Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban watoto na wazee bilioni moja wenye uhitaji wa teknolojia ya usaidizi wamekosa fursa ya ufikiaji

Mwanamke akiwekewa kifaa cha kumsaidia kusikia.
Unsplash/Mark Paton
Mwanamke akiwekewa kifaa cha kumsaidia kusikia.

Takriban watoto na wazee bilioni moja wenye uhitaji wa teknolojia ya usaidizi wamekosa fursa ya ufikiaji

Haki za binadamu
  • Upatikanaji wa vifaa vya usaidizi kwa nchi masikini ni asilimia 3
  • Upatikanaji wa vifaa vya usaidizi kwa nchi tajiri ni asilimia 90
  • Iwapo vinapatikana hususan kwa watoto wenye ulemavu vinasaidia kubadili maisha yao na familia zao

Ripoti mpya iliyotolewa leo na mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la afya ulimwenguni WHO na la kuhudumia watoto UNICEF imefichua kuwa zaidi ya watu bilioni 2.5 wanahitaji kifaa kimoja au zaidi cha usaidizi, kama vile viti mwendo, vvifaa vya usaidizi wa  kusikia au programu zinazosaidia mawasiliano na utambuzi.

Wakati takwimu zinaonesha kuwa watu bilioni 2.5 wanauhitaji , takriban watu bilioni moja kati yao wanakosa fursa ya ufikiaji wa vifaa hivyo na wengi wao wanatoka katika nchi za kipato cha chini na cha kati.

Uchambuzi wa nchi 35 unaonesha pengo kubwa kati ya nchi tajiri na zinazoendelea ambapo wakati ufikiaji ukiwa asilimia 3 katika mataifa maskini na ya kipato cha kati, kwenye mataifa tajiri uwezekano wa wananchi kupata vifaa hivyo vya usaidizi ni asilimia 90.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo iliyopewa jina la Ripoti ya Kimataifa kuhusu Teknolojia ya Usaidizi jijini Geneva Uswisi amesema vifaa hivyo vya teknolojia ya usaidizi ni muhimu sana kwa kuwa vinabadili maisha na kufungua milango ya elimu kwa watoto wenye ulemavu, kusaidia watu kupata ajira na kuimarisha mwingiliano wa kijamii kwa watu wazima wanaoishi na ulemavu, na pia vinasaidia wazee kuwa na  maisha huru na ya utu.

Kote ulimwenguni takriban watu milioni 93 chini ya umri wa miaka 15 wanaishi na ulemavu.
© UNICEF/Vanda Kljajo
Kote ulimwenguni takriban watu milioni 93 chini ya umri wa miaka 15 wanaishi na ulemavu.

“Kuwanyima watu kupata zana hizi za kubadilisha maisha sio tu ni ukiukaji wa haki za binadamu, bali ni jambo la kutoona mbali kiuchumi. Tunatoa wito kwa nchi zote kufadhili na kuweka kipaumbele kwa upatikanaji wa teknolojia ya usaidizi na kutoa nafasi kwa  kila mtu kuishi kulingana na uwezo wake.” Amesema Dkt Tedros.

Kauli yake hiyo imeungwa mkono na mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Catherine Russell akiwa jijini New York ambaye ametaja takwimu zinazoonesha kuwa “Takriban watoto milioni 240 wana ulemavu. Kuwanyima watoto haki ya vifaa wanavohitaji ili kustawi hakudhuru mtoto mmoja mmoja tu, bali kunanyima familia na jamii zao kila kitu ambacho wangeweza kuchangia ikiwa mahitaji yao yangetimizwa.”

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNICEF Catherine amesisitiza bila ya kupata teknolojia saidizi, watoto wenye ulemavu wataendelea kukosa elimu, kuwa katika hatari kubwa ya kutumikishwa na kuendelea kunyanyapaliwa na kubaguliwa, hivyo kudhoofisha imani na ustawi wao.

Waichana walio na ulemavu wakicheza mpira wa vikapu nchini DRC.
© UNOCHA/Maxime Nama
Waichana walio na ulemavu wakicheza mpira wa vikapu nchini DRC.

Mapendekezo 10 yaliyotolewa katika ripoti 

Ripoti imetanabaisha kwamba kadri idadi ya watu inavyoendelea kuongezeka duniani na watu wenye uhitaji wa vifaa vya usaidizi huenda ukaongezeka hadi kufikia watu bilioni 3.5 ifikapo mwaka 2050.

Serikali zimeshauriwa kuhakikisha wenye uhitaji wanafikiwa na vifaa hivyo na mapendekezo 10 madhubuti ya kuweza kufikia hatua hiyo ni

1. Kuboresha ufikiaji wa ndani wa  mifumo ya elimu, afya na huduma za kijamii

2. Hakikisha kuna upatikanaji, usalama, ufanisi na uwezo wa kumudu wa vifaa vya usaidizi

3. Kuongeza, kupanua na kuboresha uwezo wa wafanyakazi

4. Kuwashirikisha kikamilifu watumiaji wa teknolojia za usaidizi na familia zao

5. Kuongeza ufahamu wa umma na kupambana na unyanyapaa

6. Kuwekeza katika takwimu na sera zinazozingatia kuwepo kwa ushahidi

7. Kuwekeza katika utafiti, uvumbuzi, na mifumo ikolojia wezeshi

8. Kuendeleza na kuwekeza katika mazingira wezeshi

9. kujumuisha teknolojia ya usaidizi katika utatuzi wa masuala mengine ya uhitaji wa kibinadamu

10.Kutoa usaidizi wa kiufundi na kiuchumi kupitia ushirikiano wa kimataifa ili kusaidia juhudi za kitaifa.

Kusoma kwa undani ripoti hiyo bofya hapa .