Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Merankabandi imenikomboa mimi na familia yangu: Mfinyanzi Nduwimana

Wanawake Burudi wakitifua udongo kwa jembe katika maandalizi ya kupanda.
©FAO/Giulio Napolitano
Wanawake Burudi wakitifua udongo kwa jembe katika maandalizi ya kupanda.

Merankabandi imenikomboa mimi na familia yangu: Mfinyanzi Nduwimana

Ukuaji wa Kiuchumi

Kutana na mfinyanzi Nduwimana Cornalie kutoka nchini Burundi ambaye maisha yake yalikuwa duni, akishindwa kukidhi mahitaji ya msingi ya familia ikiwani pamoja na kuweka mlo mezani na hata kupeleka wanawe shule, lakini sasa asante kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF lililoanzisha mrandi wa Merankabandi wa kusaidia familia duni kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, maisha yake na ya jamii yake yamebadiliaka.

Mfinyanzi Nduwimana Cornalie anayeishi katika eneo la Butaganzwa jimbo la Ruyigi Nchini Burundi akisema kabla ya kujiunga na mradi wa Merankabandi maisha yake na familia yake yalikuwa ya dhidi sana, “kama mfinyanzi niliishi kwa kutegemea ufinyanzi wa asili ambapo vyungu na mitundi niliyofinyanga haikunisaidia chochote. Maisha yalikuwa magumu , tulipata fedha kidogo sana” 

Lakini kama wasemavyo wahenga Mungu si Athumani Nduwimana akapata Habari za mradi wa Merankabandi na kuamua kujiunga nao, mradi ambao hadi sasa unasaidia kaya 56,090 zisizojiweza nchini Burundi,  hii inamaanisha karibu watoto 280,000 pia wanafaidika , na Nduwimana na familia yake wakiwa miongoni mwao. 

Mnufaika mwingine ni Nimfasha Consolate pambaye alikuwa mkimbizi kwa muda mrefu lakini sasa amerejea Butaganzwa h na anafanya biashara ya kupika na kuuza mandazi anasema,”kupokea fedha bila mafunzo haisaidii sana lakini kupitia mradi huu tumejifunza jinsi ya kuzitumia vyema fedha hizo na hiyo imetusaidia kupata faida ya fedha tulizopewa. Ninachukua mkopo na naweza kuulipa bila matatizo. Na leo hii tunajivunia kwamba tuna mradi unaotuletea pesa, tuna chakula na tunamudu kujikimu kimaisha.” 

Kwa Nduwimana ambaye kupitia mradi huu ameyapa kisogo matatizo yake, na kumudu kupeleka watoto wake shuleni hana kingine isipokuwa shukrani kwa UNICEF na Benki ya Dunia, “tunashukuru kwa mradi wa Merankabandi tumejifunza njia za kisasa za kufinyanga vyungu. Tunatengeneza vyungu vya maua, vyungu hivyo ambavyo awali tulikuwa tunauza Faranga za Burundi 100 au 200, sasa kwa faida kubwa tunaviuza kwa Faranga 5,000 na 10,000” 

Mradi huo ambao ulizinduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017, uko katika nchi nzima na lengo lake kuu ni kutumika kama ulinzi wa hifadhi ya jamii kwa familia zisizojiweza kwa kuwawezesha kwa miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na biashara za ujasiriamali, kilimo, na hata ufugaji wa mbuzi, ng’ombe na kuku.