Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Wafanyikazi wanafanya kazi kwenye shughuli ya uzalishaji katika kiwanda cha kusindika nafaka huko Skvyra, Ukraine mnamo 2017.

Vita Ukraine vyapukutisha mamilioni ya ajira: ILO

© FAO/Genya Savilov
Wafanyikazi wanafanya kazi kwenye shughuli ya uzalishaji katika kiwanda cha kusindika nafaka huko Skvyra, Ukraine mnamo 2017.

Vita Ukraine vyapukutisha mamilioni ya ajira: ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Takribani ajira milioni 4.8 nchini Ukraine zimetokomea kufuatia uvamizi wa Urusi dhidi ya taifa hilo, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani ILO katika ripoti yake iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi. 

Ripoti hiyo ikipatiwa jina. Athari za janga la Ukraine katika ajira; Tathmini ya awali, inakadiria kuwa iwapo vita itaendelea, idadi ya ajira zitakazopotea inaweza kufikia milioni 7, na iwapo itakoma basi hali itakuwa shwari na ajira milioni 3.4 zitarejea. 
“Hii itapunguza kutoweka kwa ajira kwa asilimia 8.9.” inasema ripoti hiyo. 

Hali halisi 

Uchumi wa Ukraine  umeathirika kutokana na uvamizi wa Urusi ulioanza tarehe 24 mwezi Februari mwaka huu ambapo zaidi ya raia milioni 5.2 wamekimbilia nchi Jirani. 

Wakimbizi hao wengi wao ni wanawake na watoto na wazee wenye umri wa zaidi yamiaka 60. 

Miongoni mwa hao waliokimbilia nchi Jirani, milioni 2.75 wana umri wa kufanya kazi ambapo asilimia 43.5 kati yao walikuwa na ajira na hivyo wamepoteza kazi zao. 

Serikali ya Ukraine imefanya nini? 

Katika kuchukua hatua, serikali ya Ukraine imefanya juhudi za msingi ikiwemo kuendeleza mfumo wake wa hifadhi ya jamii ili hata wale waliolazimika kuacha kazi waendelee kupata mafao yao, wakiwemo wakimbizi  wa ndani. 
 
Huduma hiyo ya kuendelea kuwapatia mafao inafanyika kwa kutumia teknolojia za kidijitali. 

Vita ya Ukraine yaleta janga la ajira kikanda 

ILO inasema janga la vita ya Ukraine linaweza kuvuruga ajira katika nchi Jirani kama vile Hungary, Moldova, Poland, Romania na Slovakia.  
“Iwapo vita itaendelea, wakimbizi wa Ukraine watakalazimika kuishi ugenini kwa muda mrefu, na kuweka shinikizo kwenye soko la ajira na mifumo ya hifadhi ya jamii ya nchi Jirani sambamba na wengi kukosa ajira,” imesema ILO. 

Wanaume wanafanya kazi ya ujenzi kwenye kiwanda cha kusindika nafaka huko Skvyra, Ukrainia. (maktaba)
© FAO/Genya Savilov
Wanaume wanafanya kazi ya ujenzi kwenye kiwanda cha kusindika nafaka huko Skvyra, Ukrainia. (maktaba)

ILO imefanya nini? 

Pamoja na mwezi Machi ILO kupitisha azimio lake la kutaka Urusi ikomeshe mara moja na bila masharti yoyote uvamizi wake Ukraine, shirika hilo pia limependekeza hatua kadhaa za kuchukua. 
 
Mosi, kufanikisha mipango ya waajiri na vyama vya wafanyakazi ili waweze kutoa misaada ya kibinadamu na kuhakikisha ajira inaendelea pale inapowezekana. 
 
Pili kwenye maeneo ambako ni salama kuweka mazingira ambamo kwayo kazi zitaweza kuendelea kufanyika, mathalani kuweka programu za kuhamishia wafanyakazi kwenye maeneo salama. 
 
Tatu kusaidia mfumo wa hifadhi ya jamii Ukraine ili uendelee kulipa mafao kwa waajiriwa hata kama wamepoteza ajira zao. 
Na nne, ni kuandaa mkakati wa kujikwamua baada ya vita kuisha na kuhamasisha kuweka ajira zenye utu na tija.