Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukikutana na wakimbizi ni vigumu kutoguswa na simulizi zao- Guterres akiwa Moldova

Wakimbizi kutoka Ukraine (sura zao zimefichwa kwa ajili ya kuficha utambulisho wao) wamepata hifadhi huko Moldova
UN /Mark Garten
Wakimbizi kutoka Ukraine (sura zao zimefichwa kwa ajili ya kuficha utambulisho wao) wamepata hifadhi huko Moldova

Ukikutana na wakimbizi ni vigumu kutoguswa na simulizi zao- Guterres akiwa Moldova

Amani na Usalama

Ni vigumu kukutana na wakimbizi halafu usiguswe na simulizi zao! Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyotoa leo huko Chişinau, mji mkuu wa Moldova wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea kituo cha kuhifadhi wakimbizi kutoka Ukraine, kituo kilichoko mjini humo.

Guterres amesema “watu wamekimbia makombora yaliyokuwa ‘yanamiminwa’ kwenye miji yao. Kuna mke na mume ambao wamenisimulia kuwa bomu lilianguka kwenye ua wa nyumba yao. Watu wametelekeza kila kitu, ikiwemo sehemu za familia zao.”

Aliposema ‘familia zao’ Guterres amefafanua kwa wanahabari kuwa wanatambua wanaume huko Ukraine hawakuruhusiwa kuondoka nchini mwao.

Katibu Mkuu amesema janga hili la Ukraine linadhihirisha kuwa vita haina maana yoyote na kwamba vita hii lazima ikome.

Vita si jawabu la changamoto zinazokabili dunia hivi sasa, ni lazima tukomeshe hii vita sasa. António Guterres- Katibu Mkuu wa UN

Vita si jawabu la changamoto

Katibu Mkuu amerejelea tena wito wake kuwa vita si jawabu la changamoto zinazokabili dunia hivi sasa, akisema « ni lazima tukomeshe hii vita saa tunahitaji kuona sheria ya kimataifa inazingatiwa. »

Hali halisi Ukraine hivi sasa

Katibu Mkuu akiwa nchi jirani ya Moldova, Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa ufuatiliaji wa haki za binadamu nchini Ukraine Matilda Bogner, amezungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi na kuelezea kinagaubaga kile alichoshuhudia wakati wa ziara yake kwenye miji 14 ya majimbo ya Kyiv na Chrnihiv, ambayo ilikaliwa na majeshi ya Urusi hadi mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu.

“Leo ni siku ya 76 tangu Urusu ishambulie Ukraine. Siku 76 zimeharibu maisha, na miji, shule, hospitali na nyumba. Watu wametusimilia jinsi ndugu zao, Jirani zao na marafiki zao wameuawa, wameshikiliwa na hata kutoweshwa,” amesema Bi. Bogner.

Huko Makariv, familia moja ya watu watano ilifyatuliwa risasi na majeshi ya Urusi wakati wakijaribu kuondoka ndani ya gari lao.

Mwanaume huyu na mkewe ni miongoni mwa raia wengi wa Moldova ambao wamepatia hifadhi wakimbizi kutoka Ukraine
UN /Mark Garten
Mwanaume huyu na mkewe ni miongoni mwa raia wengi wa Moldova ambao wamepatia hifadhi wakimbizi kutoka Ukraine

“Ni huzuni kubwa kwamba ni wawili tu kati ya hao watano ndio walinusurika,” amesema Mkuu huyo wa ujumbe wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine.

Idadi ya wakimbizi wa ndani Ukraine Yazidi kushamiri- IOM

Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM limesema idadi ya wakimbizi wa ndani nchini Ukraine kutoka na vita imevuka milioni 8.

Huko Makariv, familia moja ya watu watano ilifyatuliwa risasi na majeshi ya Urusi wakati wakijaribu kuondoka ndani ya gari lao - Matilda Bogner, Mkuu wa ujumbe wa UN wa ufuatiliaji wa Haki za Binadamu Ukraine

Taarifa ya IOM iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inasema idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 24 ikilinganishwa na takwimu za tarehe 16 mwezi Machi mwaka huu.

Takwimu za sasa zinatokana na utafiti uliofanyika kati ya tarehe 17 mwezi Aprili na tarehe 3 mwezi Mei mwaka huu, na kuonesha mahitaji yaliyoongezeka ya wakimbizi wa ndani.

Theluthi mbili za wale waliopitiwa na utatifi wamesema wanahitaji msaada wa fedha taslimu, ikilinganishwa na asilimia 49 wakati vita ilipoanza.

Zaidi ya asilimia 70 wamesema wanatumia msaada wa fedha taslimu kukidhi mahitaji ya chakula na matibabu.

Asanteni Moldova

Hali inavyozidi kuwa tete na mahitaij yakizidi Ukraine, Katibu Mkuu Guterres kwa mara nyingine tena ameeleza kuvutiwa kwake na ukarimu wa wananchi wa Moldova na serikali yao kwa kuwa asilimia 95 ya wakimbizi wakimbizi wako ndani ya nyumba zao.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (kushoto) akisalimiana na Maia Sandu, Rais wa Moldova kwenye mji mkuu, Chisnau
UN /Mark Garten
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (kushoto) akisalimiana na Maia Sandu, Rais wa Moldova kwenye mji mkuu, Chisnau

Moldova ni nchi ambayo si mwanachama wa Muungano wa Ulaya na pia inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi na ndio maana Katibu Mkuu anasisitiza usaidizi wa kimataifa ili kunusuru mafanikio ya taifa hilo ya kiuchumi na kijamii yasitwamishwe na vita vya Ukraine.

Mapema Guterres alikutana na Rais wa Moldova Mina Sandu na kuelezea shukrani zake kwa ukarimu na mshikamano mkubwa uliooneshwa na serikali yake kwa wale wanaokimbia vita Ukraine.