Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shukrani Moldova kwa kufungulia wakimbizi milango licha ya changamoto- Guterres

Kambi ya wakimbizi huko Palanka, nchini Moldova mpakani na Ukraine.
UN News
Kambi ya wakimbizi huko Palanka, nchini Moldova mpakani na Ukraine.

Shukrani Moldova kwa kufungulia wakimbizi milango licha ya changamoto- Guterres

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umesema uko na mshikamano na wananchi na taifa la Moldova kutokana na kitendo chake cha kufungua milango yake na kukaribisha raia takribani nusu milioni kutoka Ukraine wanaokimbia vita nchini mwao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa shukrani alipozungumza na waandishi wa habari kwenye mji mkuu wa Moldova,  Chişinau mkutano ambao umehudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa taifa hilo la Ulaya, Natalia Gavrilița.  

“Niko hapa kwa siku mbili kuonesha mshikamano na kushukuru Moldova kwa mchango wake thabiti katika amani, na ukarimu wa wananchi wake wa kufungua nyoyo na nyumba zao kwa takribani wakimbizi nusu milioni kutoka Ukraine,” amesema Guterres katika mkutano huo uliofanyika baada ya mazungumzo yake na Waziri Mkuu Gravilita.

Ametanabaisha kuwa Moldova kama nchi nyingine inakabiliwa na changamoto za tabianchi, COVID-19 na za kiuchumi lakini hilo halikuzuia ukarimu wa wananchi wake.
 
Katibu Mkuu amesema athari za vita Ukraine zimesambaa kwenye ukanda wa Ulaya na dunia nzima na kueleza wasiwasi wake juu ya hatari ya vita hiyo duniani kote.

“Nina wasiwasi juu ya uwezekano wa vita hii iliyoanzishwa na Urusi inaweza kusambaa dunia nzima sambamba na madhara yake. Nchi kama Moldova, tayari zinahaha kutokana na madhara ya vita hii,” amesema Guterres katika siku hii ya ya leo ya tarehe 9 mwezi Mei ambayo ni tarehe ya kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili barani Ulaya na bara hilo kuibuka mshindi.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (kushoto) akiwa na mwenyeji wake Waziri Mkuu wa Moldova Natalia Gavrilița.
UN /Mark Garten
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (kushoto) akiwa na mwenyeji wake Waziri Mkuu wa Moldova Natalia Gavrilița.

Moldova isaidiwe inaposaidia wengine

Katibu Mkuu amesema ni wakati muafaka kwa jamii ya kimataifa kunyooshea Moldova mkono wake kwa kuwa haina rasilimali za kutosha kusaidia wakimbizi waliomiminika nchini humo.

Moldova si nchi tu ambayo inapokea wakimbizi, bali ni ni nchi ambayo imepokea wakimbizi wengi zaidi kulinganisha na idadi ya wananchi wake.
“Moldova inahitaji na ina haki ya kupata msaada mkubwa kama vile wa bajeti yake, ili uendene na mzigo iubebao au ilingane na ukarimu wake na hivyo basi kuwe na hakikisho la utulivu ndani ya nchi,” amesema Guterres.

Guterres amesema alishuhudia janga la kibinadamu Ukraine kwa macho yake, “lakini kwa kushikamana na wananchi wa Ukraine, Moldova na nchi nyingine Jirani na Ukraine zimechukua hatua za hali ya juu ili kukabili janga hili la kikanda la wakimbizi,”
Katibu Mkuu amekaribisha pia hatua za Moldova na nchi nyingine Jirani za kulinda wakimbizi dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu, ukatili wa kingono na aina nyingine za unyanyasaji.

Moldova hatuna kambi za wakimbizi

Katibu Mkuu amesema kuwa nchini Moldova, haikuwa rahisi kwa Umoja wa Mataifa kuweza kushughulikia wakimbizi. “Hapa hatuna kambi za wakimbizi. Wakimbizi wanaishi na jamii za wenyeji. Hapa hatuna mbinu za kawaida za kusaidia wakimbizi kwenye nchi zinazoendelea au zenye changamoto. Tulilazimika kujipanga upya ili kukidhi mahitaij ya ushirikiano ambao Moldova unahitaji kutoka Umoja wa Mataifa.”
Amesema hata hivyo hivi sasa wanafanya kila wawezalo ili kuweza kuongeza programu za usaidizi hususan ile yenye matokeo ya haraka zaidi ya kutoa fedha taslimu, “kwa sababu ni lazima tuamini kuwa watu wanafahamu mahitaji yao.”

Walengwa wa mradi wa UN

Katibu Mkuu amesema wamelenga kufikia zaidi ya wakimbizi 90,000 wa Ukraine pamoja na raia 55,000 wa Moldova wanaowapatia hifadhi, na watafanya hivyo kwa ushirikiano na serikali na wadau.
Hadi sasa ni nchi 12 zimejiunga na jukwa la Muungano wa Ulaya la usaidizi na tayari nchi hizo zimeahidi kuhamishia wakimbizi kutoka Moldova kwenda kwenye nchi zao.

Bwana Guterres alikuwa awe na mazungumzo na Spika wa Bunge la Moldova Igor Grosu na kisha mlo rasmi wa usiku anaondaliwa na Waziri Mkuu na kesho atatembelea kituo cha wakimbizi kinachoendeshwa kwa msaada na mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Urusi ilishambulia Ukraine tarehe 24 mwezi Februari mwaka huu wa 2022 na hadi leo hii bado vita hiyo inaendelea licha ya wito kutoka kwa nchi, mashirika pakmoja na Umoja wa Mataifa wa kutaka vita hiyo ikome.