Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa UN wa kukabiliana na hali ya jangwa wang’oa nanga Abidjan

Picha iliyopigwa angani ikionyesha wilaya ya Plateau mji wa Abidjan nchini Côte d'Ivoire.
UN Photo/Basile Zoma
Picha iliyopigwa angani ikionyesha wilaya ya Plateau mji wa Abidjan nchini Côte d'Ivoire.

Mkutano wa UN wa kukabiliana na hali ya jangwa wang’oa nanga Abidjan

Tabianchi na mazingira

Takriban asilimia 40 ya ardhi isiyo na barafu kwa sasa imeharibiwa na matokeo mabaya ya mabadiliko ya tabianchi, viumbe hai na uchumi.  

Tatizo hili linajadiliwa na washiriki wa kikao cha 15 cha mkutano wa nchi wanachama wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na kuenea kwa Jangwa, COP15 ulioanza leo mjini Abidjan, nchini Côte d'Ivoire. 

Maudhui ya mkutano huo ni “Dunia, maisha, urithi: Kutoka uhaba hadi ufanisi.” Ni wito wa kuchukua hatua unaolenga kufufua na kuhifadhi ardhi kwa ajili ya vizazi vijavyo hasa mifumo ya ikolojia ya nchi kavu kama vile ardhi ya kilimo, nyasi, misitu, ardhi oevu na maeneo mengine muhimu. 

Mkutano huo umeanza kwa kikao cha kilele cha wakuu wa nchi na viongozi wa ngazi za juu ili kutoa msukumo wa kisiasa katika juhudi za kuzuia uharibifu wa ardhi unaotokea kwa sababu ya mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu. 

Asilimia 40 ya udongo wote duniani umeharibiwa 

 Hadi sasa, asilimia 40 ya udongo wote duniani kote umeathiriwa na mmomonyoko wa udongo, kuziba na chumvi, uchujaji wa vitu vya hewa ukaa, atindikali, uchafuzi wa mazingira, kugandamiza udongo na madhara mengine. 

Akihutubia mkutano huo, Rais wa kikao cha 76 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Abdullah Shahid amesisitiza kuwa juhudi za kurejesha mifumo ya ikolojia zitasaidia kurejesha uwezo wa ardhi wa kuhifadhi hewa ukaa na kupunguza utoaji wa gesi chafuzi, kuzuia kupungua kwa kasi kwa mimea na wanyama, kuongeza rutuba ya udongo na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na uhaba wa maji. 

Ameongeza kuwa "Kwa kufikia lengo la kukarabati duniani kote ardhi iliyoharibiwa, tutaweza kuhifadhi tani bilioni tatu za hewa ukaa ya angani kwenye udongo kila mwaka. Hili lingeweza kupunguza takriban asilimia 10 ya uzalishaji wa sasa wahewa ukaa itokanayo na nishati kwa mwaka. Kwa kuchukua hatua za kuzuia, kupunguza na kurudisha nyuma uharibifu wa ardhi, tunaweza kuchangia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, jambo ambalo ni muhimu ili kuhakikisha kuwa kasi ya ongezeko la joto duniani haizidi nyuzi joto mbili ifikapo mwaka 2030.” 

Abdullah Shahid pia amekumbusha kuhusu tangazo la Baraza Kuu la Umoja wa Mastaifa kuhusu muongo wa urejeshaji wa mfumo wa ikolojia. 

Kukarabati ekari bilioni moja za ardhi iliyoharibiwa ifikapo 2030 

Washiriki wa mkutano huu wanajadili njia za kurejesha katika ubora ekari bilioni moja za ardhi iliyoharibiwa ifikapo 2030, kuboresha ufanisi wa matumizi ya ardhi ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, na kukabiliana na hatari zinazoongemoto wa nyika. 

Mkutano huo utakaokamilika Mei 20, unahudhuriwa na wakuu wa nchi na serikali zaidi ya 12, mawaziri na wajumbe wasiopungua 2,000 kutoka nchi 196 na Muungano wa Ulaya EU.  

Miongoni mwa washiriki wa mkutano huo ni Amina J. Mohammed, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Mkutano wa 15 wa nchi zinazoshiriki ni mkutano wa kwanza kati ya mikutano mitatu ya mikataba ya Rio itakayofanyika mwaka 2022, kukiwa na kongamano la bioanuwai na kongamano la mabadiliko ya tabianchi litakaloitishwa baadaye Kunming, China na Sharm el-Sheikh, Misri.