaotaka kuzuia ujauzito hawatumii mbinu salama za  uzazi wa mpango. Kati yao hao milioni 172 hawatumii njia zozote kabisa. Kutotambua au kukosa mbinu hizo ni moja ya sababu zisizotajwa kuwa sababu za kutotumia. Sababu kubwa zinazotajwa ni madhara yake, kutokujamiana au kupinga matumizi ya kondomu na mbinu nyingine. Taarifa potofu kuhusu madhara ya muda mrefu kwenye uzazi huongeza hofu juu ya mbinu za uzazi wa mpango. 

UNFPA inasisitiza upatikanaji wa njia za uzazi wa mpango, ikisambaza kondomu milioni 724 za kiume, vidonge vya uzazi wa mpango vya mizunguko milioni 80 na makumi ya mamilioni ya aina nyingine ya mbinu za uzazi wa mpango kwa mwaka 2020 pekee. Upatikanaji ni muhimu lakini kushughulikia vikwazo vya kibinafsi na vya kijamii vya kupata hudumu hizo ni muhimu pia. 

3: Uwepo wa huduma za kutoa mimba hushawishi wanawake kujamiiana bila kinga 

Ambako utoaji mimba unaruhusiwa, kiwango cha ujauzito usiotarajiwa ni kidogo kuliko kule ambako hairuhusiwi. 

Sababu? Uhusiano kati ya ujauzito usiotarajiwa, kupata huduma salama za utoaji wa mimba na kiwango cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii. 

Sheria legezi za utoaji mimba hazina uhusiano wowote na mtu kuamua kutoa au kutotoa. Badala yake, sheria hizo ziko kule ambako haki za wanawake na wasichana zinaheshimiwa na huduma za afya ya uzazi zinapatikana kwa watu wote wenye umri wa kuweza kujamiiana. 

Kwa kifupi ni kwamba wanawake wanapokuwa na uwezo wa kupata huduma sahihi za afya na kuweza kufurahia haki zao juu ya miili yao, viwango vya mimba zisizotarajiwa hupungua bila kujali uwepo au kutokuwepo kwa sheria za utoaji mimba. 

Ukosefu wa taarifa au uelewa kuhusu ngono na afya ya uzazi umechangia msichana wa miaka 18 kupata mimba isiyo tarajiwa huko Timor Leste
© UNFPA/Ruth Carr
Ukosefu wa taarifa au uelewa kuhusu ngono na afya ya uzazi umechangia msichana wa miaka 18 kupata mimba isiyo tarajiwa huko Timor Leste

4: Mimba isiyotarajiwa ni kosa la mtu Fulani. Aibu tunavyozipinga 

Wakati mimba isiyotarajiwa kwa mtu binafsi ni matokeo ya kujamiiana bila kinga, sababu kubwa mara nyingi ni jamii. Tafiti zinaonesha kuwa viwango vya mimba hizo hotufatiana kati ya nchi na nchi na kulingana na kiwango cha maendeleo. 

Mazingira ya kiuchumi na kijamii kama vile kipato, elimu, usawa wa kijinsia na upatikanaji wa huduma za afya, yana mchango mkubwa katika kuona iwapo mwanamke anaweza kupata mimba bila kutarajia au la. 

Kuona suala hilo kama wajibu wa mtu mmoja ni kupuuza mambo ya msingi. 

Na inaweza kuwa hatari, Unyanyapaa dhidi ya mimba zisizotarajiwa huongeza vikwazo vya kupata huduma za uzazi wa mpango kwa vijana balehe na wanawake wasioolewa na hivyo kukwamisha uwezo wao wa kupata huduma za taarifa kuhusu mbinu za kukinga mimba. Na baya zaidi ni pale wanaonyanyapaliwa ni wanawake badala ya wanaume waliowatia mimba. Mfano mauaji ya kuua ili kuleta heshima, kitendo kinachokumba wanawake na wasichana. 

Fuatilia kupata sehemu ya pili.