Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres alaani mauaji ya itikadi kali ya kibaguzi kwenye duka kubwa mjini Buffalo nchini Marekani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres akizungumza na wanahabari jijini New York, Marekani
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na wanahabari jijini New York, Marekani

Guterres alaani mauaji ya itikadi kali ya kibaguzi kwenye duka kubwa mjini Buffalo nchini Marekani.

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres Jumapili ametoa wito wa kujitolea zaidi ili kuhakikisha maelewano na utangamano katika jamii siku moja baada ya watu 10 kuuawa, na watatu kujeruhiwa, katika shambulio la ubaguzi wa rangi kwenye duka kubwa huko Buffalo, New York. 

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Guterres amesema mshukiwa, wa shambulio hilo Payton S. Gendron mwenye umri wa miaka 18 ambaye ni mzungu, alirekodi  moja kwa moja shambulio hilo, ambalo lilitekelezwa katika duka kubwa la Tops katika eneo ambalo lina  watu weusi wengi katika jiji hilo, lililoko kaskazini mashariki mwa Marekani. 

Waathirika wengi katika shambulio hilo walikuwa ni Wamarekani wenye asili ya Afrika. 

Shambulio hilo limelaaniwa vikali 

Bwana Guterres amesema kupitia taarifa yake iliyosomwa na naibu msemaji wa umoja wa Mataifa Farhan Haq kwamba ameshangazwa na kitendo hiki kiovu cha itikadi kali za kibaguzi.  

“Katibu Mkuu analaani vikali ubaguzi wa rangi katika aina zote na ubaguzi mwingine ukiwemo wa dini, imani au asili ya kitaifa. Ni lazima sote tushirikiane katika kujenga jamii zenye amani na umoja”. 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia na wapendwa wa waathirika na anatumai kuwa haki itapatikana haraka. 

Mshambuliaji huyo alikamatwa kufuatia mzozo na polisi. 

Tukio hilo ni ishara ya mauaji mabaya zaidi ya watu wengi kufyatuliwa risasi nchini Marekani kwa mwaka huu. 

Nas mauaji hayo  yanafuatia mauaji mengine ya hivi karibuni ya kibaguzi, ikiwa ni pamoja na mauaji ya Juni 2015 ya Waamerika tisa katika kanisa huko Charleston, South Carolina, na shambulio la Oktoba 2018 kwenye Sinagogi la Tree of Life huko Pittsburgh, Pennsylvania, ambapo watu 11 waliuawa na sita kujeruhiwa. .