Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Chanjo kwa jamii zinazohifadhi wakimbizi Uganda.

Ingawa hatua zimepigwa Afrika kukabili COVID-19, lakini bado kuna changamoto:UNITAID

© UNICEF/Maria Wamala
Chanjo kwa jamii zinazohifadhi wakimbizi Uganda.

Ingawa hatua zimepigwa Afrika kukabili COVID-19, lakini bado kuna changamoto:UNITAID

Afya

Bara la afrika limepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya janga la COVID-19, idadi ya wagonjwa na vifo inapungua lakini bado kuna changamoto kubwa kuhusu janga hilo limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kufanikisha upatikanaji wa dawa na tiba kwa gharama nafuu UNITAID ambalo linajikita katika kutafuta suluhu za kibunifu za kuzuia, kutambua na kutibu magonjwa kwa haraka zaidi katika nchi za kipato cha kati na cha chini.

Akizungumza kutoka Nairobi Kenya msemaji wa UNITAID Herve Verhoosel ambaye yuko ziarani nchini humo amesema kesho Mei 12 viongozi wa dunia wanakutana kutafakari hatua muhimu za kimataifa zinazofuata katika kukabiliana na janga hilo kwenye mkutano wa pili wa kimataifa wa COVID-19.

Kwa mujibu wa UNITAID kuna pengo kubwa baina ya nchi za kipato cha ju una za kipato cha chini. Kwa mantiki hiyo Verhoosel amesema “Ni muhimu sana kwa jumuiya ya kimataifa kuzingatia ahadi zake kwa nchi za kipato cha chini na cha kati katika vita dhidi ya COVID-19. Sio tu chanjo ambazo leo zinapatikana lakini pia uwekezaji wa ziada unahitajika kwa ajili ya dawa na upimaji. Tunahitaji kuweza kuwapima na kuwatibu wagonjwa walio hatarini ambaopo wameambukizwa. Kwa mfano leo hii katika nchi za kipato cha chini na cha Kati kuna vipimo viwili tu kati ya wakazi 10,000 kwa siku hii ni mara 50 pungufu ya nchi za kipato cha juu ambako kwa siku kunafanyika vipimo 100 kati ya wakazi 100,000. Hivyo shirika la afya la UNITAID linatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuwekeza zaidi katika nchi za kipato cha chini na cha kati  hususan hapa Afrika.”

Ameongeza kuwa mbali ya COVID-19 fursa ya kupata matibabu ya kuokoa maisha ikiwemo dawa za kupunguza makali ya ukimwi ni ndogo , wakati nchi nyingi bado zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa Oksijeni.

Mfanyakazi wa afya akiwa katika Maaabara ya kupima COVID-19 katika hospitali ya Mlipo nchini Zimbabwe
© ILO/KB Mpofu
Mfanyakazi wa afya akiwa katika Maaabara ya kupima COVID-19 katika hospitali ya Mlipo nchini Zimbabwe

Makadirio ya sasa yanaonesha kuwa karibu wagonjwa milioni 1 wa COVID-19 kwa siku wanahitaji mitungi 500,000 ya hewa ya Oksijeni.

UNITAID inata wito kwa sekta ya madawa kuhakikisha upatikanaji mkubwa wa matibabu haya katika nchi za kipato cha chini na cha katiikiwemo kupitia leseni za hiyari.

Shirika hilo limeongeza kuwa mkutano wa wiki hii ni fursa ya kuimarisha ahadi za jumuiya ya kimataifa ya kusaidia vita dhidi ya COVID-19 katika nchi za kipato cha chini na cha kati hususan barani Afrika.