Umoja wa Mataifa wakaribisha kukamilika kwa uchaguzi wa rais wa Somalia
Umoja wa Mataifa wakaribisha kukamilika kwa uchaguzi wa rais wa Somalia
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha kukamilika kwa uchaguzi wa amani wa rais nchini Somalia tarehe 15 Mei 2022.
Pia Bwana Guterres amempongeza Bwana Hassan Sheikh Mohamud kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la 10 la Somalia.
“Anampongeza Rais anayemaliza muda wake Mohamed Abdullahi Mohamed “Farmaajo” kwa kukubali mara moja matokeo na kumuunga mkono mrithi wake.” Imeeleza taarifa iliyotolewa hii leo na Stephane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu UN.
Aidha taarifa imeeleza kuwa Katibu Mkuu anaeleza matumaini yake kwamba Rais mpya atafanya haraka kuunda Baraza la Mawaziri shirikishi, na kwamba Serikali mpya na nchi wanachama wa shirikisho zitashirikiana kwa karibu ili kuendeleza vipaumbele muhimu vya kitaifa na kushughulikia changamoto zinazokabili Somalia.
Katibu Mkuu ameendelea kusisitiza kuhusu Umoja wa Mataifa kuendelea kuunga mkno Serikali na watu wa Somalia na anatazamia kuendelea kufanya kazi kwa karibu na utawala mpya ili kuendeleza ajenda ya ujenzi wa serikali ya Somalia na kushughulikia hali mbaya ya kibinadamu nchini humo.
Kwa upande wake Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, James Swan, mapema leo Jumatatu asubuhi amepongeza kukamilika kwa uchaguzi wa Somalia akisema, "ningependa kumpongeza Rais mpya mteule Hassan Sheikh Mohamud kwa ushindi wake usiku wa leo, lakini pia kutoa shukrani zetu kwa wagombea wengine, na hasa Rais anayemaliza muda wake Mohammed Abdullahi Mohamed 'Farmaajo,' kwa kuheshimu matokeo na kuendeleza mila ya Wasomali ya kukumbatia yeyote atakayeshinda na kuwaunga mkono kwenda mbele. Anga usiku wa leo, nadhani, lilikuwa nzuri sana,"
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini UNSOM alikuwa akizungumza wakati wa kuhitimisha uchaguzi huo, katika ukumbi mjini Mogadishu unaojulikana kama "hangar," ulioko karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden Adde, ambapo yeye na wawakilishi wengine wa washirika wa kimataifa wa Somalia walikuwa wamealikwa.
Rais Hassan Sheikh Mohamud ameshinda wadhifa wake huo katika duru ya tatu ya upigaji kura wa wabunge wa nchi hiyo, baada ya saa kumi na mbili za kupiga na kuhesabu kura. Kulikuwa na takriban wagombea 40 waliogombea kwenye ofisi hiyo.
Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa ameashiria kuwa mchakato wa uchaguzi umekuwa mrefu, na vilevile ulikuwa na ushindani mkubwa na kwamba kuzingatia vipaumbele vya ndani na vya serikali kunapaswa kuwa jambo kuu.
“Kumekuwa na nyakati ngumu katika uchaguzi huu mrefu. Hata hivyo, ninaamini kwamba mchakato wa usiku wa leo umeonesha kwamba zilikuwa mbio za kweli za farasi, kwamba ulikuwa uchaguzi wenye ushindani, na kwamba kulikuwa na fursa kwa wagombea wote kugombea kwa haki, na kwa hivyo nadhani hii ni fursa sasa kudhihirisha kuwa matokeo ni ya kuaminika.” Amesema Bwana Swan.
Aidha Bwana Swan ameongeza kusema kuwa sasa ni wakati wa Wasomali na marafiki wa Somalia kuja pamoja ili kuunga mkono serikali mpya inapowekwa, na kufanyia kazi vipaumbele muhimu vya kitaifa ambavyo bado vinaikabili Somalia na akasema, "kuna kazi nyingi za kufanywa, na tunatazamia kuwa washirika wa Somalia kwenda mbele."
Bwana Swan pia amebainisha kuwa baadhi ya vipaumbele muhimu vya nchi ni pamoja na kumaliza mchakato wa marekebisho ya katiba, kushughulikia mahitaji ya dharura ya kuboreshwa kwa maendeleo, usalama na ukame uliopo.
Baadaye katika ujumbe wa Twitter, Umoja wa Mataifa nchini Somalia pia umewasifu Maspika na Manaibu Spika wa Bunge la Somalia, kamati ya maandalizi ya uchaguzi wa rais na wafanyakazi wenye weledi wa bunge, pamoja na vikosi vya usalama vya Somalia na Ujumbe wa Mpito wa Muungano wa Afrika nchini Somalia (ATMIS), kwa kuhakikisha Uchaguzi wa rais wa Jumapili wenye utaratibu, amani na usalama, ambao matokeo yake yamekubaliwa kikamilifu.