Uhamasishaji wa nyumba kwa nyumba DRC wachochea watu kupata chanjo ya COVID-19
Uhamasishaji wa nyumba kwa nyumba DRC wachochea watu kupata chanjo ya COVID-19
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC linatumia wafanyakazi wa kijamii kuhamasisha wakazi wa vitongoji vya mji mkuu, Kinshasa kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona, au COVID-19 kwa kuwa baadhi ya watu bado wanasuasua kupatiwa chanjo hiyo.
Brigitte Kevani, muhudumu wa kijamii jijini Kinshasa, huambana na wahudumu wengine kutembelea eneo lake la N’sele kuhamasisha wanajamii wapatiwe chanjo ya coronavirus">COVID-19.
Hupita nyumba kwa nyumba na kuhamasisha umuhimu na faida ya chanjo kwa mtu binafsi na kwa jamii yake.
Miongoni mwa waliotembelewa na Bi. Kevani, ni Bwana Jean Mulumba aambaye katika ziara ya leo anasikiliza kwa makini kwa nini ni muhimu apatiwe chanjo tena dozi zote mbili, na kisha wanaondoka pamoja hadi kituo cha afya ambako naye anapatiwa chanjo.
Bi. Kevani anasema yeye mwenyewe alipatiwa chanjo kama njia ya kujilinda na kujengea imani wengine ili wachanjwe na zaidi ya yote “nafurahi kwa sababu hata kama mtu amehamasika lakini haendi kuchanja, utaona siku tatu baadaye anakwenda, hili ni jambo zuri. Kama Mulumba tulimhamasisha na akashawishika kwa sababu watu wameanza kuelewa ikilinganishwa na awali. Kwa sasa mambo yanakuwa mazuri.”
Kwa upande wake Bwana Mulumba naye anasema, “kwa ugonjwa wa surua tuliona tofauti kati ya mtoto aliyepata chanjo na ambaye hakupata, kwa ugonjwa ukilipuka unaona mwenye chanjo anakuwa imara lakini ambaye hana chanjo anaugua na anakuwa dhaifu na anaweza kufa siku inayofuata. Hebu tupate chanjo kwa sababu kama sote tutachanjwa, basi ugonjwa hautafanya chochote.”
TAGS: UNICEF, DRC, COVID-19, Afya