Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Wanafunzi wakiwa darasani wilaya ya Kasese nchini Uganda.

Programu ya UNICEF Uganda yamuepusha mtoto ‘Sarah’ kujiua

© UNICEF/Maria Wamala
Wanafunzi wakiwa darasani wilaya ya Kasese nchini Uganda.

Programu ya UNICEF Uganda yamuepusha mtoto ‘Sarah’ kujiua

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini Uganda linaendesha programu ya waelimishaji rika ambayo imesaidia watoto kadhaa wa kike akiwemo Sara kuacha kujiua baada ya kubakwa na kupewa ujauzito na hatimaye kurejea shuleni kusoma huku akilea mtoto wake na kuwa na matarajio makubwa kwa siku za usoni

"Niliporejea nyumbani wakati wa likizo mwezi Mei, ndipo aliniambia kwa baba yake amefariki Dunia, basi nikaenda nyumbani kwake kumpa pole!" ni maneno ya Sarah (si jina lake halisi), msichana mwenye umri wa miaka 16 mkazi wa Arua nchini Uganda, ambaye alilaghaiwa na kijana rafiki wa kaka yake, akambaka na kumpatia ujauzito. 
 
Sara katika video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, huku sura yake imefichwa anasema alipofika kwa kijana huyo hakukuweko mtu yeyote bali yeye peke yake na akafanya alichofanya. 
 
Alitambua kuwa amepata ujauzito baada ya kukosa hedhi kwa miezi mitatu mfululizo. “Alinitishia na nikahofia kumjulisha mtu yeyote. Ndio  maana nikaamua kukimbia nyumbani, na nilihisi kuwa nimemuumiza mama yangu.” 
 
Baadaye baba mzazi wa Sarah alikubali kuwa bora wayamalize. “Wahusika waje nyumbani na alitaka walimpe mahari ya shilingi milioni 10  sawa na dola zaidi ya 2,700, na wanichukue kwa kuwa hanitaki tena. Mambo yalikuwa magumu sana. Na huku kijana alinikataa akisema hakusiki. Niliona kwamba moyo wangu hauwezi kuvumilia tena.” 
 
Anicy Alezuyo ambaye ni mshauri rika chini ya programu ya UNICEF anasema, “alitaka kutoka ujauzito kwa kuwa kuna rafiki alimwambia anaweza kumsaidia kupata fedha za kutoa ujauzito. Lakini fedha hazikupatikana. Ndipo akaja kwangu.” 
 
Kijana aliyempa ujauzito naye alimshauri atoe ujauzito lakini alikataa, halikadhalika baba yake mzazi alitaka atoe lakini Anicy alimshauri kuwa asitoe na hatimaye alijifungua na wiki mbili baada ya operesheni amerejea shuleni na analea pia mtoto wake.  
 
Sasa Sarah ana ndoto, “nataka mtoto wangu akue kwenye upendo na si machungu kama mimi. Nataka nisome hadi Chuo Kikuu bora ili nifikie ndoto  yangu ya kuwa daktari.” 
 
Kwa mujibu wa UNICEF, Anicy pamoja na waelimishaji rika wengine 20 wilayani Arua nchini Uganda wanatembelea shule kuelimisha vijana balehe kuhusu afya ya uzazi, fursa za maisha na kusalia shuleni.