Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma salamu za heri kwa mamilioni ya waumini wa madhehebu ya Budha duniani wanaoadhimisha siku ya Vesak hii leo.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kutoka New York Marekani , Guterres amesema “Kwa mamilioni ya Wabudha ulimwenguni kote, mwezi Mei ambapo usiku mwezi wote ukiwa umetoka na kuonekana kamili unawakilisha hafla takatifu ya kuheshimu kuzaliwa, kutaalamika na kufariki dunia kwa Bwana Buddha.”
Ameeleza kwamba mwaka huu, sherehe ya Vesak inafika wakati ambapo kuna migogoro inayoibuka kila uchao huku dunia ikishuhudia ahueni isiyo na usawa kuanzia kwenye janga la Corona au COVID-19, athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi, hadi mizozo, migawanyiko na vurugu.
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amehitimisha ujumbe wake kwa kueleza kuwa “Kila shida inatukumbusha jinsi tulivyojitenga na mafundisho ya Bwana Buddha. Vesak hii, hebu tuchukue wakati huu wa upyaji wa kiroho, na tuheshimu hekima ya Buddha kwa kukusanyika pamoja kama kitu kimoja, kwa mshikamano, na kuunda ulimwengu bora, wenye amani zaidi kwa watu wote.”