Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fifisha mwanga wa taa usiku ili kuokoa maisha ya ndege wanaohama duniani:UN 

Njia za ndege kuhama zinawapitisha katika miji mingi kote ulimwenguni
© Unsplash/Karen Hammega
Njia za ndege kuhama zinawapitisha katika miji mingi kote ulimwenguni

Fifisha mwanga wa taa usiku ili kuokoa maisha ya ndege wanaohama duniani:UN 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katika siku ya ndege wanaohama duniani Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuchukua hatua kufifisha nuru ya mwanga usiku ili kunusuru maisha ya mamilioni ya Ndege kila mwaka. 

Maudhui ya mwaka huu ya siku hiyo ni “Uchafuzi wa nuru ya mwanga unatishia ndege ulimwenguni kote lakini suluhu zinapatikana kwa urahisi”. 

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa uchafuzi wa mwanga na athari zake kwa ndege wanaohama ni kampeni ya kimataifa ambayo inalenga kuongeza ufahamu wa ndege wanaohama na haja ya ushirikiano wa kimataifa ili kuwahifadhi. Shughuli za kuadhimisha siku hiyo zitafanyika duniani kote chini ya mada "Fifisha taa kwa ajili ya ndege usiku". 

Umoja wa Mataifa unasema uchafuzi wa mwanga unaongezeka kote ulimwenguni ambapo zaidi ya asilimia 80 ya idadi ya watu duniani kwa sasa wanakadiriwa kuishi chini ya anga yenye mwanga, na katika idadi hiyo karibu asilimia 99 wako Ulaya na Amerika Kaskazini.  

Taarifa imeongeza kuwa kiasi cha mwanga bandia kwenye uso wa dunia kinaongezeka kwa angalau asilimia 2 kila mwaka na kinaweza kuwa kikubwa zaidi ya hapo. 

Siku ya ndege wanaohama.
UNEP_AEWA
Siku ya ndege wanaohama.

Kufifisha mwanga kuna faida kubwa 

Amy Fraenkel, katibu mtendaji wa mkataba wa aina zinazohama za ndege na wanyama wa porini (CMS) amesema “Giza la asili lina thamani ya uhifadhi kwa njia sawa na maji safi, hewa, na udongo. Lengo kuu la siku ya ndege wanaohama duniani 2022 ni kuongeza ufahamu wa suala la uchafuzi wa mwanga na athari zake mbaya kwa ndege wanaohama. Suluhu zinapatikana kwa urahisi, na tunatumai kuwahimiza watoa maamuzi wakuu kuchukua hatua za kushughulikia uchafuzi wa mwanga.” 

 Ameongeza kuwa uchafuzi wa mwanga ni tishio kubwa na linaloongezeka kwa wanyamapori ikiwa ni pamoja na aina nyingi za ndege wanaohama.  

“Kila mwaka, uchafuzi wa mwanga huchangia vifo vya mamilioni ya ndege. Unabadilisha mifumo ya asili ya mwanga na giza katika mfumo wa ikolojia. Unaweza kubadilisha mifumo ya uhamiaji ya ndege, tabia ya kutafuta chakula, na mawasiliano ya sauti. Wanavutiwa na mwanga wa bandia usiku, hasa kunapokuwa na mawingu, ukungu, mvua au wakati wa kuruka kwenye miinuko ya chini, ndege wanaohama huchanganyikiwa na wanaweza kuishia kuzunguka katika maeneo yenye mwanga. Akiba ya nishati iliyopunguzwa inawaweka katika hatari ya kuchoka, kushambuliwa na kugongana na majengo ambapo wengi hufa.” Amesisitiza 

Naye Jacques Trouvilliez, katibu mtendaji wa Afrika-Eurasian (AEWA) wa mkataba wa ndege wa majini amesema: "Ndege wengi wa aina mbalimbali, wanaofanya kazi usiku, wanapitia madhara ya uchafuzi wa mwanga. Ndege wengi wanaohama usiku kama vile bata, bata bukini, plovers, sandpipers na ndege waimbao huathiriwa na uchafuzi utokanao na mwanga unaowasababisha kuchanganyikiwa na migongano yenye matokeo mabaya. Ndege wa baharini kama vile petrels na shearwater huvutiwa na taa bandia kwenye nchi kavu na kuwa mawindo ya panya na paka.” 

Suluhisho na mapendekezo ya kupunguza uchafuzi wa mwanga 

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa miongozo kuhusu uchafuzi wa mwanga unaofunika kasa wa baharini, ndege wa baharini na ndege wanaohamahama iliidhinishwa na vyama vya CMS mwaka 2020. Miongoni mwa mapendekezo yao, ni kwamba miongozo hiyo imeweka kanuni sita za utendakazi bora wa mwanga na kutaka ifanyike tathmini ya athari za mwanga kwa mazingira na kwa miradi husika ambayo inaweza kusababisha uchafuzi wa mwanga. 

Haya yanapaswa kuzingatia vyanzo vikuu vya uchafuzi wa mwanga kwenye maeneo fulani, aina za ndege wa porini ambao wanaweza kuathiriwa, na ukweli kuhusu ukaribu wa makazi muhimu na njia zinazotumika na ngege wahamao. 

Miongozo mipya inayolenga ndege wa ardhini na popo wanaohama kwa sasa inaandaliwa chini ya CMS.  

Itawasilishwa kwa wanachama wa CMS ili kupitishwa katika Mkutano wa 14 wa wanachama wa CMS mwaka 2023. 

Hatua zimeanza kuchukuliwa  

Serikali nyingi, miji, makampuni, na jumuiya kote ulimwenguni tayari zinachukua hatua kukabiliana na uchafuzi wa mwanga. 

Mathalani Umoja wa Mataifa unasema katika baadhi ya miji, hasa Amerika Kaskazini, mipango kama vile programu za kampeni kama "Zima Taa" na miongozo ya ujenzi inayofaa kwa ndege wanaohama inalenga kulinda ndege wanaohama kutokana na uchafuzi wa mwanga kwa kuwahimiza wamiliki wa majengo na wasimamizi kuzima mwanga wowote usio wa lazima wakati wa ndege kuhama. 

Susan Bonfield, mkurugenzi, mazingira Marekani amesema "Siku ya ndege wanaohama duniani ni wito wa kuchukua hatua kwa uhifadhi wa kimataifa wa ndege wanaohama. Huku safari ya ndege wanaohama wakivuka mipaka, kuwatia moyo na kuwaunganisha watu njiani, ni lengo letu kutumia siku hizi mbili mwaka 2022 kuhamasisha juu ya tishio la uchafuzi wa mwanga na umuhimu wa anga yenye giza kwa uhamaji wa ndege."