Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake na wasichana wakumbwa na ukatili wa kingono Ukraine

Mwanamume akitembea katika jengo lililoharibiwa Kharkiv, Ukraine.
© UNICEF/Ashley Gilbertson
Mwanamume akitembea katika jengo lililoharibiwa Kharkiv, Ukraine.

Wanawake na wasichana wakumbwa na ukatili wa kingono Ukraine

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu Michelle Bachelet amesema ofisi yake imethibitisha matukio ya ukatili wa kingono dhidi ya wanawake nchini Ukraine, ambako mapigano yanaendelea tangu uvamizi uliofanywa na Urusi kuanzia tarehe 24 mwezi Februari mwaka huu.

Akihutubia Baraza la Haki za Binadamu kwa njia ya video kutoka Vienna, Austria hii leo, Bi. Bachelet amesema wamethibitisha makumi kadhaa ya matukio ya ukatili wa kingono kwenye maeneo ya mkoa wa Kyiv ambayo awali  yalikuwa chini ya majeshi ya Urusi. 

“Kulikuweko na matukio ya ubakaji na mauaji ya waliobakwa au jamaa zao. Manusura mara nyingi hawako tayari kuzungumza kwa hofu ya usalama wao na unyanyapaa. Wanawake na wasichana ndio waathirika wakuu,” amesema Bachelet huku akiongeza kuwa ripoti za wanaume na wavulana kuwa miongoni mwa waathirika nazo zinaanza kuibuka. 

Ukatili dhidi ya wanaume na wavulana 

Bi. Bachelet amesema uchunguzi pia umebaini kuwa majeshi ya Urusi na washirika wao wanakamata raia, hususan wanaume na wavulana na kuwahamishia nchini Belarus na Urusi ambako wanashikiliwa kwenye vituo bila mashtaka yoyote. 

“Tangu tarehe 24 mwezi Februari tumerekodi matukio 204 ya watu kutoweshwa wakiwemo wanaume 169, wanawake 34 na mvulana 1,” amesema Mkuu huyo wa Ofisi ya Haki za Binadamu akiongeza kuwa 38 kati yao hao wameachiliwa huru na kurejea nyumbani, huku watu 5 wakiwemo wanaume 4 na mwanamke mmoja wamekutwa wamekufa. 

“Idadi ya wanaotoweshwa inaweza kuwa kubwa,” amesema Bachelet. 

Hata katika maeneo ambako yanamilikiwa na serikali ya Ukraine, nako kuna ripoti za watu kutoweshwa, hususan watu wanaounga mkono Urusi. 

“Matukio hayo yanaonekana kutekelezwa na maafisa wa serikali ya Ukraine,” amesema Kamishna Mkuu huyo. 

Matukio mengine ya ukiukwaji wa haki 

Kamishna Mkuu huyo akimulika matukio mengine amesema kimsingi, “mwelekeo wa sababu za vifo na majeruhi miongoni mwa raia bado hazijabadilika sana. Matukio mengine yanaendelea kusababishwa na matumizi ya silaha za vilipuzi kwenye maeneo ya raia, kama vile makombora na maroketi.” 

 Amesema kwa mujibu wa taarifa walizo nazo, matukio mengine yanaweza kuhusishwa na pande zote kwenye mzozo unaoendelea, lakini kwa kiasi kikubwa wahusika ni majeshi ya Urusi na washirika wao. 

Hadi leo hii maiti zaidi ya 1,000 wamepatikana kwenye mkoa wa Kyiv peke yake. “Baadhi wameuawa kwenye mapigano na wengine yaonekana walipigwa tu risasi na kuuawa. Wengine wamekufa kwa kihoro kutokana na magonjwa na ukosefu wa matibabu,” amesema Bi. Bachelet. 

Amesimulia kisa cha wakazi 360 katika Kijiji cha Yahidne mkoa wa Chernihiv ambao walilundikana kwenye handaki la nyumba kwa siku 28 na hawakuweza hata kulala bali kusimama wima. 

“Hawakuwa na huduma za choo, maji wala hewa. Wazee 10 walikufa,” amesema Bi. Bachelet. 

Jawabu mujarabu 

“Njia pekee ni kwa vita hii kukoma, na hili liwe lengo letu la msingi,” amesema Bachelet akiongeza kuwa majeshi kwenye vita hiyo waeleze bayana kwa watendaji wao kuwa yeyote atakayekiuka kanuni za kimataifa na kushambulia raia lazima awajibishwe. 

OCHA yalaani mashambulizi ya hivi karibuni Ukraine 

 Nalo Baraza la Usalama hii leo limekuwa na mjadala kuhusu amani na usalama likijikita na Ukraine ambapo Msaidizi wa Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa kuhusu misaada ya dharura, Joyce Msuya amelaani mashambulizi ya hivi karibuni nchini Ukraine, ambayo amesema yanazidisha machungu hasa mikoa ya Kusini na Mashariki mwa nchi hiyo. 

Hali ni mbaya sana na inatia hotu kwenye mkoa wa Luhanska ambako takribani watu 40,000 hawana huduma ya umeme, maji na gesi sambamba na huduma ya usafiri. Eneo hilo linadhibitiwa na serikali ya Ukraine na miundombinu imeharibiwa. 

“Wafanyakazi wenzetu wa huduma za kibinadamu wanaripoti kuweko kwa mashambulizi makali ya makombora katika siku za karibuni,” amesema Bi. Msuya ambaye pia ni Naibu Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA

Huko Odesa, Kusini mwa Ukraine, mashambulizi kadhaa ya makombora kutoka angani yamesababisha uharibifu mkubwa wa makazi, uwanja wa ndege, na miundombinu mingine muhimu ya raia. 

“Raia kadhaa wameripotiwa kuuawa, lakini bado hatujaweza kuthibitisha takwimu,” amesema. 

UN inasaka mbinu zote 

Amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa umejizatiti kusaka mbinu zote ili kufikia watu wengi wenye uhitaji. 

 “Nasihi pande zote kwenye mzozo kuondoa vikwazo vyote dhidi ya wafanyakazi wa kibinadamu ili waendelee kusambaza misaada ya kibinadamu katika maeneo yote ya Ukraine,” amesema Bi. Msuya, akisisitiza kuwa raia ndio wanalipa gharama kubwa ya mzozo unaoendelea. 

Amesema pande kwenye mzozo zina wajibu wa kuzingatia sheria za kibinadamu za kimataifa ili kulinda raia, makazi, hospitali, shule na miundombinu mingine muhimu.