Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti mpya ya UNICEF yaonya kuhusu tatizo la uzito mdogo kwa watoto  

Mvulana wa miezi 4 ananyonywa kwa kijiko na mfanyakazi katika kituo cha utulivu cha watoto wenye utapiamlo huko Multan, Pakistani.
© UNICEF/Giacomo Pirozzi Mtoto wa miezi minne akilishwa na muhudumu wa afya hospitali, jimbo la Punjab, Pakistan.

Ripoti mpya ya UNICEF yaonya kuhusu tatizo la uzito mdogo kwa watoto  

Afya

Idadi ya watoto walioathirika na uzito mdogo wa kupindukia imekuwa ikiongezeka hata kabla ya vita ya Ukraine ambayo inatishia kuitumbukiza dunia kwenye mgogoro mkubwa wa chakula imeonya ripoti mpya kuhusu watoto iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Ripoti hiyo yenye jina, "Upotevu mkubwa wa uzito, dharura iliyopuuzwa ya maisha ya mtoto” inaonesha kwamba licha ya kuongezeka kwa viwango vya watoto walio na uzito mdogo wa kupindukia na kupanda kwa gharama za matibabu ya kuokoa maisha, ufadhili wa kimataifa wa kuokoa maisha ya watoto wanaoteseka pia uko hatarini. Uzito mdogo wa kupindukia ni pale ambapo watoto wanakuwa wembamba sana kuliko urefu wao kutokana na kutokuwa na kinga mwilini. 

"Hata kabla ya vita ya Ukraine kuhatarisha uhakika wa chakula duniani kote, migogoro, majanga ya hali ya hewa na coronavirus">COVID-19 tayari vilikuwa vinaharibu uwezo wa familia kulisha watoto wao." Amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell. 

Mama wa Kisomali akimbeba mwanawe mdogo kwenye kitanda cha hospitali katika Kituo cha Udhibiti wa Hospitali ya Gode nchini Ethiopia, huku akipokea matibabu ya lishe kwa utapiamlo.
© UNICEF/Zerihun Sewunet Mtoto akipokea matibabu ya lishe katika kituo kinachofadhiliwa na UNICEF, Somali, Ethiopia.

Kwa sasa, angalau watoto milioni 10 walio na uzito mdogo kupindukia au watoto 2 kati ya 3 hawana uwezo wa kupata matibabu ya uhakika ya tatizo lao hilo, chakula cha matibabu kilicho tayari kutumika (RUTF). 

UNICEF inaonya kwamba mchanganyiko wa mishtuko ya kimataifa kwa uhakika wa chakula ulimwenguni inayoongozwa na vita vya Ukraine, uchumi unaopambana na kupona kutoka katika janga la Covid-19, na hali ya ukame inayoendelea katika baadhi ya nchi kutokana na mabadiliko ya tabianchi, inaleta hali ya ongezeko kubwa la viwango vya kimataifa vya uzito mdogo kupindukia. 

Wakati huo huo, bei ya chakula cha matibabu kilicho tayari kutumika inakadiriwa kuongezeka kwa hadi asilimia 16 katika muda wa miezi sita ijayo kutokana na kupanda kwa kasi kwa gharama ya malighafi. Hii inaweza kuacha hadi watoto 600,000 wa ziada bila kupata matibabu ya kuokoa maisha katika viwango vya sasa vya matumizi. “Gharama za usafirishaji na usambazaji pia zinatarajiwa kubaki juu.” Imeeleza UNICEF. 

Ripoti  imeeleza kuwa duniani kote takribani watoto milioni 13.6 wa umri wa chini ya miaka 5 wana tatizo la uzito mdogo wa kupindukia na kusababisha kifo 1 kati ya 5 kwa watoto wa kundi hilo. 

Asia Kusini inasalia kuwa ‘kitovu’ cha uzito mdogo wa kupindukia, ambapo takriban mtoto 1 kati ya 22 ana uzito mdogo kupindukia, mara mbili zaidi ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Na kote ulimwenguni, nchi zinakabiliwa na viwango vya juu vya upotevu mkubwa kihistoria. Nchini Afghanistan, kwa mfano, watoto milioni 1.1 wanatarajiwa kuteseka kutokana na uzito mdogo mwaka huu, karibu mara mbili ya idadi ya mwaka 2018. Ukame katika Pembe ya Afrika unamaanisha kwamba idadi ya watoto walio na uzito mdogo inaweza kuongezeka haraka kutoka milioni 1.7 hadi milioni 2. wakati ongezeko la asilimia 26 linatabiriwa katika Sahel ikilinganishwa na mwaka 2018. 

Aidha ripoti imebainisha kuwa hata nchi zilizo katika hali ya uimara kama vile Uganda, zimeshuhudia asilimia 40 au zaidi ya uzito mdogo wa tangu mwaka 2016, kutokana na kuongezeka kwa umaskini na uhaba wa chakula cha kaya na matatizo ya ubora na mzunguko wa mlo kwa watoto na wajawazito.  

Ili kufikia kila mtoto na matibabu ya kuokoa maisha dhidi ya uzito mdogo kupindukia, UNICEF inatoa wito kwa: 

·       Serikali kuongeza misaada katika suala la uzito mdogo kwa angalau  asilimia 59 juu ya viwango vya mwaka 2019 ili kusaidia kufikia kusaidia watoto wote wanaohitaji matibabu katika nchi 23 zenye mzigo mkubwa. 

  •        Nchi zijumuishe matibabu ya uzito mdogo wa kupindukia wa watoto katika mipango ya afya na ufadhili wa maendeleo ya muda mrefu ili watoto wote wanufaike na programu za matibabu, na sio tu zile nchi zilizo katika mazingira ya shida ya kibinadamu. 
  •      Kuhakikisha kwamba mgao wa bajeti kushughulikia janga la njaa duniani ni pamoja na mgao maalum kwa ajili ya afua za chakula cha matibabu ili kushughulikia mahitaji ya haraka ya watoto wanaokabiliwa na uzito mdogo kupindukia. 
  •        Wafadhili na mashirika ya kiraia kuweka kipaumbele cha fedha kwa ajili ya tatizo la uzito mdogo ili kuhakikisha mfumo tofauti, unaokua na wenye afya wa usaidizi wa wafadhili. 

"Hakuna sababu kwa nini mtoto ateseke kutokana na uzito mdogo kupindukia. Sio katika wakati ambao tuna uwezo wa kuzuia. Lakini kuna wakati mdogo wa kuamsha juhudi za kimataifa za kuzuia, kugundua na kutibu utapiamlo kabla hali mbaya haijawa mbaya zaidi.” Amesema  Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF.