UN yatoa dola za Marekani milioni 19 kusaidia watu nchini Sudan Kusini kujiandaa na mafuriko makubwa 

7 Mei 2022

Dola za Marekani milioni 19 zimetolewa kusaidia jamii nchini Sudan Kusini kujiandaa na mafuriko makubwa yanayotarajiwa wakati wa msimu wa mvua zimetolewa. 

Mfuko wa Kibinadamu wa Sudan Kusini (SSHF) na mfuko wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya dharura (CERF) wametoa pesa hizo kabla ya mafuriko kutokea ili kuepusha janga la kibinadamu. 

“Sudan Kusini inatarajiwa kukumbwa na mafuriko makubwa kwa mwaka wa nne mfululizo katika miezi ijayo.” Imeeleza taarifa ya OCHA iliyotolewa Jumamosi ya leo. 

Ufadhili huo utakwenda kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kuandaa na kuwalinda watu katika kambi ya Bentiu kwa ajili ya wakimbizi wa ndani na maeneo jirani katika Jimbo la Unity, ambayo ni miongoni mwa maeneo yaliyo katika hatari ya mafuriko makubwa. 

Kwa mujibu wa Kituo cha Takwimu za Kibinadamu, mvua nchini Sudan Kusini zikianza tena, maeneo makubwa ya ardhi katika maeneo haya bado yana maji kutokana na msimu wa mvua uliopita. Huku viwango vya maji vya juu ya mto bado vikiwa juu, hata mvua chache zinaweza kusababisha mafuriko katika mashamba, kusomba makazi na kuzidisha magonjwa yanayotokana na maji. 

Katika Jimbo la Unity, mafuriko yanayotarajiwa yanaweza kuweka zaidi ya watu 320,000, zaidi ya theluthi moja ya ambao tayari wameyahama makazi yao  katika hatari ya kuhama zaidi, kupoteza maisha, milipuko ya magonjwa na uhaba wa chakula. 

Kiasi cha dola milioni 4 za fedha za SSHF zitawezesha NGOs na mashirika ya Umoja wa Mataifa kuimarisha mitaro karibu na barabara muhimu, makazi ya watu waliofurushwa, uwanja wa ndege na miundombinu mingine. Mgao wa CERF wa dola milioni 15 utasaidia watu kulinda nyumba zao na miundombinu muhimu, kama vile vyoo na visima vya maji, kutokana na maji ya mafuriko, na hivyo kulenga kuepusha dharura ya afya ya umma. 

"Miaka mitatu ya mafuriko ambayo hayajawahi kushuhudiwa imeharibu maisha ya watu," amesema Sara Beysolow Nyanti, Mratibu wa Kibinadamu kwa Sudan Kusini akiongeza kuwa "msimu wa mvua unapoanza, ufadhili huu utawezesha mashirika ya kibinadamu kupunguza pigo la mgogoro mwingine kwa kuandaa na kulinda jamii huko Bentiu mapema." 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter