Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yatoa msaada wa magari ya kubeba wagonjwa 20 kusaidia sekta ya afya Ukraine

Picha zikionesha mji wa Mariupol nchini Ukraine kabla na baada ya mfululizo wa mabomu.
Vitalii Falkovskyi
Picha zikionesha mji wa Mariupol nchini Ukraine kabla na baada ya mfululizo wa mabomu.

WHO yatoa msaada wa magari ya kubeba wagonjwa 20 kusaidia sekta ya afya Ukraine

Msaada wa Kibinadamu

Katika kusaidia huduma ya afya nchini Ukraine, shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO limetoa msaada wa magari ya kubeba wagonjwa 20 ili kuiwezesha sekta ya afya kutoa huduma katika maeneo yaliyoathiriwa na ambayo hayafikiki kutokana na vita nchini humo.

Msaada huu umekuja kufuatia ziara ya Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ambaye kwa siku tatu alizuru maeneo mbalimbali kujionea uharibifu uliotokea na kufanya mikutano na wadau pamoja na viongozi wa serikali ili kufahamu mahitaji yanayohitajika katika sekta ya afya.

Hatuleti tu vifaa lakini tunatoa msaada kulingana na mahitaji yao. Leo tunawakabidhi  magari 20 ya kubebea wagonjwa, pamoja na jenereta na jokofu za kuhifadhia damu kwa hospitali popote zinapohitajika." Alisema Dk Tedros wakati akimkabidhi funguo Naibu Waziri wa Afya Iryna Mykychak mjini Lviv, Ukraine. Huku akisisitiza  jambo muhimu zaidi wanalotaka kuona likitolekea ni amani.

Baada ya kupokea msaada huo Naibu waziri Mykychak alisema wanafurahi kuunganisha nguvu na wadau mbalimbali wa kimataifa ili kusaidia kutoa huduma ya matibabu na uokoaji.

“Magari haya ya kubebea wagonjwa yanaweza kuelekea katika maeneo muhimu zaidi, hata pale ambako barabara zimeharibiwa zaidi. Tunashukuru sana washirika wetu wote wa kimataifa kwa msaada huu muhimu kwa Ukraine.”

Katika kipindi cha miezi miwili ya vita, miundombinu ya matibabu nchini Ukraine imeharibiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya huduma za afya, na upatikanaji wa huduma za afya katika maeneo mengi umeathiriwa sana. Mchango huu wa magari 20 utasaidia kuleta huduma muhimu ya kuokoa maisha kwa watu nchini Ukraine na kuboresha huduma za afya.

Mwakilishi wa WHO na Mkuu wa Ofisi ya Nchi ya WHO nchini Ukraine Dkt. Jarno Habicht akisimulia umuhimu wa usafiri amesema. “Mmoja wa wahudumu wa afya tuliozungumza naye alikumbuka jinsi siku za mashambulizi ya mara kwa mara katika jiji lao, magari ya kubebea wagonjwa yaliendelea kufanya kazi hata wakati wa amri ya kutotoka nje ili kuhakikisha watu wanapata huduma wanayohitaji. Tumetiwa moyo na ujasiri wa wafanyakazi wa afya wa Ukraine na tunatumai mchango huu utachangia kazi yao.”

WHO hadi sasa imewasilisha tani 393 za vifaa vya dharura na matibabu, na vifaa tiba kwa nchi ya Ukraine. Kati ya kiasi hicho, tani 167 zimefikishwa mahali zilipokusudiwa, hasa mashariki, kusini na kaskazini mwa nchi ambako uhitaji ni mkubwa zaidi.