Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pombe inaua mtu mmoja kila baada ya sekunde 10 : WHO

Unywahi pombe nchini Russia umepungua kwa 43% kutoja mwaka 2003 mpaka 2016, kwa mujibu wa ripoti ya WHO
Unsplash/chuttersnap
Unywahi pombe nchini Russia umepungua kwa 43% kutoja mwaka 2003 mpaka 2016, kwa mujibu wa ripoti ya WHO

Pombe inaua mtu mmoja kila baada ya sekunde 10 : WHO

Afya

•    Ripoti ya WHO yafichua mbinu za ushawishi zinazotumiwa na kampuni za pombe
•    Mbinu hizo zinazidi udhibiti wa matangazo.
•    Watu mashuhuri mitandaoni watumika
•    Mbinu mpya zabuniwa kuwalenga wanawake

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la  Afya Ulimwenguni WHO imeeleza kuongezeka kwa matumizi ya mbinu za kisasa za uuzaji wa pombe mtandaoni na kwamba kunahitajika udhibiti mzuri zaidi wa serikali. 

Akizungumza kuhusu ripoti hiyo akiwa Geneva Uswisi Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema vijana na wanywaji pombe kupindukia wanazidi kulengwa na matangazo ya pombe, na hivyo mara nyingi kuhatarisha afya zao.

“Pombe huwanyang'anya vijana, familia zao na jamii maisha na uwezo wao. Hata hivyo licha ya hatari za wazi kwa afya, udhibiti wa uuzaji wa pombe ni dhaifu sana kuliko bidhaa zingine za uraibu. Udhibiti bora, unaotekelezwa vyema na thabiti zaidi wa uuzaji wa pombe ungeokoa na kuboresha maisha ya vijana kote ulimwenguni.”

Ripoti hiyo iliyopewa jina la “Kupunguza madhara yatokanayo na pombe - kwa kudhibiti uuzaji wa pombe kuvuka mipaka na  utangazaji” ni ripoti ya kwanza kutoka WHO kufafanua kiwango kamili cha jinsi pombe inavyouzwa kuvuka mipaka ya kitaifa  na mara nyingi kwa njia za kidijitali bila kujali mazingira ya kijamii, kiuchumi au kiutamaduni katika nchi zinazopokea.

Vifo milioni 3 kwa mwaka

Dkt. Tedros ametanabaisha kuwa ulimwenguni kote, watu milioni 3 hufa kila mwaka kutokana na matumizi mabaya ya pombe, hii ni sawa na mtu mmoja kila baada ya sekunde 10  akiwakilisha karibu asilimia 5 ya vifo vyote.

Idadi isiyo na uwiano ya vifo hivi vinavyohusiana na pombe hutokea miongoni mwa vijana, huku asilimia 13.5 ya vifo vyote ikiwa ni kati ya wale walio na umri wa miaka 20-39 wakihusishwa na pombe.

Mwanamke akiangalia vilevi katika duka
WHO/Sergey Volkov
Mwanamke akiangalia vilevi katika duka

Mapinduzi ya kidigitali na mbinu zinazotumika kusaka masoko 

Chanzo kimoja cha takwimu kilichonukuliwa katika ripoti hiyo kilikokotoa zaidi ya asilimia 70 ya matumizi ya vyombo vya habari ya wauzaji pombe maarufu nchini Marekani kwa mwaka 2019 yalikuwa kupitia ni matangazo, uwekaji wa bidhaa na matangazo ya mtandaoni katika mitandao ya kijamii.

“Kuongezeka kwa umuhimu wa vyombo vya habari vya kidijitali kunamaanisha kuwa uuzaji wa pombe umezidi kuvuka mipaka", amesema Dag Rekve kutoka Kitengo cha Pombe, Madawa ya Kulevya na Tabia za Kulevya katika shirika hilo la Umoja wa Mataifa la  Afya Ulimwenguni. 

Watu mashuhuri au wenye ushawishi:

Utangazaji unaolengwa kwenye mitandao ya kijamii unakuwa thabiti kwakuwa mbali na kutumia takwimu  na kuifikia jamii husika pia wanatumia washamishi mitandaoni ambao kuweka machapisho katika akaunti zao na hivyo kuifikia jamii.

Ufadhili wa Ligi Kuu:

Ufadhili wa michuano ya ligi kuu za michezo katika viwango vya kimataifa, kikanda na kitaifa ni mkakati mwingine muhimu unaotumiwa na kampuni za kimataifa za pombe. Ufadhili kama huo unaweza kuongeza ufahamu wa chapa zao kwa hadhira mpya. 

Ushirikiano  na vilabu:

Mbinu hii inatumika kati ya makampuni yanayozalisha vileo kushirikiana na ligi za michezo na vilabu mbalimbali ili kuweza kuwafikia watazamaji na watumiaji watarajiwa katika sehemu mbalimbali za dunia.

Kushiriki kwenye matukio ya kijamii na kushawishi wanawake:

Utafiki unaonesha unywaji pombe kwa wanawake ni wa viwango vya chini ( Robo tatu ya wanywaji pombe duniani ni wanaume) na makampuni yamekuja na mbinu mpya za  kuonesha wanawawezesha na kuleta usawa. Kupitia programu za uwajibikaji katika jamii na mada mbalimbali kama vile saratani ya matiti au unyanyasaji wa majumbani makampuni haya yamekuwa yakishiriki ili kukuza kujulikana kwako. 

Serikali lazima zishirikiane katika mbinu za udhibiti wa uuzaji wa pombe 

Kwa mbinu zinazotumika sasa imekuwa ni vigumu zaidi kwa nchi ambazo zinadhibiti uuzaji wa pombe kudhibiti ipasavyo katika mamlaka zao na hivyo ushirikiano zaidi kati ya nchi katika eneo hili unahitajika.

Ingawa nchi nyingi zina aina fulani ya sheria za kudhibiti uuzaji wa pombe, kwa ujumla wake mbinu hizo huwa dhaifu. Katika utafiti wa WHO wa 2018, ilibainika kuwa, wakati nchi nyingi zina aina fulani ya udhibiti wa uuzaji wa pombe katika vyombo vya habari vya jadi, karibu nusu ya nchi hizo hazina udhibiti wa mtandao (48%) na mitandao ya kijamii (47%) ya uuzaji wa pombe.

Ripoti hiyo inahitimisha kwa kuzihimiza serikali za kitaifa kuhakikisha zinajumuisha vikwazo vya kina au marufuku ya uuzaji wa pombe, ikijumuisha vipengele vyake vya kuvuka mpaka ya nchi, katika mikakati yake ya afya ya umma. 
Pia zimekumbushwa kuangazia vipengele muhimu na chaguo za udhibiti wa uuzaji wa pombe kuvuka mipaka na kusisitiza haja ya ushirikiano thabiti kati ya mataifa katika eneo hili.

Kusoma ripoti kamili bofya  hapa